Friday, July 31, 2015

Katibu CCM Newala asimamishwa kwa kukutwa na karatasi za kura za maoni ofisini kwa mgombea

Katibu wa CCM mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe.

Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Mtwara na mtia nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Newala vijijini kupitia CCM, Haroun Maarifa.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa Shaibu Akwilombe amemsimamisha kazi aliekuwa katibu wa chama hicho wilaya ya Newala, Juma Namkoveka, kutokana na kukutwa  akichapisha kura za maoni katika ofisi ya mmoja wa watiania ya kugombea ubunge katika jimbo la Newala vijijini.
 
Akwilombe aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa, katibu huyo alikutwa akichapisha karatasi hizo juzi saa 4 usiku katika ofisi ya Haroun Maarifa ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha Radio Safari cha mjini Mtwara na mgombea ubunge wa jimbo la Newala vijijini kupitia CCM.
 
Alisema kitendo cha karatasi hizo kukutwa katika ofisi ya mgombea ubunge hakiwezi kuaminiwa na wagombea wengine wanaowania naye kupitishwa kuwa wagombea wa jimbo hilo na hakistahili kufanywa na mgomea yoyote ili kuhepusha migongano ya kimasilahi baina yao.
Alisema baada ya kukamata karatasi hizo zilipelekwa katika vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuzihifadhi, na kwamba jana alizichukua na kuzipeleka wilayani Newala ambako ndiko eneo sahihi lililotakiwa kuchapisha na sio mjini Mtwara kama ilivyofanywa na katibu huyo.
“Katika mazingira kama hayo kwa wagombea wengine wanaweza wakapata mashaka..sasa baada ya kuchukua hizi hatua za mwanzo za kuhakikisha kwamba karatasi zinakuwa salama, tumeamua kwamba zikitoka polisi zile karatasi nitakabidhiwa mimi na nitakwenda nazo Newala..” alisema.
Aliongeza kuwa “nikifika Newala nimemteuwa kaimu katibu wa wilaya mwingine, anaitwa Jenifer Chingwile, ni katibu msaidizi na muhasibu wa wilaya ya Tandahimba na nimeagiza nimkute Newala..lakini wakati huo huo aliekuwa katibu wa wilaya ya Newala nimetengua mamlka yake ya kiuchaguzi kuanzia leo na nimekwishampa barua yake..” aliongeza.
Alisema katibu huyo alikosa umakini kwa kile alichokifanya, na kwamba kwa mtu makini hawezi kuchukuwa karatasi za kupigia kura na kuzipeleka nyumbani au ofisini kwa mgombea kwa namna yoyote, kwani kila wilaya inapaswa kutengeneza karatasi hizo kwa gharama zake.
Aidha, alisema waligundua kuwa karatasi za jimbo la Newala vijijini ambako Haroun Maarifa ndiko anakogombea zilikuwa zimepungua kutoka idadi ya karatsi 26,000 zilizokuwa zinahitajika na kuwa karatasi 21,000.
Kwa upande wake, katibu aliyesimamishwa, Juma Namkoveka, alipotakiwa kuzungumzia swala hilo alikataa na kudai kuwa hawezi kuzungumza chochote na kwamba yaliyozungumzwa na katibu wa mkoa yanatosha.
 
NEWS ROOM ilimtafuta Haroun Maarifa ambaye ni katibu mwenezi wa CCM mkoa, na kuzungumza naye kwa njia ya simu kutoka wilayani Newala ambapo alikana kutambua taarifa hizo na kusema kuwa ofisi yake haihusiki na kazi za kuchapisha karatasi.
 

No comments: