Mbunge wa Tandahimba anayemaliza muda wake, Juma Njwayo. |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
MBUNGE wa
Tandahimba anayemaliza muda wake Mhe. Juma Njwayo, amesema hajaridhishwa na
matokeo ya kura za maoni katika uchaguzi wa kuwapata wagombea ubunge kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika hivi karibuni ambapo ameshindwa kutetea
nafasi yake ya kuwa mgombea katika jimbo hilo.
Akizungumza na NEWS ROOM kwa njia ya simu muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Njwayo
aliyeshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 4,304, alisema awali alizunguka
katika matawi mbalimbali na kujiridhisha kuwa aliongoza lakini katika
majumuisho akajikuta ameshindwa na kuwa katika nafasi ya tatu.
Alisema viongozi
wa CCM wilaya walipofanya majumuisho hawakuwashirikisha wagombea na kwamba
tatizo likaanzia hapo kwasababu kuna kata ambazo anaamini kura ziliongezwa huku
akiitaja kata ya Mihuta ambayo ilikuwa na kura 522 lakini baadaye ilionekana
kuwa na kura zaidi ya 1,000.
“Mtu mmoja
alipewa kura 994 ambaye alipata kura 30, kwanini hiyo..sasa baada ya hayo yote
kwasababu inaonekana kulikuwa na uchakachuaji, bado tukaenda ku ‘count’
(Kuhesabu) kura zile zile zilizochakachuliwa..kwahiyo ndio maana nasema
sijaridhika sana na mimi napinga zoezi hilo.” Alisema Njwayo.
Alisema kwa
namna zoezi hilo lilivyoendeshwa, amekosa imani na viongozi wa CCM wilayani
humo na kwamba atafuata taratibu zote za chama katika kuhakikisha anapata haki
yake ya msingi.
Awali katibu
wa CCM wilaya ya Tandahimba, Mohamed Manyamba, alisema mshindi katika jimbo
hilo ni Shaibu Salim Likumbo aliyepata kura 4,719 akifuatiwa na Abdullah
Suleiman Lutavi ambaye alipata kura 4,521 huku Juma Njwayo akiambulia nafasi ya
tatu kwa kupata kura 4,304.
Alisema,
hata hivyo Njwayo aliktaa kusaini karatasi ya matokeo hayo kutokana na msimamo
wake wa kutokubaliana nayo jambo halitoweza kubadilisha matokeo.
No comments:
Post a Comment