Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe, akizungumza na NEWS ROOM leo ofisini kwake, juu ya mchakato wa wagombea Ubunge katika Mkoa wa Mtwara. |
Na Mwaandishi wetu.
Jumla ya
makada 45 wamechukuwa na kurejesha fomu za kugombea ubunge katika majimbo yote
10 mkoani Mtwara, huku waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Hawa Ghasia, akiwa na nafasi kubwa ya kupita bila kupingwa katika
jimbo lake kutokana na kukosa mpinzani.
Akizungumza
na NEWS ROOM jana, katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara, Shaibu
Akwilombe, alisema katika wagombea wote waliojitokeza ni Ghasia pekee ambaye
amekosa mpinzani na hivyo anasubiri vikao vya chama kuweza kumpitisha.
Aidha,
waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika ambaye ni mbunge
aliyemaliza muda wake katika jimbo la Newala mijini, amejikuta akipata upinzani
wa wagombea wawili ambao wamejitokeza katika jimbo hilo ambao ni Kwame Andrew
Daffari na Rajab Hamis Kazibure na kufanya idadi ya wagombea watatu.
Jimbo la
Mtwara mjini ambalo lilikuwa chini ya Asnein Murji ambaye anawania tena,
limepata wagombea wengine wanne ambao ni Hussein Kasugulu, Saidi Swala, Mussa
Chimae na Salum Nahodha.
Akwilombe
aliwasihi wagombea wote wanaowania nafasi ya ubunge kuwa na lugha nzuri katika
majukwaa mbalimbali wanayopita katika kipindi hiki cha kampeni za ndani, ili
kuhepusha mpasuko wa wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama.
“Natoa wito
kwa hawa makada wetu ambao ndio wagombea wenyewe, wanakwenda kwenye kampeni,
hizi ni kampeni za ndani ya chama..ni kampeni za ndani ya familia moja kwahiyo
naamini kwa upeo wao na uwelewa wao watatumia lugha za staha, lugha ambazo
hazita chukiza watu wengine na watatumia lugha ambazo zitatufanya tukishamaliza
mchakato huu chama kibakie kuwa kimoja, chenye mshikamano, kupendana na chenye
ushirikiano..”alionya.
Alisema
mpaka mtu anafanya uamuzi wa kuingia katika mchakato wa kugombea ni wazi kwamba
anajua kanuni na taratibu zote zinazopaswa kufuatwa, hivyo hatarajii kuona
kunatokea mkanganyiko baina ya wanachama wenyewe kwa wenye au wagombea na
kwamba mchakato huo utaisha kwa amani.
“Kama mtu
unajua kanuni na taratibu, basi pale ambapo hujaridhika utajua utaratibu wa
kuufuata ili kuweza kuonesha hali yako ya kutoridhishwa..na tukienda na
utaratibu huo siamini kama itafikia wakati mtu atafikiria kwenda mahala pengine
kwa ajili ya kutafuta ridhaa hiyo, tutafanya uchaguzi wa wazi kabisa na haki
ili kila mwanachama aridhike..” aliongeza.
…………………………………………………mwisho…………………………………………………..
No comments:
Post a Comment