Sunday, June 12, 2016

Wananchi Mtwara waanzisha miradi kupitia mpango wa TASAF.





Baadhi ya wakazi wa kata ya Ziwani, wakisubiri kupatiwa fedha za kujikimu zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini.



Mnufaika wa TASAF akitoka kupatiwa fedha kutoka kwa wawezeshaji.


Mmoja wa wazee wa kijiji cha Nambeleketela, kata ya Ziwani halmashauri ya wilaya ya Mtwara, akipokea fedha za kujikimu kutoka kwa wawezeshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)



Na Juma Mohamed, Mtwara.
Wananchi wa kijiji cha Nambeleketela tarafa ya Ziwani, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, wamefanikiwa kuanzisha miradi ya ufugaji na kuwatimizia mahitaji ya shule watoto wao kutokana na kupatiwa fedha za msaada kupitia mpango wa TASAF wa kunusuru kaya masikini.
Wakizungumza kijijini hapo wakati wa kupokea fedha hizo, walisema mpango huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa hali ngumu ya maisha ambayo walikuwa wakikabiliana nayo huku wengine wakiiomba serikali kuzidi kuuboresha na kuongeza muda zaidi.
“Kwavile msaada huu ninaoupata unanisaidia, unanisaidia kwasababu kwamba sioni alafu mahala kama nilikuwa na nyumba yangu mbaya mbaya mungu amenijaalia upande mmoja nimepata mtu wa kunijengea lakini upande mwingine sijamaliza..naiomba wazidishe msaada..” alisema Hassan Makini, mkazi wa Nambeleketele.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Ziwani, wanaotoka katika kaya masikini wakipatiwa fedha kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)



Naye, Hashim Meshetwe ambaye alimwakilisha mama yake alisema, tayari mzazi wake huyo ameanzisha mradi wa kufuga kuku lakini kabla ya kupata mgao huo alikuwa katika hali mbaya ya kifedha kwahiyo aliwashukuru wawezeshaji kwakua fedha hizo zimesaidia kutatua baadhi ya mahitaji muhimu katika kipindi hiki cha mfungo wa Radhamn.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Mahamudu Ally, aliishukuru serikali kupitia mpango huo ambao unaelekea kufikia mwisho kwa kuweza kuwakomboa wananchi wake, huku mwezeshaji wa mpango huo Agatha Tembo, amewataka wanufaika na mpango huo kutumia fedha wanazozipata katika kuwekeza katika mitaji itakayowasaidia baadae pale mpango huo utakapofikia mwisho.
Jumla ya kaya 121 zimepata mgao wa fedha hizo katika kijiji hicho kupitia mpango huo ambao unatekelezwa kwa miaka mitano kwa kila awamu.

No comments: