Wachezaji wa Ndanda na Mtibwa wakichuana katika mechi ya ligi kuu ya vodacom Tanzania Bara iliyochezwa jana Nangwanda Sijaona Mtwara-Timu hizo zilifungana goli 1-1 |
William Lucian wa Ndanda akimtoka mchezaji wa Mtibwa. |
Wachezaji wa akiba wa Ndanda Fc wakishangilia goli baada ya timu hiyo kusawazisha katika dakika za majeruhi. |
Jukwaa la mashabiki wa Ndanda lilivyokuwa baada ya timu yao kusawazisha goli |
Na Juma Mohamed.
Timu ya soka ya Ndanda Fc jana ilijitupa uwanjani Nangwanda Sijaona Mtwara katika mfululizo
wa michezo ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara walipochuana na Mtibwa Sugar ya
Morogoro, mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1.
Mtibwa ndio
walioanza kupata bao katika dakika ya 30 likifungwa na Seleman Rajab baada ya
makosa ya golikipa wa Ndanda Jeremia Kisubi aliyeutema mpira wa kona
iliyochongwa na Issa Rashid, ambapo
mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Mtibwa walikuwa mbele kwa goli hilo moja.
Kipindi cha
pili Ndanda walirejea kwa kasi na kujaribu kupanga mashambulizi ya mara kwa
mara langoni mwa Mtibwa huku wakifanya mabadiliko ya kuwapumzisha baadhi ya
wachezaji wake kama Omega Seme na nafasi yake kuchukuliwa na Said Mohamed na
Omary Mponda aliyempisha Buruhan Rashidi huku Mtibwa wakiwapumzisha Mohamed
Ibrahim ambaye aliumia nafasi yake ikachukuliwa na Ally Sharifu, Ibrahim Juma
alimpisha Henry Joseph na Seleman Rajab aliyempisha Vicent Barnabas.
Atupele Green-akipongezwa na mashabiki wa Ndanda baada ya mchezo |
Mabadiliko
ya Ndanda yalionekana kuzaa matunda, ambapo katika dakika ya 84 mshambuliaji
Atupele Green alitumia vyema makosa ya golikipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed
ambaye aliudaka mpira na kuwachia mbele ya mchezaji huyo kwa lengo la kutaka
kuupiga mbele ndipo Atupele alipopata nafasi ya kuucheza na kumpasia Bryson
Raphael aliyeukwamisha wavuni na kuisawazishia Ndanda goli.
Kabla ya
kufungwa kwa goli hilo, mwamuzi Israel Mujuni Mkongo alimwonesha kadi ya njano
mchezaji Said Mkopi wa Mtibwa baada ya kumchezea madhambi kiungo wa Ndanda,
Kiggi Makasi.
Hata hivyo
bao la Ndanda lilionekana kulalamikiwa zaidi na viongozi wa na wachezaji wa
Mtibwa kwa madai kuwa wachezaji wa Ndanda walimpokonya mpira golikipa ambaye
alikuwa tayari ameshaudaka.
Kocha wa
Mtibwa Sugar Meck Mexime alionekana mwenye jazba baada ya kufungwa kwa goli
hilo na kudai kuwa mwamuzi hakuwatendea haki huku akisema milele soka la
Tanzania haliwezi kuendelea kutokana na aina ya maamuzi yanaamuliwa katika
baadhi ya mechi.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Meck Mexime, akiongea na waandishi baada ya mchezo. |
Mfungaji wa bao hilo, Bryson Raphael, alisema ni bao halali ambapo lilitokana na makosa ya golikipa wa Mtibwa ambaye aliuwachia mpira kwa ajili ya kuanza na kwamba mpira ukishauwachia maana yake tayari umekwishauanzisha na ndio maana Atupele aliuwahi kabla ya kumpatia yeye na kuukwamisha wavuni.
Bryson Raphael akiongea na waandishi baada ya mchezo |
Naye kocha
msaidi wa Ndanda Mussa Mbaya aliyekaimu nafasi ya kocha mkuu anayesubiriwa
kujiunga na timu hiyo kutokea JKU ya Zanzibar, Malale Hamsini, aliwasifu
wachezaji wake kwa kupambana mpaka dakika za wisho huku akijinasibu kucheza
soka safi katika kipindi cha pili na kupelekea kupata bao la kusawazisha.
Kocha msaidizi wa Ndanda, Mussa Mbaya, akiongea na waandishi baada ya mchezo |
Ndanda sasa
inafikisha alama 17 baada ya kushuka dimbani mara 18 ambapo imepanda kwa nafasi
moja kutoka nafasi ya 11 mpaka nafasi ya 10 huku Mtibwa ikisalia katika nafasi
yake ya Nne baada ya kucheza mara 18 na kujikusanyia alama 33.
No comments:
Post a Comment