Na Juma Mohamed, Mtwara.
MAHAKAMA kuu
kanda ya Mtwara imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la
Newala mjini katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana,
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF)
Juma Manguya dhidi ya mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Mhe. George Mkuchika.
Akisoma
hukumu ya kesi hiyo iliyosikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Newala, Jaji wa
mahakama kuu ya Tanga, Amour Khamis, alisema maamuzi hayo yametokana na
mlalamikaji kushindwa kuthibitisha katika kesi yake kwa kiwango stahiki kwamba
uchaguzi huo haukuendeshwa kwamujibu wa sheria, huku walalamikiwa wakitoa
ushahidi wa kutosha.
Kesi hiyo
namba 1 ya uchaguzi mwaka 2015 ambayo hukumu yake ilianza kwa kusomwa madai
yote 13 ambayo yaliwasilishwa na mlalamikaji kabla ya kutolewa maamuzi, ilikuwa
katika hali ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi huku ikishuhudiwa askari wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakizunguka barabarani na gari lao.
Akizungumza
baada ya kutolewa hukumu hiyo, Manguya ambaye madai yake yote 13 aliyowasilisha
mahakamani hapo yamekataliwa, alisema hakubaliani na maamuzi hayo na kwamba
atakaa na jopo lake ili waweze kukata rufaa.
“Tutakaa na
wakili wangu kuangalia zile hoja tatu, ipo hoja ambayo sisi tuna pakupitia
ambayo tutakwenda tukae na mawakili tuweze kwenda mbele zaidi..na nachukua
nafasi hii kama nilivyotangulia mwanzo kutoka mahakamani kuwataka wale wafuasi
wetu wa UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) na Chama cha Wananchi CUF wawe
watulivu hapa sio mwisho tutaendelea mbele mpaka pale haki itakapopatikana..”
alisema Manguya.
Wakili wa
Manguya aliyekuwa akimsimamia katika kesi hiyo, Rainery Songea, ameahidi kwenda
kudai nakala ya hukumu ili aipitie vizuri kabla ya taratibu za kukata rufaa.
“Nimemsikiliza
Jaji kwa makini na nimeona maamuzi yake yalivyo, kimsingi mimi kama wakili kitu
ambacho nataka nikifanye kwanza nataka niombe ‘copy’ (Nakala) ya hiyo hukumu noisome
kwa makini lakini pia kwa jinsi nilivyomsikiliza naona kuna kuna vitu Fulani
ambavyo vina haja ya kuvikatia rufaa..” alisema.
Kwa upande
wake, mshindi katika kesi hiyo, George Mkuchika, aliishukuru mahakama kwa
maamuzi hayo na kuahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo lake bila ubaguzi.
“Mimi nataka
kusema tu kwamba nashukuru maamuzi ya mahakama nimeyapokea kazi iliyobaki
kwangu sasa hivi ni kuwatumikia wananchi wa Newala wote bila kubagua
walionipigia kura na ambao hawakunipigia kura..” alisema.
Naye wakili
wake Hussein Mtembwa ambaye ni wakili wa kujitegemea aliwataka wafuasi wa
Mkuchika kusherehekea ushindi kwa amani na utulivu huku akiwashukuru wadau
waliohusika katika kufanikisha ushindi huo pamoja na mahakama kwa kutenda haki.
“Nichukue nafasi
hii kuwashukuru wadau wote ambao wamehusika muda wote wa kesi ikiwa ni pamoja
na mahakama kwa lile suala moja tu la kutoa haki..sasa kwaniaba ya Mbunge nitoe
rai tu kwa wale wafuasi wa Mhe. Mkuchika washerehekee ushindi huu kwa amani na
utulivu kabisa..” alisema.
Mahakama
hiyo ilimtaka mlalamikaji Juma Manguya, kumlipa mlalamikiwa George Mkuchika
gharama zote alizotumia wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo ambapo hata hivyo
imempa nafasi ya kuendelea kukata rufaa iwapo hatoridhika na maamuzi.
………………………………………..mwisho……………………………………….
No comments:
Post a Comment