Sunday, September 13, 2015

Ndanda Sc vs Mgambo zaingiza Mil. 5 Nangwanda Sijaona

Wachezaji wa timu za Ndanda Sc na Mgambo JKT wakiinua mikono juu kusalimia mashabiki kabla ya kuanza mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, uliopigwa jana katika uwanja Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara. Timu hizo zilifungana goli 1-1.


Wachezaji wa timu za Ndanda Sc na Mgambo JKT wakipeana mikono na waamuzi kabla ya kuanza kwa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona


Na Juma Mohamed.

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) kimesema jumla ya sh. 5,070,000 zimepatikana baada ya makusanyo ya mlangoni (Get Collection) katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Ndanda Sc ya mkoani humo na Mgambo JKT ya Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, katibu wa chama hicho, Charles George, amesema mapato hayo yalitokana na mashabiki 1,240 waliongia uwanjani kwa kulipa viingilio vya sh. 5,000 katika majukwaa yote matatu na 3,000 kwa mzunguko.

Katibu wa Chama cha Mipra wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Charles George, akiongea na waandishi wa habari juu ya mapato yaliyopatikana katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Ndanda Sc na Mgambo JKT katika uwanja wa Nangwanda Sijaona

Alisema mgawanyo wa mapato hayo ulizingatia kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ilikuwa ni sh. 785,160 huku gharama za tiketi ni sh. 700,008.
Alisema asilimia 15 za gharama za uwanja ilikuwa ni sh. 536,526 ambapo maandalizi ya uwanja ikiwa ni pamoja na gharama za ulinzi, huduma ya kwanza (First Aid) na wauzaji wa tiketi, ilikuwa ni sh. 286,147.
Mgawanyo mwingine ulikuwa ni asilimia 5 ya TFF ambayo ni sh. 178,842, asilimia 9 inayokwenda kwenye bodi ya ligi ni sh. 321,915, asilimia 3 ya MTWAREFA ni sh. 107,305, huku mapato kwa timu zote mbili yakiwa ni asilimia 35 kwa timu mwenyeji ambayo ni sh. 1,251,000 na asilimia 25 kwa timu ngeni iliyoambulia sh. 844,210.
Aidha, alisema chama kimeshangazwa na kusikitishwa na taarifa zilizotangazwa na chombo kimoja cha habari mkoani hapa kuwa viingilio vilikuwa ni sh. 5,000 na 3,000 kinyume na ilivyotamkwa awali katika kikao kati ya chama na waandishi wa habari, na kupelekea kupata usumbufu wakati wa uuzwaji wa tiketi.

“Sisi tulivyokutana na vyombo vya habari tulitangaza kwamba kiingilio ni sh. 5,000 na 3,000 lakini hao waliotangaza sh. 2,000 hatujui kiwango hicho walikipata wapi na kwakweli wamechangia kuleta usumbufu milangoni..sasa naomba tu kwamba mnapopewa taarifa kuhusu viingilio, basi mtangaze vile ambavyo vimetangazwa na wasimamizi wa mchezo husika..” alisema.
Timu hizo zilichoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 ambapo Ndanda ndio walioanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji wao mpya Atupele Green, aliefunga goli la mapema dakika ya pili ya mchezo baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Mgambo, kabla ya Fullu Maganga kusawazisha katika dakika ya 72 kutokana na makosa binafsi yaliyofanywa na walinzi wa Ndanda.

No comments: