WACHEZAJI 13 wameripoti kwenye
mazoezi ya Simba SC jioni hii, wakiwemo Kiggi Makassy aliyesajiliwa kutoka kwa
mahasimu, Yanga ingawa mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Dong Tam Long An ya
Vietnam, Danny Davis Mrwanda hakutokea.
Mashabiki wengi wa Simba
walifika mapema Uwanja wa TCC Chang’ombe, Dar es Salaam jioni hii kuwashuhudia
wachezaji wao, kiu zaidi ikiwa kumuona mpachika mabao wao wa zamani, aliyerejea
kikosini Mrwanda, lakini Meneja wa Simba, Nico Nyagawa akaiambia BIN
ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo ni miongoni mwa waliotoa
udhuru.
Waliohudhuria ni pamoja na
Salim Kinje, Abdalllah Juma, William Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun
Athumani, Haruna Shamte, Amri Kiemba, Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu
Mbivayanga na Abdallah Seseme.
Mazoezi hayo yaliongozwa na
Kocha wa Mazoezi ya Viungo, Mganda Hamatre Richard kwa sababu Kocha Mkuu,
Mserbia Milovan Cirkovick bado anakula sikukuu kwao.
Simba itaendelea na program ya
mazoezi kwa jioni tu wiki hii na Nyagawa amesema anatarajia idadi ya wachezaji
itakuwa ikiongezeka taratibu wiki hii, wakiwemo wachezaji waliokuwa na timu ya
taifa Msumbiji nao pia wanatarajiwa kuungana na wenzao wakirejea kutoka nchini
humo.
Mrwanda ambaye amesaini
mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Simba, ambao hauna kipengele cha kumruhusu
kuuvunja kabla haujamalizika naye anatarajiwa kuanza maozezi wakati wowote wiki
hii.
Mrwanda, awali ilielezwa
anataka kusaini mkataba ambao wakati wowote akipata timu nje, aondoke, lakini
kwa mujibu wa mkataba aliosaini Simba ni kwamba akipata timu italazimika
kumnunua kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi, au isubiri hadi amalize
mkataba.
Habari za uhakika, kutoka
ndani ya Simba SC ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba
Mrwanda ameridhika na mkataba huo na ameahidi kufanya vitu baab kubwa
Msimbazi.
Kwa
upande mwingine, Simba SC imeamua kumtema kiungo Salum Machaku kwa makubaliano
maalum ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba. Simba ilitaka kumtoa kwa mkopo
Machaku, lakini mwenyewe akasema bora aachwe moja kwa moja.
Tayari Simba imemsajili kiungo
wa Yanga, Kiggi Makassy kuziba nafasi ya Machaku. Machaku sasa ameingia kwenye
mazungumzo na Yanga.
Simba SC inajiandaa na
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayotarajiwa
kuanza Julai 14 hadi 29, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Timu nyingine za
Tanzania zitakazoshiriki michuano hiyo ni mabingwa watetezi, Yanga na washindi
wa pili wa Ligi Kuu Azam FC.
Azam pia wameshaanza kujifua
kwenye Uwanja wao wa Chamazi, wakati Yanga wanatarajiwa kuanza kesho Uwanja wao
wa Kaunda, Jangwani, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment