Riphati Khamisi akiwa na tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Novemba wa VPL |
Juma Mohamed, Mtwara
Wekundu wa
Msimbazi Simba Sc leo wamefanikiwa kurejea kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania
Bara na kuwashusha Yanga waliokaa kwa saa kadhaa, baada ya kuwasambaratisha
Ndanda FC ya Mtwara kwa jumla ya mabao 2-0 katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Simba
wanaonolewa na Joseph Omog, walicharuka zaidi kipindi cha pili cha mchezo huo
baada ya kushindwa kuliona lango katika dakika 45 za kipindi cha kwanza,
ambacho Ndanda walishuhudiwa wakifika langoni mwa Simba mara kadhaa bila
mafanikio.
Alikua ni
Mzamiru Yasin alieanza kupeleka kilio kwa wanakuchele katika dakika ya 63,
baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mohamed Ibrahim, ambaye baadaye dakika ya 81
alishindilia msumari wa mwisho langoni mwa Ndanda.
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi hiyo, walimkabidhi mshambuliaji kinda wa Ndanda FC Riphati Khamisi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 1 ikiwa ni tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Novemba wa VPL.
Simba sasa
inafikisha alama 38 baada ya kucheza michezo 16 na kuongoza ligi kwa alama
mbili nyuma ya Yanga, huku Ndanda wakisalia na alama zao 19.
No comments:
Post a Comment