Wednesday, August 5, 2015

DIRISHA LA USAJILI BONGO KUFUNGWA KESHO


Dirisha la Usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Ligi Daraja la kwanza (FDL), na Ligi Daraja la Pili (SDL) linatarajiwa kufungwa kesho Alhamis saa sita usiku.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), linavikumbusha vilabu vyote vinavyoshirki msimu mpya wa 2015/2015 kuhakikisha vinakamilisha usajili wa wachezaji wao kabla ya dirisha la usajili kufungwa kesho.

Kipindi cha dirisha la usajili kwa timu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kilifunguliwa Juni 15, 2015 na kitamalizika kesho kwa awamu ya kwanza ya usajili.


TWIGA STARS KUINGIA KAMBINI KESHO ZANZIBAR
Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho kisiwani Zanzibar kujiandaa na Fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofayika mwezi Septemba mwaka huu nchini Congo Brazzavile.

Kikosi hicho cha wachezaji 25 chini ya Kocha Mkuu Rogasian Kaijage, tayari kimeanza mazoezi kujiandaa na michuano hiyo ambapo Tanzania ilikata tiketi ya kushiriki fainali hizo baada ya kuiondoa Zambia kwa jumla ya mabao 6-5.

Twiga Stars inaingia kambini  kwa gharama za TFF, huku jitihada za TFF kuwasiliana na Kamati ya Olimpiki nchini (TOC) zikiendelea kuona ni jinsi gani kamati hiyo inaihudumia timu hiyo ya Taifa kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo ya Michezo Afrika.

TFF inatambua TOC ndio wana jukumu la kuhudumia timu za Taifa kuelekea kwenye michuano hiyo ya Michezo ya Afrika ikiwemo Twiga Stars.

Twiga Stars ambayo imefuzu kwa Fainali za Michezo ya Afrika itakayoanza kutimua vumbi Septemba 04 – 17 imepangwa kundi A na wenyeji Congo Brazaville na Nigeria pamoja na Ivory Coast.

SOURCE: TFF

No comments: