Ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imetolewa leo, ambapo jumla ya timu 16 zinakutana katika hatua hiyo (16 bora) itakayoanza kutimua vumbi wikiendi ya Februari 26-1 Machi 2015 katika viwanja mbalimbali nchini.
Michuano hiyo iliyoshirikisha jumla ya timu 64 kutoka ngazi za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, inaingia katika mzunguko wa nne huku kukiwa na timu kutoka katika ngazi zote za ligi za TFF nchini.
Ijumaa tarehe 26 Februari kutachezwa michezo miwili ambapo, Ndanda FC watawakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, huku Coastal Union wakiwa wenyeji wa wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Jumamosi, Februari 27, Mwadui FC watawakaribisha Rhino Rangers katika uwanja wa Mwadui Complex - Shinyanga, Jijini Mbeya Tanzania Prisons watacheza na mshindi kati ya Mbeya City/Wenda FC kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Februari 28, michezo mitatu itachezwa, Simba SC watawakaribisha Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Panone FC watacheza dhidi ya Azam FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi, huku Toto African wakicheza na wachimba madini wa Geita Gold katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Raundi hiyo itamalizika Machi 01, 2015 kwa mchezo mmoja kuchezwa ambapo Young Africans watawakaribisha JKT Mlale katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mwaka huu ataiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya kombe la Shirikisho Barani Africa (CAF CC) mwakani 2017
SOURCE: TFF
No comments:
Post a Comment