Thursday, August 20, 2015

Gesi asilia Mtwara yafunguliwa rasmi..kuanza matumizi baada ya siku chache.




Mnara wa kuunguzia gesi asilia ukiwa anawaka moto baada ya gesi kuruhusiwa kutoka katika kisima cha (MB 3) kilichopo Mnazibay, mkoani Mtwara, ambapo inapelekwa kiwandani Madimba kwa ajili ya kuchakatwa kabla ya kusafirishwa kwenda Kinyerezi, Dar es Salaam.

Mnara ukiwa unawaka moto bada ya gesi kuruhusiwa.


Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, James Mataragio, akifungua 'Valve' kwa mara ya kwanza kuruhusu gesi kutoka katika kisima cha (MB 3) kilichopo Mnazibay mkoani hapa, kwa ajili ya kupelekwa kiwandani Madimba.

 

Picha ya pamoja, viongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wafanyakazi wa kampuni ya Morel and Prom (M&P) kabla ya kuingia ndani ya uzio wa kisima cha gesi asilia (MB 3) leo, Mnazibay Msimbati.


Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja pembeni ya kisima cha gesi (MB 3) Mnazibay.


Baadhi ya wafanyakazi wa M&P


Mwandishi wa NEWS ROOM Juma Mohamed, wapili kushoto akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa M&P akiwemo Remna Rashidi, wapili kulia.

Na Juma Mohamed, Mtwara.

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa mara ya kwanza limeruhusu gesi asilia kutoka katika kisima kimoja (MB 3) kilichopo Mnazibay, Msimbati mkoani hapa kwenda kiwandani Madimba, kwa ajili ya kuchakatwa kabla ya kusafirishwa kwenda kinyerezi, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kufungua gesi hiyo, mkurugenzi wa shirika hilo, James Mataragio, alisema ni jambo la kihistoria ambalo limefanyika kwasababu kulikuwa na changamoto kadhaa katika kipindi chote cha utafiti wa gesi mpaka kukamilisha ujenzi wa visima.
Aidha, baada ya kuiruhusu kutoka katika kisima ilifikishwa katika mnara maalumu uliopo kando kidogo na kisima hicho kwa ajili ya kuiunguza kwa lengo la kujiridhisha juu ya  uwepo wa gesi na uimara wa mabomba na kwamba baadae mnara ulizimwa ili ifikishwe kiwandani.
Mataragio alisema, kisima hicho ambacho ni kimoja kati ya visima vitano vilivyopo, kina gesi yenye futi za ujazo kati ya milioni 20-30 huku kukitarajiwa kuwa na ongezeko kwasababu bado utafiti unaendelea.
“Kwakweli siku ya leo ninajisikia mwenye furaha sana nafikiri kama alivyosema hapo mtaalamu kwamba kulikuwa na changamoto za hapa na pale..lakini ukizingatia ukubwa wa mradi na muda tulioutumia, huu mradi umetumia muda mfupi sanana kwakeli kazi imefanyika vizuri sana, na changamoto zilikuwepo kutokana na baadhi ya watanzania kutoamini kama tutafikia hapa kwamba gesi kufikishwa kwenye bomba na baada ya muda tutazalisha umeme kwa kutumia gesi..” alisema.
Kwa upande wake, meneja mradi wa kampuni ya Morel and Prom (M & P) ambayo ndiyo inashughulika na utafiti na uchimbaji wa visima vya gesi, alisema jambo hilo sio la kawaida na kilichofanyika ni kuwaonesha watanzania kwamba gesi iko tayari na imeanza kupita katika mitambo.
Alisema hiyo ni hatua kubwa na muhimu zaidi kwasababu kufanikisha kutoa gesi katika kisima ikiwa salama bila kuathiri kitu au mtu yeyote ni jambo la kufurahisha, na hatua itakayofuata baada ya hapo ni kuisafirisha kutoka kiwandani Madimba kwenda Kinyerezi, Dar es Salaam tayari kwa matumizi.















No comments: