Thomas Ulimwengu wa Ngorongoro |
Na Princess
Asia
TIMU ya taifa ya soka ya
vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inashuka dimbani kwenye
Uwanja wa Chamazi, kumenyana na vijana wenzao wa Rwanda katika mchezo wa
kirafiki, kujiandaa na mechi dhidi ya Nigeria Julai 29, kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Afrika.
Rwanda ‘Nyigu Wadogo’,
waliwawasili Dar es Salaam jana mchana Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la
ndege la Rwanda kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ngorongoro
Heroes.
Rwanda yenye msafara wa watu
27 wakiwemo wachezaji 20, imefikia katika hoteli ya Sapphire na baada ya mechi
ya leo, timu hizo zitacheza tena keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Ngorongoro Heroes iko kambini
chini ya Kocha wake, Mdenmark Jakob Michelsen na msaidizi wake Mohamed Adolf
Rishard.
Mechi dhidi ya Nigeria ambayo
ni ya kwanza ya raundi ya pili kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika
zitakazofanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Julai 29 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
KOMBE LA KAGAME, YANGA YAKATA UTEPE LEO
Kikosi cha Yanga 2012 |
Na Prince
Akbar
HATIMAYE pazia la michuano ya
Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame,
linapenuliwa leo, kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Yanga SC dhidi ya
Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10:00
jioni.
Mabingwa hao mara nne wa
michuano hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wiki moja tu tangu wapate kocha
mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet ambaye ni juzi tu alitaja wachezaji 20
atakaowatumia kwenye michuano hiyo.
Saintfiet aliwaacha kwenye
kikosi chake wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na
Frank Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda
mrefu.
Aidha, pia aliwaacha beki
mkongwe na Nahodha Nsajigwa Shadrack na kiungo Nurdin Bakari.
Saintfiet alisema kwamba
Omega, Msuva na Damayo watakuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa
miaka 20, inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa
ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.
Kocha Tom Saintfiet |
“Kwa mujibu wa kanuni
natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na
Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye maandalizi
ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu
hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia
Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini
amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Wachezaji aliowateua baada ya
kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni;
makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David Luhende,
Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar
Joshua, Stefano Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif
‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi
Kiiza na washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Tangu aichukue timu, Saintfiet
alicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu na kushinda mabao 2-0. Katika
mechi hiyo aliwasilisha falsafa mpya ya uchezaji ya timu, ambayo ni soka ya
utulivu zaidi mfano kama wa kupaki basin a kushambulia kwa
kushitukiza.
Mtakatifu Tom alisema falsafa
yake ni ushindi iwe wa 1-0 au 5-0 na timu inayoshinda ni ile ambayo kwanza
inajilinda vizuri.
Hivyo wana Yanga waende
uwanjani na leo, wakitarajiwa kuendelea kuona timu yao ikipaki basi na hawana
budi kuuvmilia mfumo huo, kwa sababu Tom anataka uzoeleke ili autumie kwa
ufanisi baadaye kwenye michuano mikubwa ya Afrika.
Tom
alitolea mfano mafanikio ya Chelsea msimu uliopita kutokana na mfumo huo,
uliowawezesha kuving’oa vigogo wakiwemo waliokuwa mabingwa watetezi Barcelona
kabla ya kuifunga Barcelona kwenye fainali na kubeba ndoo ya Ulaya.
Mchezo kati ya Yanga na
Atlecito, utatanguliwa na mechi baina ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo,
APR ya Rwanda dhidi ya Waw Salaam.
KIKOSI CHA YANGA
KAGAME;
Makipa; Yaw Berko na
Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul,
David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus
Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi
‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar
Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said
Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
No comments:
Post a Comment