Aliyekuwa kocha wa Ndanda Fc, Amimu Mawazo. |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
BAADA ya
wiki mbili za kuwa nje ya majukumu ya kukinoa kikosi cha Ndanda Fc ya mkoni
hapa inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, aliyekuwa kocha wa timu
hiyo Amimu Mawazo, ameibuka na kudai kuwa viongozi wa Ndanda walimkosea kwa
kufanya maamuzi ya kumuweka pembeni bila kumshirikisha.
Amimu ambaye
alipewa majukumu ya kukinoa kikosi hicho kuanzia mwanzoni mwa msimu kwa
makubaliano ya kushikilia nafasi hiyo ambaye iliachwa wazi na Jumanne Charles
ambaye alikuwa na leseni C huku waraka
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa wakati huo kuwataka makocha
wa vilabu vya ligi kuu kuwa na Leseni B za ukocha, alisema viongozi hao
hawakupaswa kumficha jambo lolote katika maamuzi yao.
Alisema walipaswa
kukaa naye na kumweleza sababu za kuachana naye lakini haikufanyika hivyo na
baadala yake alisoma taarifa kupitia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na
magazeti yakidai kuwa moja ya sababu ni kuto kubali ushauri kutoka kwa
wasaidizi wake katika benchi la ufundi, jambo ambalo alilipinga.
“Mara
mwandishi wa Ndanda anaandika vyake kuhusiana na mimi mara gazeti lingine
linaandika vitu tofauti kuhusu mimi..sasa mimi nashangaa kwasaabu niliona vitu
vingine vinaandikwa mimi sivijui, kwasababu kuna gazeti nimeshawahi kuona
limeandika kwamba kwasababu ya kutokubali kushuriwa..lakini mimi ni
‘Technician’ ananishauri nani tena..” alisema.
Alisema
kushauriwa katika mpira kupo lakini sio lazima kila ushauri unaopewa ukubaliane
nao, unaweza kupokea ushauri lakini unaangalia kama utaona hauna tija basi
unaachana nao, na kueleza kuwa unapofanya kazi ya uwalimu wa mpira wa miguu
hupaswi kuwa mwoga katika kufanya maamuzi.
Alisema hata
kama sababu ilikuwa ni matokeo mabaya ambayo timu ilikuwa ikiyapata katika
michezo yake 15 ya mzunguko wa kwanza wa ligi ambapo alishinda mchezo mmoja
pekee dhidi ya Coastal Union kwa goli 1-0 na kupata alama 9 katika michezo hiyo
15 ambayo walikwenda sare mara 6 na kupoteza mara 8, alitakiwa kuambiwa
kwasababu kazi ya uwalimu suala la kuachishwa kazi sio kitu cha ajabu.
“Mimi
nilikuta timu wakati imesajiliwa, labda niwapeni ‘background, sasa timu
ikishasajiliwa ule uwezo wa wachezaji unaufahamu vipi, kwahiyo unaanza kufanya
kazi kwanza kwa kuwajua majina alafu sasa ndio uanze kazi ya kuufahamu uwezo wa
kila mchezaji, baada ya hapo sasa unze kuangalia kila mchezaji anamanufaa
katika nafasi gani..kwahiyo matokeo yale mabaya mimi siyakatai kwasababu watu
si ndio wanaona..” alisema.
Aidha,
aliweka wazi kwamba hana chuki kabisa na timu hiyo ambayo amekuwa nayo kwa
kipindi kirefu kuanzia inacheza katika ligi daraja la kwanza ambapo suala la
kuingia na kutoka akiwa kama mwalimu ni kawaida kwake kwani ilishawahi kutokea
hata wakati timu hiyo ilipoamua kuachana na kocha ambaye aliipandisha daraja na
kuifikisha ligi kuu, Denis Kitambi na kuamua kumkabidhi yeye wakati ikitafuta
mwalimu mwingine.
Kwahiyo
nasema mimi bado ni mpenzi wa timu ya Ndanda, na ni mtu ambaye bado timu ya
Ndanda naithamini na sina chuki naye kwasababu timu ya Ndanda haijanikosea hata
hili lililofanyika sio timu inawezekana ni mambo tu ya ngazi mbalimbali..”
aliongeza.
Amimu ambaye
ni mkufunzi wa TFF mwenye Lesi A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
na Leseni B ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB), kabla ya kupewa
jukumu la kukinoa kikosi hicho alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa timu.
Kwa upande
wake, msemaji wa timu hiyo Idrisa Bandari, alisema maamuzi ya kumuondoa Mawazo
kwenye nafasi hiyo yalitokana na kikao cha kamati ya utendaji ambacho kilikaa kabla
ya mchezo wa Ndanda na JKT Ruvu uliochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona,
na Ndanda kupoteza kwa kufungwa magoli 3-1.
Alisema
kamati iliamua kuvunjwa kwa benchi lote la ufundi ambapo maamuzi hayo
yalipelekwa kwenye bodi ya wakurugenzi ambao hata hivyo waliamua wavute subira
lakini wakati timu ikiwa katika mapumziko mafupi wakati ule michuano ya kombe
la mapinduzi ikiendelea visiwani Zanzibar, aliyekuwa msaidizi wa Mawazo,
Ngawina Ngawina aliamua kuachia ngazi kwa madai kushinikizwa na mashabiki wa
timu hiyo ambao walimshutumu kuwa anaigawa timu na hana maelewano mazuri na
mkuu wake.
“Suala la
mzee Amimu kama mtakumbuka sisi tuliingia mkataba na mwalimu Jumanne Charles ambaye
alikuwa na Leseni C ambayo hata hivyo Shirikisho la Mpira (TFF) walipoleta
waraka walitaka mwalimu ambaye anafundisha timu za ligi kuu awe na Leseni B
kwahiyo moja kwa moja waraka ule ukamwondoa Jumanne Charles..” alisema na
kuongeza:
“Tulichokifanya
tukamwomba mzee Amimu aje afanye kazi ile ya kocha mkuu mpaka pale tutakapopata
mwalimu..kwahiyo tangu kipindi kile viongozi walikuwa wanahangaika kutafuta
mwalimu ambaye atakuja kutusaidia kwenye timu..” aliongeza.
Alisema
baada ya mchakato huo wa muda mrefu wa kutafuta mwalimu, timu hiyo ilifanikiwa
kuingia makubaliano na mwalimu wa JKU ya Zanzibar, Malale Hamsini ambaye
alijiunga na timu ikielekea katika mchezo wake na Mgambo Shooting ya Tanga
kabla ya kurejea JKU kuiongoza katika michezo yake ya Kimataifa.
Bandali
alibainisha kwamba kamati ya utendaji ilikubaliana kuwa Mawazo arejeshwe katika
nafasi yake ya ukurugenzi wa ufundi na alishapelekewa barua ya kuitwa katika
majukumu hayo.
No comments:
Post a Comment