Mashali akivalishwa mkanda wake wa ubingwa baada ya kuutetea jana kwa kumtwanga TKO raundi ya tano Maisha |
Na Prince
Akbar
BAADA ya kumtwanga kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Samson Maisha wa Mbeya, bingwa wa Taifa wa TPBO, Thomas Mashali 'Simba wa Teranga' amesema anamtaka mshindi wa pambano kati ya Japhet Kaseba na Francis Cheka apande naye ulingoni, ili adhihirishe yeye ndiye ‘king’ wa ndondi Tanzania.
BAADA ya kumtwanga kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Samson Maisha wa Mbeya, bingwa wa Taifa wa TPBO, Thomas Mashali 'Simba wa Teranga' amesema anamtaka mshindi wa pambano kati ya Japhet Kaseba na Francis Cheka apande naye ulingoni, ili adhihirishe yeye ndiye ‘king’ wa ndondi Tanzania.
Mashali akiwa amemdondosha Maisha jana |
Akizungumza na BIN
ZUBEIRY kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese jana baada ya ushindi
wake huo, Mashali alisema kwamba anaamini kwa sasa katika nchi hii hana mpinzani
na ameomba yeyote atakayeshinda kati ya Kaseba na Cheka asikwepe kupanda naye
ulingoni.
“Huyu mtoto (Maisha), si saizi
yangu, wamempakazia tu, baada ya kuona mabondia wote wa Dar es Salaam sasa hivi
wananiogopa, nilikuwa nampiga huku namhurumia, na bado amefia katikati ya safari
(raundi ya tano). Namtaka mshindi kati ya Kaseba na Cheka,”alisema Mashali.
Katika pambano hilo la jana la
uzito wa Middle, Mashali alimzidi uwezo mpinzani wake kuanzia raundi ya kwanza
na katika raundi ya tano alimkalisha chini kwa ngumi kali ya mkono wa
kulia.
Maisha alijitutumua kuinuka
ili aendelee na pambano, lakini alionekana dhahiri hajiwezi na ndipo Kocha wake,
Bagaza Mambane akarusha taulo ulingoni. Hata hivyo, Maisha anaonekana ni bondia
mzuri akipata mazoezi zaidi na ujanja wa mjini.
NGASSA AJISALIMISHA AZAM FC, BOCCO 'HASOMEKI'
Ngassa mazoezini Azam FC |
Na Prince
Akbar
WACHEZAJI wa Azam FC waliokuwa
na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars akiwemo Mrisho Khalfan Ngassa
anayevumishiwa kuwa katika mpango wa kurejea klabu ya zamani, Yanga leo wameanza
mazoezi rasmi na timu hiyo, kwa maandalizi ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame.
Kutoka Azam, BIN
ZUBEIRY imeelezwa kwamba, wachezaji wanne hawakufanya mazoezi leo
asubuhi, kwa sababu ambazo hazikuweza kufahamika mara moja, hao ni makipa Deo
Munishi ‘Dida’ na Mwadini Ally na viungo Waziri Salum na Jabir Aziz na
mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.
Waziri aliripoti kambini wiki
iliyopita na kutoa taarifa ya kuuguliwa na baba yake akarejea Zanzibar na Stima
alikuwepo tangu mazoezi yanaanza, wakati Bocco alikuwa Taifa Stars.
Wachezaji wengine waliokuwa na
timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kwenye michunao ya Kombe la Dunia ya
nchi zisizo wanachama wa FIFA, Abdi Kassim ‘Babbi’, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’,
Abdulghani Gullam na Hamisi Mcha tayari wameripoti na wameendelea na mazoezi leo
Chamazi.
Kiungo Salum Abubakar ‘Sure
Boy Jr.’ aliyeumia kabla ya Stars kwenda Msumbiji, yeye anaendelea na programu
maalum ya daktari wa timu hiyo na tayari ameripoti.
John Bocco 'Adenayor' |
Tayari Azam, washindi wa pili
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wamekwishamalisha usajili wa wachezaji wao
hata kabla ya kwenda likizo.
Programu ya maandalizi ya
Kombe la Kagame, inayoendelea hivi sasa itamalizika siku moja kabla ya kuanza
mashindano hayo, Juni 28 na yatakapomalizika, wachezaji watapewa mapumziko ya
siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi
Kuu.
Maandalizi kwa ajili ya VPL
yatahusisha pia ziara ya nje ya nchi ya kujiandaa na msimu mpya, ingawa amesema
nchi hiyo itatajwa baadaye.
Wachezaji wapya kikosini Azam
msimu huu ni kiungo Mkenya George ‘Blackberry’ Odhiambo na kipa Deogratius
Munishi kutoka Mtibwa Sugar, wakati Aishi Salum, Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim
Rajab Jeba na Joseph Kimwaga, wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili cha Azam FC
kinaundwa; na makipa, Mwadini Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi Salum na Jackson
Wandwi, mabeki wa Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samir Haji Nuhu,
Luckson Kakolaki, Said Mourad, Joseph Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre Bolou,
Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim Sadalla, Ramadhani
Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam, Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima,
Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche, Mrisho Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha
na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati washambuliaji ni Gaudence Mwaikimba, John
Bocco ‘Adebayor’.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada ya kushika nafasi
ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la Kagame mwaka huu,
wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wakati
Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.
MILOVAN AWASILI USIKU WA MANANE, KIKOSI SIMBA CHAREJEA DAR USIKU WA LEO
Milovan Cirkovick |
Na Princess
Asia
WAKATI Kocha Mkuu wa Simba SC,
Milovan Cirkovick amewasili alfajiri ya leo kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa
mapumziko, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu kinapanda ndege ya ATC saa1:00
usiku wa leo mjini Mwanza, kurejea Dar es Salaam kuungana na mwalimu hiyo kwa
maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame.
Ofisa Habari wa Simba SC,
Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi hii
kwa simu kutoka Mwanza kwamba timu ikifika itaendelea na mzoezi Uwanja wa TCC,
Chang’ombe, Dar es Salaam chini ya Profesa Milovan, aliyetua kwa ndege ya
shirika la ndege la Uturuki saa 8:45 usiku wa jana.
Simba, mabingwa mara sita wa
Kombe la Kagame, 1975, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa
kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la
ubingwa wa Ligi Kuu kwa mashabiki wao wa huko.
Katika ziara yao hiyo, Simba
ilicheza mechi ya mwisho jana Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa
Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga
Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba mabao 2-0.
Katika mchezo wa jana, kiungo
mpya wa Simba SC, Kiggi Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu
ajiunge nayo mwezi huu kutoka kwa mahasimu, Yanga.
Hata hivyo, bao hilo la Kiggi
lilidumu kwa dakika 20 tu, kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai
Wekundu na hadi kipyenga cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
Michuano ya Kombe la Kagame
inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu
tatu, mbali na Simba watakuwepo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na
washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC.
PETER SHILTON: Aliyefungwa bao la ‘Mkono wa Mungu’ na Maradona
Shilton alivyo sasa |
PETER
Shilton ni mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa ya England aliyezaliwa
Septemba 18, mwaka 1949 Mjini Leicester, England.
Anashikilia rekodi ya kucheza
mechi nyingi katika timu ya taifa ya England, zaidi ya wachezaji wengine,
amecheza jumla ya mechi 125.
Katika miaka 30 aliyocheza
soka, ameweza kucheza klabu tofauti 11, pamoja na fainali tatu za Kombe la Dunia
na michuano miwili ya Mataifa ya Ulaya na zaidi ya mechi 1,000 za
michuano.
Shilton hakucheza fainali za
Kombe la Dunia hadi alipofika umri wa miaka 32, lakini amecheza jumla ya mechi
17 na kuweka rekodi ya kutofungwa mechi 10 katika fainali hizo za Kombe la
Dunia, rekodi ambayo pia imewekwa na mlinda mlango wa Ufaransa, Fabien
Barthez.
Alipokuwa Nottingham Forest
alishinda mataji mawili ya UEFA Super Cup, ubingwa Ligi Daraja la Kwanza na
Kombe la Ligi na mataji mengine mengi.
Shilton alikuwa ni mwanafunzi
wa umri wa miaka 13 katika shule ya King Richard III Boys School, iliyopo
Leicester, wakati alipoanza kufanya mazoezi na klabu ya Leicester City mwaka
1963.
Mei
mwaka 1966, akiwa na umri wa miaka 16, Shilton alianza kucheza kwa mara ya
kwanza katika klabu ya Leicester dhidi ya Everton, kuanzia hapo alikuwa
akipangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Pamoja na kuwa na msimu mbaya
wakiwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini walifanikiwa kuingia fainali ya
Kombe iliyochezwa Wembley, akiwa na umri wa mika 19. Shilton alikuwa ni mchezaji
mdogo katika mechi hiyo, lakini walifungwa kwa bao 1-0 na Manchester
City.
Timu yake ilishuka daraja,
lakini aliamua kubaki nayo, pamoja na kucheza timu ya daraja la chini, lakini
alimshawishi kocha wa timu ya taifa ya England wakati huo, Alf Ramsey, kumpa
nafasi ambapo alicheza dhidi ya Ujerumani Mashariki Novemba mwaka 1970. England
ilishinda mabao 3–1.
Baadaye aliisaidia Leicester
kupanda daraja na kupata nafasi nyingine ya kuichezea timu ya taifa katika
mchezo uliomalizika bila ya kufungana dhidi ya Wales katika Uwanja wa
Wembley.
Na
mechi yake ya tatu, huku ikiwa ni ya kwanza ya ushindani alicheza dhidi ya
Uswisi, ambapo walitoka sare 1–1, katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya
Ulaya.
Aliendelea kuichezea England
mechi ya nne na ya tano, wakati huo Shilton akiwa mlinda mlango namba mbili na
Oktoba mwaka 1972, mlinda mlango namba moja Gordon Banks, alipata ajali na
kupoteza uwezo wa kuona na kukatiza soka lake, ambapo nafasi yake ilichukuliwa
na Ray Clemence wa Liverpool.
Shilton aliondoka Leicester na
kujiunga na Stoke City kwa ada ya pauni 325,000, wakati huo wakiendelea kugombea
namba kwenye kikosi cha England na Clemence, ambaye alionekana kumzidi Shilton
kwa kucheza mechi nane kati ya tisa.
Shilton alicheza mara moja tu
mwaka 1975 kwenye kikosi cha England, hakucheza kabisa mwaka 1976 na 1977
alicheza mara mbili.
Msimu wa mwaka 1976 Manchester
United walimtaka Shilton na Stoke walikubali kumtoa kwa pauni 275,000, lakini
walishindwa juu ya mshahara alioutaka kipa huyo na kuamua kuachana
naye.
Shilton enzi zake |
Aliendelea kubaki kwenye
kikosi hicho cha Stoke, ingawa kilishuka daraja mwaka 1977, Nottingham Forest
walitoa ofa ya pauni 250,000 na Shilton alikubali kusaini msimu mpya na timu
hiyo ya Forest kupanda daraja.
Walishinda Kombe la Ligi
katika mchezo wa marudiano baada ya kutoka sare dhidi ya Liverpool, katika
mchezo ambao Shilton alionyesha uwezo wake, akiokoa michomo na vichwa vya Mick
Ferguson. Shilton alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya PFA, kocha mpya wa
England, Ron Greenwood, alimchagua Shilton na kumuacha Clemence na mashabiki na
wachambuzi wengi wa soka kukosoa jambo hilo.
Shilton, alisaidia England kwa
ajili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1980 nchini Italia, ushindi
dhidi ya Hispania, ulimfanya ashinde mechi 30.
Mlinda mlango huyo, aliwahi
kushtakiwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kupigwa faini ya pauni
350, huku tetesi za kutaka kuondoka Nottingham mwaka 1982, zilianza
kuzagaa.
Shilton, aliondoka Forest na
pamoja na kutakiwa na Arsenal, alikwenda kucheza Southampton na kukutana na
wachezaji wenzake wa timu ya taifa kwenye klabu hiyo kama vile, Kevin Keegan,
Alan Ball na Bobby Robson, aliivunja rekodi ya Bank kwa kucheza mechi 188,
wakati mwenzake alicheza 73.
Wakati wa fainali za Kombe la
Dunia mwaka 1986, England walianza taratibu kwa kupoteza mechi ya kwanza ya
makundi dhidi ya Ureno, wakatoka sare na Morocco, wakati huo Robson akiwa
majeruhi na Wilkins alipewa kadi nyekundu.
Kutokana na kukosekana kwao
wote, Shilton alipata nafasi ya kucheza mechi na kuwa nahodha wa England na
kuichapa Poland 3–0 kwenye mechi ya mwisho ya kundi lao, mabao yote yakifungwa
na Gary Lineker.
Walikutana na Paraguay katika
hatua iliyofuata na Shilton kufanya kazi kubwa ya kuokoa mipira ya hatari katika
kipindi cha kwanza, England walishinda 3-0 mabao yakifungwa na Lineker mawili na
moja Peter Beardsley.
Hatua ya robo fainali
walikutana na Argentina, mechi iliyoonyesha uwezo wa Shilton katika kipindi
chake chote cha soka.
Nahodha wa Argentina, Diego
Maradona, alikuwa nyota wa michuano hiyo, lakini katika mchezo wao, England
walimudu kumbana katika kipindi cha kwanza, kazi ilikuwa pale kipindi cha pili,
Maradona alipobadili uchezaji wake na kumchanganya sana Shilton.
Maradona alianza kushambulia
na kuingia kila wakati kwenye eneo la hatari England, beki wa England alifanya
madudu na Maradona, akawahi mpira kwenye eneo la hatari, lakini Shilton aliokoa
mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo wakiwa wamebaki wawili.
Baadaye Maradona alitumia
mbinu nyingine ya kumfunga mlinda mlango huyo baada ya kushindwa kufanya hivyo
hapo mwanzo.
Ulipigwa mpira na Maradona
akaruka na kuangalia ule mpira wakati Shilton akiunyemelea hewani, Maradona
alinyoosha mkono wake na kuugonga mpira na ukaingia nyavuni.
Wachezaji wa England pamoja na
mlinda mlango wao walilalamika kwamba Maradona ameshika, lakini mwamuzi kutoka
Tunisia, Ali Bin Nasser, alikubali bao hilo.
Baadaye Maradona alipoulizwa
alisema ni bao la mkono wa Mungu, na mwamuzi Nasser hakupewa nafasi nyingine
tena ya kuchezesha michuano mikubwa kama hiyo.
Hivyo Shilton, aliepuka
kukosolewa kutokana na vyombo vya habari vya England kuona tukio zima
lilivyokuwa.
Lakini baadaye Maradona
alifunga bao jingine la kawaida, baada ya kuwakusanya mabeki wote wa England
pamoja na Shilton na kupasia nyavu zikiwa tupu. Lineker alifunga bao moja na
kukaribia kusawazisha lakini bahati haikuwa yao, walitolewa katika hatua hiyo ya
robo fainali.
Shilton aliendelea kuichezea
England kwenye michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1988, iliyofanyika Ujerumani
Mashariki.
Juni mwaka 1989, Shilton
alivunja rekodi ya Bobby Moore, aliyecheza mechi 108, wakati yeye akicheza 109,
alicheza mechi tatu bila kufungwa katika kampeni za kushiriki fainali ya Kombe
la Dunia mwaka 1990 na wakafanikiwa kufuzu.
Baada ya kustaafu kuichezea
timu ya Taifa mwaka mwaka 1991, alikataa kuwa kocha kuchukua nafasi ya Stan
Ternent kwa ajili ya kuinoa Hull City.
Yeye na mkewe Sue, walioana
mwaka 1970 na wana watoto wawili, Michael na Sam.
Sam
anacheza soka katika nafasi ya kiungo, amecheza klabu kubwa mbalimbali kama
Plymouth Argyle na Coventry City.
Desemba 18 mwaka 2011,
ilitangazwa kwamba ametengana na mkewe baada ya kuishi wote miaka 40 ya ndoa
yao.
WASIFU WAKE
JINA: Peter Leslie
Shilton
KUZALIWA: Septemba18, 1949
(62)
ALIPOZALIWA: Leicester,
England
UREFU: Futi 6 inchi
1
NAFASI: Mlinda
mlango
TIMU ZA VIJANA
1963–1966 Leicester
City
TIMU ZA WAKUBWA
1966–1974 Leicester City,
(mechi 286, bao 1)
1974–1977 Stoke City, (mechi
110)
1977–1982 Nottingham Forest,
(mechi 202)
1982–1987 Southampton, (mechi
188)
1987–1992 Derby County, (mechi
175)
1992–1995 Plymouth Argyle,
(mechi 34)
1995 Wimbledon,
(hakucheza)
1995 Bolton Wanderers,
(mechi 1)
1995–1996 Coventry City,
(hakucheza)
1996 West Ham United,
(hakucheza)
1996–1997 Leyton Orient,
(mechi 9)
Jumla amecheza mechi 1,005 na
bao 1
(Tangu 1970 hadi 1990,
aliichezea England mechi 125)
UKOCHA: 1992–1995 Plymouth
Argyle
No comments:
Post a Comment