Friday, August 7, 2015

Mpoto ahamasisha wananchi kujiunga na mpango wa hiyari kujiwekea akiba PSPF.

 

Balozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSPF) Mrisho Mpoto, akizungumza na waandishi wa habari, katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi katika maonyeso ya kilimo (NANENANE) juu ya umuhimu wa wananchi kujiunga na mfuko huo hasa katika mpango wa hiyari.

 
 
Na Juma Mohamed, Lindi.

WANANCHI wametakiwa kujiunga na mpango wa hiyari wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSPF) ambao ni haki ya kila Mtanzania ili waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na mfuko huo.
Hayo yamezungumzwa juzi na balozi wa mfuko huo nchini Tanzania, Mrisho Mpoto, katika maonyesho ya kilimo (NANENANE) yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
Alisema kwa sasa mfuko huo unafanya jitihada za ziada katika kuhamasisha wananchi kujiunga hasa katika mpango huo wa hiyari, ambapo wanajitahidi kutoa elimu mbalimbali kupitia maonyesho hayo ili kuhakikisha wananchi wanahamasika na kuamua kujiunga, jambo ambalo linaonekana linafanikiwa.
“Tukasema ni jambo zuri sana tuje tuhamasishe watu ili tuweze kusaidia kwasababu tuna mafao chungu nzima ambayo tunatoa..kuna watu wanakuwa na ndoto za kusomesha, ndoto za kusoma, kuendeleza familia zao na wengine wana matatizo ya kukosa mitaji, lakini tunawaambia PSPF ni suluhisho lao..” alisema Mpoto.
Alisema, mwanachama akichangia kiasi fulani kwa muda uliopangwa anaruhusiwa kuchukuwa nusu ya kile ulichochangia kwa ajili ya kwenda kufanyia mabo yako mengine na kiasi kingine kinachobakia kinakuwa kwa ajili ya faida yako ya baadae.
“Kwasababu sisi lengo letu ni kuhudumia jamii, tukasema twendeni pale tukahudumie jamii..kwahiyo tutahakikisha tunawahudumia na tutawafuata popote pale walipo ili tuweze kuwahudumia.” Aliongeza.
Naye, Vintani Kiosi Kawogo, ambaye alijiunga kwa mara ya kwanza na mfuko huo, alisema wananchi hasa wenye kipato cha kati wanatakiwa kuona umuhimu wa kujiunga na mpango wa hiyari ambao utawawezesha kujiwekea malengo katika maisha yao.
“Maisha ni malengo, bila malengo huwezi kufikia..kwahiyo mimi najiwekea hapa akiba kwasababu ninamalengo na najua kwamba hapo baadae naweza kukwama, kwahiyo najua mfuko huu utanisaidia..” alisema.
……………………………………………mwisho……………………………

No comments: