Wednesday, September 16, 2015

Wananchi Nanyamba walia na kero ya maji

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa jimbo la Nanyamba, wakifurahi wakati wa zoezi la kuomba udhamini kwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Abdalla Chikota.


Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Nanyamba, Oscar Ng'itu, akimkabidhi fomu mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdalla Chikota.



Na Juma Mohamed.

WAKAZI wa halmashauri ya mji wa Nanyamba wamelalamikia tatizo la uhaba wa maji lililodumu kwa miaka mingi kiasi cha kulazimika kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 50  mpaka Ruvuma kufuata huduma hiyo.
Wakizungumza na kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao walisema maji wanayotumia sio salama kwasababu ni ya mabwawa ambapo hata hivyo upatikanaji wake wanalazimika kusafiri kwa zaidi ya kilomita 10, hali inayopelekea kuzorotesha shughuli zingine za kimaendeleo.
“Hapa tatizo la maji lipo kwa miaka mingi tu..kwasababu halina mwaka jana wala mwaka juzi, maana toka nimezaliwa miaka 39 iliyopita mpaka leo tabu hii mimi ninayo, tunachota huko mabwawani na yakituishia huko ndio tunaondoka huko Ruvuma ni kama kilomita 100 sisi tunaenda..kwahiyo hakuna muda wa kufanya kazi tunataabika na hali kama hizi tu..” alisema Hamisi Manzi.

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa jimbo la Nanyamba, wakifurahi wakati wa zoezi la kuomba udhamini kwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Abdalla Chikota.


Naye, Ahmad Salum, mkazi wa kijiji cha Mjimwema, aliwataka wanasiasa wanasimama majukwaani kunadi sera zao kuomba nafasi mbalimbali za uongozi, kushughulikia kero hiyo iwapo watafanikiwa kupata ridhaa ya kuwatumikia wananchi.
Mussa Mohamed, mkazi wa kijiji cha Kiromba juu, alisema halmashauri yao na Mtwara vijijini kwa ujumla inakumbwa na tatizo hilo kwa muda mrefu, na kwamba kuna miradi iliyowekwa na serikali lakini haina uhakika kutokana na kutofanya kazi toka imewekwa, na kuwafanya wananchi hao kutokuwa na imani na serikali kwa kile wanachoahidi juu ya kutatua tatizo hilo.
“Hili tatizo hatuwezi kujua kama litakwisha kweli..maana ni lamuda mrefu sana, serikali inaleta hii miradi lakini si miradi yenye uhakika..na hata serikali leo wataongea chochote juu ya maji kiukweli hatuamini kama yatapatikana..” alisema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Nanyamba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdallah Chikota, ambaye amekosa mpinzani katika jimbo hilo ameahidi kutatua tatizo hilo iwapo ataapishwa kuwa mbhunge, kwa kufufua na kuanzisha miradi mingine ya maji.
Aliitaja miradi ambayo inahitaji marekebisho kuwa ni mradi wa AMREF na mradi wa Makonde, unaohudumia halmashauri tatu za Nanyamba, Newala na Tandahimba huku miradi miwili mipya ikitarajiwa kuanzishwa.
“Kuna mradi wa maji ambao unatoka mto Ruvuma kwenda kiwanda cha Dangote..kwahiyo tutahakikisha kwamba vijiji vinavyopitiwa na huo mradi vinafaidika, lakini vilevile kuna mradi tena ambao unatoa maji kutoka Mitema, wilayani Newala na utakuja maeneo ya kata ya Nyundo, Mnima, Njengwa na Hinju..kwahiyo nafikiri miradi hiyo ikianza kufanya kazi na ile ya zamani ikikarabatiwa basi asilimia ya watu kupata maji itakuwa ni kubwa.” Alisema.
Aidha, mkurugenzi wa halmashauri ya Nanyamba, Oscar Ng’itu, alisema zipo baadhi ya changamoto ambazo zinapelekea uwepo wa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kukosa nishati ya uhakika katika vyanzo vya maji ambapo wanalazimika kutumia mafuta kiasi cha zaidi ya lita 150 kwa siku kwa ajili ya kuwasha jenereta, ambalo haliwezi kufanya kazi kwa saa 24.
Alisema, tatizo hilo limeshafika serikalini ambapo kwa sasa linashughulikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku akisema tayari wameshatangaza tenda ya kupata mzabuni wa kuweka umeme katika chanzo cha maji, na kuweza kufikisha huduma karibu na wananchi.
Katika hatua nyingine ya kutatua tatizo hilo, alisema wameshafikia hatua nzuri ya kuunganisha mradi wa Makonde, ambao umeshafika katika halmashauri ya Tandahimba na wamekutana na viongozi kwa ajili ya kuafikiana mahitaji yao.

“Maeneo ya Nyundo, Njengwa, Mnima ia wale ambao watanufaika na huo mradi na tukishakuwa na miradi mikubwa hii miwili ninaimani ndani ya muda mfupi huko kote maji yatakuwa yamefika kwasababu maeneo mengi tayari mtandao ule ulishafika..” alisema.

No comments: