Thursday, March 3, 2016

Serikali yasema hairidhishwi na bei ya Saruji ya Dangote.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara, katika ziara maalumu ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko.


Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo jirani, wakiwa katika uwanja wa Mashujaa kusikiliza hotuba ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI imesema itawaita viongozi wa kiwanda cha saruji cha kampuni ya Dangote Group kilichopo mkoani hapa kuwataka waeleze sababu zilizopelekea saruji inayozalishwa kiwandani hapo kuuzwa bei ghali mkoani Mtwara huku Dar es Salaam ikiwa bei ya chini.
Hayo yameelezwa na waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Mtwara katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa, katika ziara yake ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na Bandarini na kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba.
Alisema serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vingi zaidi ili kutoa mwanya kwa wananchi kuweza kupata ajira na kwa kuanzia jitihada zimeanza kuonekana katika viwanda vya saruji ambavyo uzalishaji umeanza lakini haijaridhishwa na bei ya bidhaa hiyo iliyoanza kuingizwa sokoni hivi karibuni kutoka katika kwanda cha Dangote.
“Tunahangaika na bei, hatujapata bado vizuri bei ya Dangote, naambiwa saruji Mtwara 13,500 lakini saruji hiyo hiyo ukienda Dar es Salaam ni 11,000, hili bado serikali itafuatilia..tutawaita tutawataka watupe maelezo sahihi, maana ya kuwa na kiwanda mahali ni pamoja na kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu, kama Dangote anazalisha saruji halafu saruji hiyo hiyo Mtwara 13,500 Dar es Salaam 11,000 haieleweki..” alisema.

Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo jirani, wakiwa katika uwanja wa Mashujaa kusikiliza hotuba ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.


Alisema serikali bado ina matumaini makubwa na uwepo wa viwanda hivyo kwa kuwanufaisha wananchi waweze kununua saruji kwa bei ya kawaida ili kila mmoja aweze kumudu kujenga nyumba kwa imara kwa kutumia saruji.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha mbolea ambacho mchakato wake unaendelea, alisema serikali itahakikisha inafanya mapitio ya mikataba ikiwa pamoja na kuwahimiza kuharakisha ujenzi huo ili wakulima waanze kutumia mbolea hiyo na wananchi watapata taarifa hizo kupitia viongozi wao.
Aidha, katika kuwaondoa hofu Wanamtwara juu ya ubovu wa miundombinu ya barabara, alisema serikali imedhamiria kufungua milango ya Mtwara kwenda nje ya mkoa huo ambapo barabara ya Uchumi ya Mtwara-Nanyamba-Tandahimba-Newala na Masasi ipo kwenye mpango wa ujenzi kwa kiwango cha lami.
“Taratibu za awali za kutambua wanasema usanifu, tayari zimeshafanywa, na wabunge hili ndio jambo ambalo wamelisimamia kidete kwamba lazima barabara ile inajengwa kwa lami..tena wabunge wote, mpaka yule wa Ndanda (Cecil Mwambe) ambaye ana lami tayari anaunga mkono wenzake kwa kuisemea barabara ya Mtwara-Nanyamba-Tandahimba-Newala na Masasi..” alisema.

No comments: