Saturday, September 8, 2012

AZAM YAMPASUA KICHWA MILOVAN, ASEMA JUMANNE LAZIMA KIELEWEKE

 



Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic
Na Calvin Kiwia KOCHA wa Simba, Milovan Cirkovic amepigwa butwaa na kutamka kuwa hafahamu kilichowakuta mabeki wake wapya wa kati, Paschal Ochieng na Komanbilli Keita lakini akatamka kwamba watakapokutana na Azam, Jumanne itakuwa ni habari nyingine.
Milovan alikiri kwamba katika mechi zote nne za kirafiki alizocheza dhidi ya Mathare United, JKT Oljoro zote ikishinda mabao 2-1 na Sony Sugar aliyotoka nayo sare ya bao 1-1 hazifikii ugumu wa Sofapaka iliyowakung'uta Wekundu hao mabao 3-0 juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
"Kwenye mechi ya Ngao ya Hisani na Azam hatuwezi kucheza hivi, itakuwa ni stori tofauti kabisa. Mnatakiwa kujua kwamba Sofapaka ilikuwa mechi yetu ya kwanza tangu tutoke kambini Arusha na sikuridhika na hali halisi.
"Mambo yatakuwa tofauti tunaingia kuikabili Azam kwa mtazamo tofauti kwa kuwa tunaingia kwenye mashindano ya msimu huu," alisisitiza kocha huyo ambaye kwenye kambi ya wiki tatu jijini Arusha aliridhishwa na kazi ya safu yake ya ulinzi na kutamka kwamba Simba haina tatizo kwenye safu hiyo hasa kwa ujio wa Ochieng na Keita.
"Timu yangu nimeifanyisha mazoezi kwa muda mrefu ninaijua na nafikiri kila mmoja yupo tayari kwa mashindano, ingawa kuna matatizo yaliyoonekana kwenye safu ya ulinzi katika mechi na Sofapaka. Siwezi kumlaumu Juma Kaseja isipokuwa Ochieng na Keita walishindwa kuelewana, sielewi tatizo nini wakati kwenye mechi za nyuma wamecheza vizuri.
"Ukifuatilia mabao yote matatu tuliyofungwa yalitokea kushoto na kwao, ni tatizo ambalo halikuwapo mechi zilizopita," alisema Milovan ambaye amepania kushinda mechi zote msimu huu na kutetea ubingwa bila kupoteza mchezo.
Katika mchezo wa juzi Alhamisi, beki Pascal Ochieng alianzishiwa mpira na Juma Kaseja lakini akajisahau na kujikuta adui akiwa ameshamfikia. Alifanya uamuzi wa haraka na kutoa mpira huo kuwa kona iliyozaa penalti baada ya beki Keita kuunawa akiwa katika harakati za kuosha.
Mkenya John Baraza alifunga mkwaju huo katika dakika ya 18.
Straika huyo wa zamani wa Yanga alitumia tena akili na kupachika bao la pili dakika ya 57, akiunganisha pasi ndefu ya Joseph Nyaga akiwa katikati ya Ochieng na Keita kwa kunyanyua mpira huo uliopita juu ya Kaseja na kutinga wavuni.
Kiungo Joseph Nyaga aliunganisha krosi safi kutoka winga ya kulia, akiwa na Ochieng mwenye mwili mkubwa kama straika wa Azam, Gaudence Mwaikimba.
Straika wa Simba, Mghana Daniel Akuffo alicheza dakika 35 na akaumia na kushindwa kuendelea.

No comments: