Wakazi wa kata ya Naliendele waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Mtwara mjini (CUF), Maftaha Nachuma, uliokuwa na lengo la kuwapongeza wapiga kura wake kwa kumchagua kuwa mbunge. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
MBUNGE wa
Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, amesema iwapo
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litashindwa kufikisha umeme katika maeneo
yaliyosalia katika jimbo lake mpaka kufikia mwezi Julai mwaka huu, zitatumika
nguvu za umma kwa kufanya maandamano kudai huduma hiyo.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Naliendele wa kuwapongeza wapiga kura
wake kwa kumchagua kuwa mbunge, alisema hatua inatokana na ahadi iliyotolewa na
serikali kupitia bodi ya TANESCO ambapo iliahidi kumaliza kero ya kukosa
miundombinu ya umeme kwa maeneo yaliyobaki katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ifikapo
mwezi Julai mwaka huu.
“Ni ahadi ya
serikali kupitia bodi ya TANESCO Tanzania, bodi ya TANESCO Tanzania imahidi ya
kwamba ifikapo mwezi wa saba kila kona ya Mtwara mjini kwakuwa gesi inatokea
Mtwara mjini (Mnazibay) umeme utafika ili wananchi washindwe wenyewe
kujiunganishia umeme, ahadi ya serikali ni lazima waitekeleze ahadi hiyo..”
alisema.
Wakazi wa kata ya Naliendele waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Mtwara mjini (CUF), Maftaha Nachuma, uliokuwa na lengo la kuwapongeza wapiga kura wake kwa kumchagua kuwa mbunge. |
Alisema,
kupitia kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma ambaye yeye ni mjumbe, ilishawahi
kuwaita viongozi wa TANESCO na kuwauliza maswali kadhaa ikiwa ni pamoja na
kutaka kujua kwanini maeneo yaliyopo ndani ya manispaa ya Mtwara hayana umeme
wakati mitambo ya kuzalisha huduma hiyo ipo ndani ya manispaa hiyo.
Alisema
viongozi hao walionekana kukosa majibu kwa baadhi ya maswali walioulizwa, huku
akiyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Naliendele, Comoro, Mbawala Chini,
Miseti na Miembeni.
Aidha, juu
ya ofa iliyotolewa na serikali kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kuvuta
umeme majumbani mwao kwa gharama ya sh. 99,000, alisema wapo baadhi ya
watendaji wa TANESCO wanaishawishi serikali kupandisha gharama hiyo na kufikia
katika kiwango cha kitaifa cha sh. 177,000.
Mbunge wa Mtwara mjini (CUF), Maftaha Nachuma, akisoma dua bada ya kwenda kudhuru kaburi la aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa CUF kata ya Naliendele, Dismas Mnyale. |
“Kuna
watendaji wa TANESCO baadhi yao wanakaa na kuiambia serikali iongeze bei na ile
ofa iwe mwisho, nilizungumza kwenye kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma
tulipowaita bodi ya TANESCO kwamba gesi bado ipo Kusini na popote panapotoka
gesi ambayo inalinufaisha Taifa zima, pale panapotoka gesi lazima wanufaike nae
kwa kiasi kikubwa..” alisema.
Kwa mujibu
wa afisa habari wa shirika hilo, Leila Muhaji, alisema ofa hiyo ambayo awali
ilikuwa ifikie mwisho Machi 31 mwaka huu, bado inaendelea na kwamba wananchi wa
mikoa hiyo wataendelea kunufaika nayo.
No comments:
Post a Comment