Mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela, akimkabidhi fomu ya ugombea ubunge jimbo la Mtwara mjini, mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma. |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
HALI bado
tete kwa upande wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) mkoani
hapa kutokana na kuwa na mkanganyiko juu ya chama gani kilichohalalishwa na
umoja huo kusimamisha mgombea wa ubunge katika jimbo la Mtwara mjini.
Hali hiyo
inatokana na kupishana kwa kauli za viongozi na wagombea ubunge wa vyama viwili
kati ya vinne vinavyounda umoja huo, vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi
(CUF) kuonekana kujihalalishia jimbo hilo na kudai kuwa vimepata ridhaa kutoka
kwa viongozi wa UKAWA.
Juzi mgombea
ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma,
alikwenda kuchukuwa fomu ya ugombea katika ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ya
Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela, kusema kuwa amepata ridhaa hiyo kutoka
kwa uongozi wa chama chake lakini kupitia mwamvuli wa UKAWA.
Alisema awali
waliitwa katika ofisi ya mwenyekiti mwenza wa UKAWA Mhe. James Mbatia, jijini
Dar es Salaam, ambapo alikuwa na mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi mkoa wa
Mtwara, Hassan Uledi, ambaye pia aliwahi kutangaza kuwa chama chake ndicho
kimepewa jimbo hilo na UKAWA, taarifa ambazo zilikanushwa na katibu mkuu wa
NCCR, Mosena Nyambabe.
“Baada ya
kufika tuliambiwa tuweke CV (wasifu) mezani, kwamba nani kati yetu ana uwezo
mkubwa wa kupeperusha bendera ya UKAWA Mtwara mjini, kwasababu lengo la UKAWA ni
kuhakikisha kwamba tunapata Rais mmoja..lakini sio tu Rais mmoja, ni
kuhakikisha tunapata wabunge ambao wanaenda kuwa mawaziri lakini na wabunge
ambao watahakikisha watetea masilahi ya wananchi wa sehemu husika..” alisema.
Na kuongeza
“kwahiyo tukalazimika tuoneshe CV zetu, nikaanza mimi kuzungumza baadae akaja
Mhe. Uledi ikaonekana CV za mwenzangu zimepwaya ndipo yakatoka mapendekezo
kwamba jimbo la Mtwara asimame Mhe. Maftaha kupitia CUF..” aliongeza.
Alisema,
ukiachiliambali wasifu, vigezo vingine vilivyoangaliwa ni chama kilicho na
wafuasi wengi na kilichofanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa
ambapo NCCR walipata mitaa mitano huku CUF wakipata mitaa 36.
NEWS ROOM,
ilimtafuta mwenyekiti wa NCCR mkoa wa Mtwara ambaye naye anagombea jimbo hilo,
Hassan Uledi, ambaye alikanusha taarifa hizo na kusema kwamba katika kikao
ambacho walikutana na Mbatia hakukuwa na maamuzi ya chama chochote kupewa jimbo
hilo.
Alisema
barua ambayo amepewa Maftaha na katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ni
barua ambayo kila mgombea anapaswa kupewa na katibu mkuu wa chama chake, hivyo
hata yeye anayo aliyopewa na chama chake na kwamba Agosti 17 mwaka huu
atakwenda kuchukuwa fomu ya kugombea jimbo hilo katika ofisi ya mkurugenzi wa
manispaa ya Mtwara Mikindani.
Naye, katibu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mtwara, Willy Mkapa,
alikana taarifa hizo na kusema kuwa bado wanasubiri waraka wa mgawanyo wa
majimbo kutoka kwa viongozi wa UKAWA ambao ulitegemewa kutolewa kuanzia Agosti
15 mwaka huu.
Alisema
wanaohusika katika vikao vya UKAWA sio wagombea bali ni wenye viti na makatibu
wa vyama, jambo ambalo bado halijafanyika.
“Kwahiyo
jimbo la Mtwara mjini bado halijatolewa kwa chama chochote..lakini pia naona
ingekuwa ni vizuri tusingekuwa na haraka, tusubirie mwongozo ambao utatuelekeza
vizuri ili kumaliza migogoro yote, maana leo hii (juzi) tumeletewa miongozo ya
udiwani , kwahiyo tutaachiana kwa vigezo ambavyo vimeelekezwa na viongozi wetu
wa ngazi za juu..” alisema Mkapa.
No comments:
Post a Comment