Na Juma
Mohamed, Mtwara.
ZAIDI ya
kaya 500 katika manispaa ya Mtwara Mikindani zimeathirikia na mafuriko
yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia usiku wa juzi kuamkia jana, na
kupelekea wananchi wengi wa kaya hizo kupoteza mali zao na vyakula kutokana na
kuingiliwa na maji katika nyumba zao.
Akitoa tathmini
ya mafuriko hayo, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, alisema amejitahidi
kuzungikia maeneo mbalimbali katika kata zote 18 za manispaa hiyo akiambatana
na kamati ya maafa na kubaini kuwa hakuna maafa yeyote kwa binadamu wala nyumba
ambayo imebomolewa na mvua hiyo zaidi ya upotevu wa mali na vyakula.
“Hali
tuliyoikuta ni kwamba kaya zilizoathirika ni nyingi ingawa bado tunataka tupate
taarifa kamili kutoka kwa watendaji wa kata na wanaendelea kutuletea taarifa zao
za mukhtasar wa vikao vya kamati za maafa ambazo wameshakaa huko kwenye kata na
tumeshaanza kuzipokea..lakini mpaka sasa hivi inaonyesha ni zaidi ya nyumba 500
zimeweza kuingiliwa na maji ndani.” Alisema.
Alisema bado
wilaya inafanya jitihada za kuandaa makazi kwa ajili ya wananchi watakaokosa
hifadhi katika kata zao ambapo wametenga eneo katika Chuo cha Walimu Mtwara
(TTC) ambalo linauwezo wa kuhifadhi zaidi ya kaya 30 huku jitihada za kupata
maeneo mengine zikiendelea kufanyika.
“Kwahiyo
tumeagiza kwenye kata zote kama wananchi watakosa kabisa sehemu za kusitiriwa
basi wawalete kwetu tutawasitiri lakini bado tunaendelea kutafuta sehemu
nyingine kama pale pataja basi tuwapeleke sehemu nyingine na tutaweza
kuwagharamia chakula kwa hizi siku chache zitakazokuwa kama changamoto kwao.” Alisema.
Alisema,
kamati ya maafa imetoa agizo kwa mkurugenzi wa halmashauri kwa kushirikiana na
mstahiki Meya na kamati ya fedha kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya
kukarabati miundombinu ambayo imeathiriwa na mvua.
Aidha,
alisema licha ya mfereji mkubwa uliochimbwa kuanzia Kiyangu kwa lengo la
kupeleka maji baharini kuonekana kuzidiwa na maji kiasi cha kuonekana bado
yanafurika katika nyumba zilizopo maeneo hayo, bado umejitahidi kusaidia
kupeleka maji baharini ukilinganisha na ilivyokuwa siku za nyuma.
Hata hivyo,
baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo yaliyo karibu na mfereji huo walionekana kutoridhishwa
na ubora wake na kudai kuwa umezidiwa na maji kiasi cha kuonekana kama bado
hauna msaada kwasababu maji bado yamefurika kwenye nyumba za watu.
No comments:
Post a Comment