Tuesday, July 15, 2014

RODRIGUEZ AFURAHIA 'DEAL' LA KUJIUNGA NA MADRID

James Rodriguez
Na Juma Mohamed

James Rodriguez mnamo Jumapili alijishikia vyema nafasi yake kama mmoja wa nyota waliochipukia katika Kombe la Dunia huku ripoti zikisema Real Madrid wanamtaka straika huyo wa Colombia.
“Ninaweza kufurahia sana fursa ya kwenza Real Madrid," Rodriguez aliambia gazeti la michezo la Uhispania la Marca siku ambayo mabao yake sita yalimfanya awe mshindi wa Golden Boot Kombe la Dunia. Tuzo hiyo hukabidhiwa mfungaji wa mabao mengi zaidi.
"Imekuwa ndoto yangu maishani na ikitimia, ninataka kuifurahia,” akaongeza Rodriguez, aliyetimiza miaka 23 Jumamosi.
Colombia walibanduliwa walipolazwa robofainali Kombe la Dunia nchini Brazil. Hakuna mwingine – hata Thomas Mueller wa Ujerumani au Lionel Messi wa Argentina – aliyemfikia licha ya kucheza mechi zaidi.
Bingwa wa dunia wa Ujerumani Mueller alimaliza wa pili na mabao matano. Messi, nyota wa Brazil aliyejeruhiwa Neymar na straika wa Uholanzi Robin van Persie, walishikilia kwa pamoja nafasi ya tatu na mabao manne.
"Nawashukuru sana nyote kwa uungaji mkono wenu na kwa wachezaji wenzangu kwa kufanikisha hili,” Rodriguez alisema kupitia akaunti yake ya Twitter. Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na wachezaji wenzake walimmwagia sifa na pongezi.
Miongoni mwa mabao hayo nusu dazani ya Rodriguez ni bao la kishua la kutuliza kwa kifua na kutoa kombora kali dhidi ya Uruguay, mojawapo ya mabao bora zaidi ya dimba hilo.
Fowadi huyo wa Monaco, aliyeingia kujaza pengo lililoachwa na Radamel Falcao aliyeumia, pia alifunga wakati wa kushindwa kwao 2-1 na Brazil.
Alipata bao la pili dhidi ya Uruguay katika mechi ya 16 bora, na moja katika kila mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Ivory Coast, Ugiriki na Japan.
Rodriguez aliondoka uwanjani akitiririkwa na machozi baada ya kushindwa na Brazil. Lakini amekuwa mmoja wa wachezaji wanaosakwa zaidi katika soka.
Klabu ya Monaco ililipa Porto ya Ureno €45 milioni mwaka mmoja uliopita. Ripoti katika vyombo vya habari zinasema wameitisha mara dufu kutoka kwa wanaotaka kumchukua.
Rais wa Real Madrid Florentino Perez tayari anashauriana na mwenzake wa Monaco Dimitry Rybolovlev, kwa mujibu wa Marca.
Gazeti hilo la Uhispania lilisema Real wameteremsha bei yake hadi €85 milioni.

SOURCE: SUPER SPORT

No comments: