Friday, August 21, 2015

Murji: Sitishwi na mgombea yeyote Mtwara mjini.

Mgombea ubunge wa Mtwara mjini na mbunge anayemaliza muda wake, Hasnain Murji akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya ugombea juzi katika ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela.

Mgombea ubunge wa Mtwara mjini na mbunge anayemaliza muda wake, Hasnain Murji, akipokea fomu ya ugombea kutoka kwa mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela.

Mgombea ubunge jimbo la Mtwara mjini, Joel Nanauka, akipokea fomu ya ugombea kutoka kwa mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela juzi.


Joel Nanauka akipokea kitabu cha maelekezo juu ya taratibu za uchaguzi kutoka kwa mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela, ambaye ndio msimamizi wa uchaguzi katika manispaa hiyo.


Joel Nanauka akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela

 Na Juma Mohamed, Mtwara. 

MBUNGE wa Mtwara mjini anayemaliza muda wake, Mhe. Hasnain Murji, amesema hatishwi na mgombea yeyote wa vyama vya upinzani ambao wamechukuwa fomu kwa ajili ya kugombea katika jimbo hilo.
Murji aliyasema hayo juzi bada ya kuchukua fomu ya ugombea katika ofisi ya mkurugenzi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela, na kufanya idadi ya waliochukuwa fomu hadi juzi kuwa ni wanne.
Alisema, jambo linalomfanya kutowahofia wagombea hao ni kutokana na kutoifahamu vizuri Mtwara kama anavyoifahamu yeye ambaye ameishi kwa kipindi kirefu na kupata kufahamu vizuri matatizo waliyonayo wananchi wa jimbo hilo.
“Kwahiyo sioni kama kuna mgombea yeyote maana naona tu kama wamekuja kutafuta ajira ya ubunge na sio kuwasaidia wananchi, kwasababu kipindi chote hawakuwepo Mtwara wamekuja leo kipindi cha kugombea..sasa nashangaa kwanini miaka yote tulikuwa na matatizo mengi lakini hatujawaona..” alisema.
Alisema anaimani wananchi wa Mtwara ndio mashuhuda wa aliyoyafanya kwa kipindi chote cha miaka mitano na wao ndio waamuzi wa nani anafaa kuwawakilisha bungeni na bado anaimani nao.
Kuhusu kutaka kujitoa katika kinyang’anyiro cha kugombea, Murji alisema huo ulikuwa ni uvumi tu ambao haukuwa na ukweli na kwamba kwa sasa anajiandaa kufanya kampeni za kiasasa na zakipekee kupitia chama chake cha CCM, na hakuna hata Diwani yeyote katika jimbo lake aliyekatwa katika kura za maoni kama ambavyo ilivumishwa na baadhi ya watu.
Naye mogombea mwingine wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, ambaye alikuwa wakwanza kuchukuwa fomu jana kabla ya Murji, aliwataka wananchi wa Mtwara kuendelea kuwa watulivu na kusubiri maamuzi yatakayotolewa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) juu ya chama gani kinapaswa kusimamisha mgombea katika jimbo hilo.
Alisema, lengo la UKAWA ni kuiondoa CCM madarakani na kwamba yupo tayari kuona lengo hilo linafanikiwa kwa namna yeyote hivyo yupo tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakaeidhinishwa na umoja huo ili asimame katika jimbo hilo.
“Kwahiyo mimi kama mmoja wa wagombea, napenda kusema kwamba nasubiri maamuzi rasmi yatakapotokea na nitayaheshimu pale watakapotamka kuwa ni jina la nani litakalopewa nafasi ya kupeperusha bendera yetu na nitakuwa tayari kumuunga mkono, na naamini wagombea wenzangu wako na utayari huo unaofanana na mimi..” alisema.
Kuhusu mvutano uliopo kati ya vyama viwili vya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) juu ya kupewa jimbo hilo na UKAWA, alisema ni vyema vyama hivyo vikazingatia matamko rasmi yanayotolewa na umoja huo ambapo mgawanyo wa majimbo unafanywa ngazi ya kitaifa huku wa madiwani ndio ambao unafanyika katika ngazi za wilaya.
“Mimi kama mgombea naheshimu matamko rasmi na kwahaya mengine yanayosemwa, mi niseme tu kwamba tuzingatie matamkoa rasmi yanayotolewa na taasisi za kitaifa, kwasababu kwa mujibu wa kanuni za UKAWA makubaliano ya majimbo ni ngazi ya taifa ila ya madiwani ndio ngazi ya wilaya kwahiyo tusubiri taifa watasema nini..” aliongeza.

Mpaka sasa ni jumla ya wagombea wa vyama vinne ndio ambao wamechukuwa fomu kwa ajili ya kugombea jimbo hilo ambao ni Joel Nanauka (CHADEMA), Hasnain murji (CCM), Hassan Uledi (NCCR) na Maftaha Nachuma (CUF).

No comments: