Mzee Chikomele Jabir, mkaazi wa halmashauri ya mji Nanyamba, akieleza changamoto zinazowakabili wazee katika huduma mbalimbali za kijamii. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
BAADHI ya
wazee katika halmashauri ya mji Nanyamba, wamelalamikia kero za matibabu
wanazozipata zinazotokana na kukosekana kwa kituo cha afya cha serikali na
kuwalazimu kutumia gharama kubwa katika kituo cha Nanyamba kinachomilikiwa na
shirika la kidini la Mkombozi.
Wakizungumza
na Juma News, wazee hao wamesema wanapata changamoto katika kuhudumiwa
wanapokwenda katika Zahanati ya Dinyecha kutokana na kukosa utaratibu nzuri wa
kuwahudumia wazee na kujikuta wanatumia muda mrefu kupata huduma.
Chikomele
Jabiri, ni mzee ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari, alilalamikia
ukosefu wa dawa za ugonjwa huo katika Zahanati ya Dinyecha iliyo katika
Halmasahuri hiyo na kudai kuwa dawa hizo anazipata katika kituo cha afya cha
Nanyamba kwa gharama kubwa.
“Natakiwa
kwenda kupima pale sukari kila wiki, nikifiika kwanza naandika cheti kwa sh.
2,000 alafu nakwenda kupima damu kwa sh. 2,000 alafu nikisharudi huko
naandikiwa dawa ambazo zinaweza kufikia sh. 8,000..sasa hiyo ukichanganya na
4,000 ni sh. 12,000 ndio nipate dawa za kutumia wiki moja zikiisha nakwenda
tena mchezo ndio huo, yani wagonjwa sukari wengi inawanyonya sana..” alisema.
Alisema hali
hiyo inawapa shida sana hasa wazee ambao uwezo wao wa kujitafutia kipato
umekuwa mdogo wengi wao wakiishi kwa kuwa tegemezi ambapo hata katika Zahanati
ya Dinyecha hakuna utaratibu mzuri wa kuwathamini wazee.
Mzee Chikomele Jabir |
“Tukifika
hospitali tunakuwa sawa na vijana hakuna cha kutusitiri kama sisi wazee..na
kama hauna kijana wa kuchangamka unaweza kunyanyasika sana hospitalini..naiambia
serikali iliyochukua majukumu yote ya nchi izidi kutuboreshea maana kama dawa
zikija kwa wingi na utaratibu ule ukawa unafuatwa kisheria, mimi nafikiri
mengine yatapungua..” alisema Hamisi Kamwendo.
Kamwendo pia
alilalamikia shida ya maji ambayo imekuwa ni kero ya kipindi kirefu sasa
kutokana na miradi mbalimbali ambayo pengine waliitegemea kutatua kero hiyo
kukwama ukiwemo mradi wa AMREF ambao uliishia kusambaza matenki na mabomba ambayo
hayajawahi kuwa na maji.
Alisema
chanzo cha maji kinachotumika kusambaza maji katika halmashauri hiyo ni kimoja
na hata hivyo kina changamoto ya kukosekana kwa nishati ya umeme kiasi cha
kuifanya halmashari kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua mafuta ya kuwasha
Jenereta ambalo haliwezi kutoa huduma mfululizo.
Mkurugenzi
wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, alikiri kuwapo kwa changamoto hizo huku
kuhusu afya akidai kuwa zinatokana na ukosefu wa kituo cha afya hali
inayopelekea wananchi wake kulazimika kutumia gharama kubwa katika kupata
matibabu katika Kituo cha afya cha Nanyamba ambacho sio cha serikali.
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Nanyamba, Oscar Ng'itu, akifafanua masuala mbalimbali yakimaendeleo yaliyopo katika halmashauri yake. |
Alisema kwa
sasa wanafikiria namna ya kupunguza changamoto hiyo kwa kuingia ubia na shirika
linalomiliki kituo hicho ili kiwe kituo teule amacho kitatoa huduma zake kwa
gharama zile ambazo zinapatikana katika vituo vya afya vya serikali, huku
wakiendelea na mpango wa kuwa na Zahanati ya halmasahuri.
Kuhusu
changamoto wanazozipata wazee wanapokwenda kupata matibabu, alisema alishatoa
maagizo katika vituo vya afya juu ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya
kuhudumia wazee, hivyo aliahidi kurudi tena kwa ajili ya kwenda kuhakiki na
kujua kwanini maagizo yake hayatekelezwi.
Akizungumzia
kero ya maji, Ng’itu alisema tatizo lililopo ni kwamba nishati inayotumika
katika chanzo cha maji ni Jenereta ambalo halina uwezo wa kufanyakazi kwa muda
mrefu kwasababu ya uhitaji wa mafuta.
Alisema
halmashauri inalazimika kutumia gharama za kununua mafuta kaisi cha lita 200
kila siku kwa ajili ya huduma ya Jenereta ambazo hata hivyo pesa inayopatikana
kwa mwezi kupitia mradi wa maji hazilingani na gharama zinazotumika kununua
mafuta.
“Sasa hilo
lilishaonwa nadhani kwanzia mwaka juzi wizara ya maji kwa kushirikiana na
wizara ya nishati na madini waliweka utaratibu ili umeme uweze kufika kwenye
kile chanzo..wiki moja iliyopita nilikutana na meneja wa Tanesco mkoa,
ameniambia mchakato umefikia hatua za mwisho na stage iliobaki ni kwa
mkandarasi kusaini mkataba ili aweze kwenda saiti..” alisema.
Mhandisi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa
wa Mtwara, Daniel Kyando, aliwaondoa hofu wakazi wa Nanyamba kwa kuwaambia kuwa
sasa mambo yamekaa sawa na ndani ya wiki hii mkandarasi ataanza kazi ya
kupeleka umeme katika chanzo hicho.
No comments:
Post a Comment