Mwenge wa Uhuru ukiwasili katika kiwanda cha kutengeneza chupa za maji ya Ndanda Springs, kilichopo katika kata ya Mwena, wilayani Masasi, kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi |
Burudani ya asili |
Vijana wakiwa nje ya kiwanda cha kutengeneza chupa za maji ya kunywa ya Ndanda Springs, wakisubiri msafara wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho. |
Na Juma Mohamed, Masasi.
WANANCHI wa
kata ya Mwena wilayani Masasi wameonesha kuwa na matumaini makubwa ya kujipatia
ajira kufuatia ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza chupa za maji safi na salama
ya Ndanda Springs kinachojengwa katani hapo ambacho kimewekwa jiwe la msingi na
mbio za Mwenge wa Uhuru.
Wakizungumza
na Nipashe, walisema kwa sasa vijana wengi wanakabiliwa na changamoto za
ukosefu wa ajira kiasi cha kupelekea kuona maisha magumu lakini uwapo wa
kiwanda hicho utawakomboa kuondokana na hali hiyo .
“Ninafurahi
kuanzishwa kwa kiwanda hiki maana kitasaidia kupatikana kwa ajira, vijana wengi
tunakaa hatuna kazi, kwahiyo baada ya kufunguliwa hapa nafikiri ajira zitakuwa
nyingi baadhi ya ukali wa maisha utapungua..pia tunatarajia maji yatapatikana
kwa wingi na hata bei itakuwa nafuu kwakua yatakuwa yanazalishwa kwa wingi na
chupa zinapatikana karibu hapahapa..” alisema Marun Majogo.
Naye,
Costantino Daudi ambaye ni wakala wa kuuza maji ya Ndanda Springs, alisema
kukamilika kwa kiwanda hicho kutawasaidia kuweza kununua maji kwa bei nafuu
jambo litakalowafanya na wao waweze kuuza kwa nafuu kwa wateja wao.
Akisoma
taarifa ya kiwanda hicho kwa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, George
Mbijima, mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho kutoka kitengo cha uzalishaji,
Romanus Mpanda, alisema sambamba na ujenzi huo, kipo kiwanda kingine cha
kuzalisha maji safi na salama ya kunywa cha Ndanda Springs.
“Kiwanda
hiki cha kuzalisha maji safi ya kunywa kina wafanyakazi 100 wazalendo ambao
wengi wao ni vijana wakiume na wakike ambao wametoka katika jamii inayozunguka kiwanda
hiki..katika wafanyakazi hao 100, wafanyakazi wakike wapo 61 na wakiume 39..”
alisema Mpanda.
Vijana wakiwa nje ya kiwanda cha kutengeneza chupa za maji ya kunywa ya Ndanda Springs, wakisubiri msafara wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho. |
Meneja
uzalishaji wa kiwanda cha Ndanda Springs, Benedict Macheso, alikiri kuwapo kwa
fursa za ajira katika kiwanda hicho cha chupa ambacho ujenzi wake mpaka
ulipofikia umegharimu sh. Bilioi 1.08 na kutarajiwa kumalizika katikati ya
mwezi Septemba mwaka huu
Kwa upande
wake, kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima, aliwataka vijana
watakaopata nafasi za kuajiriwa kiwandani hapo kufanya kazi kwa juhudi na kuwa
waaminifu ili kampuni ipate mafanikio ambayo yatasababisha fursa ya kuongeza
viwanda vingine.
“Tufanye
kazi kwa bidii ili apate faida, tusipowajibika yeye ana uhuru na wala hafungwi
kutafuta wafanyakazi kutoka sehemu nyingine yoyote ya nchi ambao watakuwa
tayari kufanya kazi, sasa vijana wenzangu wa hapa tusikubali tukapoteza nafasi
hii..tunapopata nafasi tufanye kazi kwa manufaa binafsi lakini tumsaidie ndugu
yetu ili aweze kufungua viwabda vingi zaidi..” alisema Mbijima.
No comments:
Post a Comment