Thursday, October 1, 2015

Jeshi la Polisi Mtwara lakanusha kukamatwa kwa masanduku ya kura za Urais, Ubunge.


Henry Mwaibambe-ACP


Na Juma Mohamed.

JESHI la polisi mkoa wa Mtwara limekanusha taarifa zinazodaiwa kuandikwa katika mtandao wa kijamii wa ‘Jamii Forum’ zikidai kukamatwa kwa baadhi ya watu katika kituo cha polisi wilaya ya Masasi mkoani hapa, wakiwa na masanduku na fomu za kupigia kura zipatazo 2000, zikiwa tayari zimetumika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara (RPC), Henry Mwaibambe (ACP), alisema, taarifa ya mtandao huo zilisema kuwa fomu hizo zilimpa alama ya vema mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. John P Magufuli na mgombea ubunge wa jimbo la Masasi kupitia chama hicho Rashid Chuachua.
 Alisema, taarifa hiyo ilidai kuwa, mkuu wa wilaya ya Masasi (Benard Nduta), aliingilia kati na watuhumiwa hao ambao hawakutajwa waliachiwa huru kwa dhamana kwa amri ya mkuu wa wilaya, ambaye ndiye aliewadhamini, na kwamba masanduku hayo na karatasi vimehifadhiwa katika kituo cha polisi wilayani humo.
Aidha, kamanda alisema taarifa hiyo siyo ya kweli na ni za upotoshaji mkubwa na kwamba hakuna mtuhumiwa wala masanduku yaliyokamatwa mkoani hapa katika wilaya hiyo.
“Tunachofahamu kupitia kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, vifaa vya kupigia kura bado havijawasili nchini na alituahidi vitaanza kuwasili mwishoni mwa mwezi huu kutoka nchini Afrika Kusini.” Alisema.
Aliongeza kuwa, jeshi la polisi linamtafuta mhalifu huyo wa mtandaoni na kuahidi kumkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria.

No comments: