Wednesday, February 3, 2016

Mifuko ya hifadhi ya jamii yatakiwa kutunza kumbukumbu za wanachama.


Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii PPF mkoa wa Mtwara waliohudhuria semina ya siku moja ya kutoa elimu kwa wadau hao juu ya mafao mapya ya Wote Scheme na fao la Uzazi. Kulia ni meneja wa PPF kanda ya kusini, Kwame Temu






Wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF mkoa wa Mtwara waliohudhuria katika semina ya siku moja ya kutoa elimu juu ya mafao mapya ya Wote Scheme na fao la Uzazi, iliyofanyika leo katika ukumbi wa Naf Beach mjni Mtwara. 



Na Juma Mohamed, Mtwara.

MIFUKO ya Hifadhi ya Jamii nchini pamoja na waajiri wametakiwa kutunza vizuri kumbukumbu za wanachama wao ili kuhepusha usumbufu pindi mwanachama anapohitaji mafao yake baada ya kustaafu.
Akizungumza jana mkoani hapa katika ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo maafisa kutoka katika kampuni na taasisi mbalimbali mkoani hapa juu ya huduma zitolewazo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, alisema katika suala la utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu pia kuwashirikisha wanachama ili wafahamu taarifa za mafao yao.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.

“Na hili lifanyike kwa kushirikiana kati ya mfuko wa hifadhi pamoja na mwajiri mwenyewe lakini mwanachama naye ni vyema ikawa sio siri na ajulishwe ni vitu gani ambavyo tunaviita ni kumbukumbu ili na yeye mwenyewe pia ashiriki kuhakikisha kumbukumbu zake zimekamilika na muda wa kustaafu ukifika asichelewe kupata mafao yake..” alisema.
Alisema, mifuko hiyo inatakiwa kupunguza manung’uniko kutoka kwa wanachama wanapostaafu anayotokana na ucheleweshwaji wa mafao na kupelekea usumbufu wa kufatilia mara kwa mara.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akipeana mkono na meneja masoko wa PPF, Abuu Kibiki.

Aidha, mkuu wa wilaya aliwataka wananchi na wajasiliamali wadogo kuchangamkia kwa kujiunga na PPF kupitia mpango wao mpya wa Wote Scheme ambao unazihusisha sekta zisizo rasmi pamoja na mfumo wa ziada uliopo kwenye sekta rasmi.
Alisema, mfumo huo unatoa fursa kwa watu au kikundi cha watu chenye mlengo wa kiuchumi kilichopo kwenye sekta isiyo rasmi kuweza kujiunga ikiwa ni pamoja na mama lishe, wakulima, wafugaji, wavuvi, waendesha pikipiki, wajasiliamali wadogo, wasanii na wanamichezo.
“Tukiangalia pale kiwango cha chini kwa mwezi ni sh. 20,000 ambapo katika wilaya yetu tukiangalia kuna vijana wengi wanaoshiriki katika biashara ndogondogo unakuta kuna wajasiliamali wanaongeza thamani ya mazao kama vile korosho, lakini pia tuna vijana wetu wa bodaboda, bajaji, wavuvi na makundi mengine mengi..” aliongeza.
Kwa upande wake, meneja wa mfuko huo kanda ya Kusini, Kwame Temu, alisema lengo kuu la semina hiyo ni kuwaelimisha wanachama na wadau wa mfuko huo juu ya mafao mapya ambayo yamezinduliwa likiwamo fao la uzazi na mpango wa Wote Scheme.

Meneja wa PPF kanda ya kusini, Kwame Temu.

Alisema, licha ya kuwa kutakuwa na program maalumu ya kukuana na wadau wa sekta zisizo rasmi hapo baadae lakini wameona ni bora kupitia semina hiyo kutoa elimu juu ya mafao hayo ambapo aliwataka wanachi wa Mtwara kuchangamkia fursa za kujiunga na mfuko huo.

Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii PPF kanda ya kusini, Kwame Temu, akizungumza na wadau wa mfuko huo wa mkoa wa Mtwara jana katika semina ya siku moja ya kutoa elimu kwa wadau hao juu ya mafao mapya ya Wote Scheme na fao la Uzazi.

Kuhusu suala la kulipa mafao ya wanachama kwa wakati, alisema mfuko huo umejitahidi kuboresha huduma zake hasa za Tehama ambapo sasa mwajiri anaweza kutambua taarifa za mfanyakazi wake akiwa ofisini kwake bila kwenda katika ofisi za PPF kwa kuingia katika linki atakayo patiwa na mfuko huo.
“Kwahiyo niseme tu kwamba tumejaribu kupambana na changamoto hiyo ya kumbukumbu na hii inatuwezesha kulipa mafao yetu kwa wakati kwasababu kama mnavyofahamu siku hizi ukiweza kuwa katika teknolojia kwa kiwango cha juu na ulipaji unakuwa ni wa haraka zaidi..” alisema.


  

No comments: