Mwanachama wa Chama cha Wazee na Wastaafu Mkoa wa Mtwara (CHAWAMU), Mchina Nnamba, akizungumza jambo juu ya changamoto zinazowakabili wazee, katika kikao na waandishi wa habari jana. |
Na Juma
Mohamed.
CHAMA cha
Wastaafu na Wazee Mkoa wa Mtwara (CHAWAMU) kimelalamikia kitendo cha wanasiasa
wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi zote, kuwasahau wazee
katika sera zao wanazozitoa wakati wa kuomba kura kipindi hiki cha kampeni za
kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza
juzi mkoani hapa, katibu wa chama hicho, Wilbard Nandonde, alisema chama
kinashangazwa na baadhi ya wagombea wa nafasi za Uras, Ubunge na Udiwani
kutoongelea juu ya mustakabali wa changamoto zinazowakabili wazee na baadala
yake wanajikita kutoa ahadi katika nyanja nyingine.
Alisema,
katika kuonyesha msisitizo juu ya changamoto lukuki walizonazo, waliamua
kusambaza makaratasi katika vyama mbalimbali vya siasa na katika ofisi za
serikali, ambazo zinaelezea changamoto hizo ambazo zimeshindwa kutatuliwa kwa
kipindi kirefu.
“Tumegawa
katika ofisi zote za vyama na baadhi ya wagombea tumewapatia..sasa hayo mambo
yako mengi lakini sisi tunaomba tu kwamba wazee wasitusahau katika kunadi sera
zao au katika ‘manifesto’ yao wawe wanatutaja sisi wazee watatufanyia nini..”
alisema.
Alisema yapo
mapendekezo mengi ya wazee ambayo serikali bado haijayafanyia kazi na kuonekana
kukaa kimya, ikiwa ni pamoja na kutopitishwa kwa sera ya wazee ya mwaka 2003
kuwa sheria ambayo kwa kiasi kikubwa ingezeweza kuwalinda.
“Angalia
toka 20013 mpaka leo ni karibu miaka 12 lakini hii sera bado haijatungiwa
sheria..mambo mengine ya manyanyaso labda mtu anakutukana, kama ingekuwa sheria
sisi wenyewe tungechukuwa hatua. Mtu anaekutukana unamkamata na kumfikisha
kwenye vyombo vya sheria, lakini kwasababu ni sera inaonekana haina mguvu
yoyote..” aliongeza.
Alieleza
mapendekezo mengine kuwa ni swala la kupata bure huduma za matibabu ambayo
ilitangazwa serikali lakini utekelezaji wake haufanyiki, ambapo alizitaka
halmashauri zote kuandaa vitambulisho vya wazee kwa ajili ya kutambulika na
kupatiwa matibabu bila kulipia gharama yoyote.
Aidha,
alitoa wito kwa serikali juu ya kukomesha vitendo vya mauwaji ya wazee ambavyo
kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikitokea katika mikoa ya kanda ya ziwa, ambapo
vinatokana na baadhi ya watu kuwa na imani potofu za kishirikina kwa kuamini
kwa kufanya hivyo watafanikiwa mahitaji yao.
Naye,
mwanachama wa chama hicho, Erntrudis Mpokwa, aliitaka manispaa ya Mtwara
Mikindani, kutoa msamaha wa kodi za majengo kwa wazee wastaafu wa manispaa hiyo
ambao uwezo wao wa kipato ni mdogo na hata nguvu ya kutafuta kipato sio kubwa
kiasi cha kumudu gharama ya kulipa sh. 20,000 inayotozwa kwa mwaka.
Mwanachama wa Chama cha Wastaafu na Wazee Mkoa wa Mtwara (CHAWAMU), Erntrudis Mpokwa, akieleza jambo juu ya changamoto zinazowakabili wazee mkoani Mtwara, katika kikao na waandishi wa habari jana. |
“Vyanzo vya
mapato kwa manispaa viko vingi, kwanini wazee ambao hatujiwezi tusisamehewe
kulipa hiyo kodi ya majengo..20,000 kwa mzee ambayo amestaafu na amechoka
kuvua, mzee ambaye alikua seremala na hawezi kuranda tena ni pesa nyingi..kwahiyo
tunamuomba tu mkurugenzi wa manispaa akubali kuwaachia wazee ambao nyumba zao
hazipangishwi na hazifanyiwi biashara wasitozwe kodi kama inavyofanywa
sasaivi..” alisema.
Mwanachama
mwingine, Mchina Nnamba, alisema kodi inayotozwa na manispaa hiyo sio ya nyumba
isipokuwa ni ya mtaa kwasababu viwango vinatozwa kutokana na hadhi ya nyumba
kutoka katika mitaa tofauti.
“Sasa
matokeo yake hawatozi kodi ya thamani ya nyumba, ila watoza kodi ya mtaa ambayo
haipo..mimi jana (juzi) nilipewa hiyo barua nikawaambia haya madai yenu ni ya
mtaa na sio ya nyumba, nyumba yenye thamani hii mimi sina kwanza uiwahi kufika
ukaiona hiyo nyumba?..hilo ni jambo ambalo wazee wamelalamika mara nyingi..”
alisema.
Chama hicho
kimejipanga kuadhimisha siku ya wazee duniani katika wilaya ya Nanyumbu mkoani
hapa itakayofanyika Oktoba 1 mwaka huu, ambapo kitaifa itaadhimishwa mkoani
Kigoma.
No comments:
Post a Comment