Friday, June 3, 2016

MTPC yamlilia katibu mkuu wizara ya habari, mikataba kwa waandishi.




Katibu mkuu wa wizara ya habari, sanaa, utamaduni na michezo, Prof. Elisante Gabriel, akisaini katika daftari la wageni baada ya kutembelea ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), kusikiliza maoni na changamoto za wanahabari. Kulia ni mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Simba.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo (MTPC), kimemuomba katibu mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Gabriel, kuwashinikiza waajiri kuwapatia mikataba waandishi wa mikoani ili kulinda masilahi yao na kutatua baadhi ya changamoto za kimkataba wanazokabiliana nazo.
Akizungumza katika ofisi ya chama hicho ambako katibu mkuu alitembelea kwa ajili ya kusikiliza maoni na changamoto za wanahabari ikiwa ni sehemu ya ziara yake, mwenyekiti wa chama hicho Hassan Simba, alisema changamoto nyingine walizomweleza ni pamoja na waandishi kutokuwa na vitambulisho maalumu (Press Card) kutoka wizara ya habari vitakavyowawezesha kufanya kazi zao mahala popote nchini.
“Kwanza ni suala la mikataba kwa wafanyakazi wanaofanya kwenye vyombo mbalimbali, kwamba hawa wawe na mikataba ambayo inaeleza wazi masialahi yao na mambo yao mengine yanayotakiwa kufanywa pamoja na yale makato kwa ajili ya mifuko ya uzeeni..” alisema na kuongeza;
“Lakini jambo jingine tumeona hapa waandishi wetu wamekuwa wakifanya kazi bila kuwa na ‘Press Card’ yani kile kitambulisho maalumu kinachotolewa na wizara ya habari kwa ajili ya kufanya kazi popote Tanzania” aliongeza Simba.

Elisante Gabriel na Hassan Simba



Hata hivyo, Simba hakusita kutoa shukrani zake kwa niaba ya chama hicho kufuatia kukabidhiwa iPad moja ambayo itasaidia katika mawasiliano baina ya chama na wizara juu ya masuala mbalimbali ya kiutendaji.
 Kwa upende wake, katibu huyo aliahidi kuyafanyia kazi maombi yaliyowasilishwa kwake pamoja na suala la ufadhili kwa wanahabari wanaohitaji kwenda masomoni kuongeza taaluma zao.
“Kilichonifurahisha kuliko vyote ni kitendo cha nyie kusema sio tu kwa vile wewe umesomea habari na ujue tu kuandika..lakini nafikiri bado mungeweza kuandika kwa Mhe. Nape (Waziri wa Habari, sanaa, utamaduni na michezo), na mimi nitamfikishia na maelezo ya ziada, na nyinyi baada ya kupanda basi kupeleka Dar es Salaam mfikishieni zawadi kwa kumtumia andiko leo (jana) ili kesho (leo) na mimi nikifika ofisini nivione alafu tuweze kuvifanyia kazi..” alisema.

Katibu mkuu wa wizara ya habari, sanaa, utamaduni na michezo, Prof. Elisante Gabriel, akimsikiliza mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), Hassan Simba.



Aidha, alikabidhi iPad moja kwa uongozi wa MTPC ambayo itasaidia katika mawasiliano baina ya MTPC na wizara juu ya masuala mbalimbali ya kiutendaji pale inapobidi.
Ziara ya katibu mkuu huyo mkoani Mtwara ilikuwa na lengo la kuitoa wizara jijini Dar es Salaam na kuipeleka mikoani kwa ajili ya kupata maoni na changamoto kutoka kwa wadau.


Unaweza kushea na wengine habari hii..

No comments: