Mashabiki wa Ndanda Fc wakifunga milango ya geti kuu la kuingia na kutokea uwanja wa Nangwanda Sijaona, kuzuia magari ya polisi yasitoke kupinga mwenzao kuchukuliwa na kupelekwa kituoni |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
JESHI la
polisi mkoani hapa limelazimika kutumia nguvu kiasi cha kufyatua mabomu ya
machozi na risasi za moto kuwatawanya mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa timu ya
Ndanda waliokuwa wanapinga mwenzao kuchuliwa na askari kupelekwa kituoni
kutokana na kudaiwa kufanya vurugu.
Shabiki huyo
aliyefahamka kwa majina ya Ally Likundasi, alionekana kuzimia baada ya Ndanda
kupata goli dakika ya 75 kupitia kwa Kigi Makasy katika mechi ya ligi kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji ya Songea, lakini baada ya muda mfupi
alizinduka na kuanza kupunga mikono kwa askari.
Baada ya
mchezo Likundasi alitaka kwenda kuwapa mikono wachezaji jambo ambalo polisi
walilipinga kwa kwasababu ya kulinda usalama wa wachezaji ambapo wanahakikisha
wachezaji wote wameingia ndani ya mabasi yao na kuondoka uwanjani ndipo
mashabiki wanaweza kuingia uwanjani.
Kitendo cha
polisi kumfunga pingu shabiki huyo na kumpandisha ndani ya gari lao kwa ajili
ya kumfikisha kituoni kilionekana kupingwa vikali na mashabiki wenzake ambao
baada ya kutoka mabasi ya wachezaji wa timu zote mbili waliamua kufunga milango
ya uwanja huo wa Nangwanda Sijaona ili magari ya polisi yasitoke.
Mashabiki hao
walijigawa wengine wakiwa ndani ya uwanja na wengine nje na kuanza kurusha mawe
huku shabiki mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika haraka akijeruhiwa
kichwani baada ya kupigwa na jiwe.
Baada ya
kuona hali inazidi kuwa mbaya huku magari yao yakiwa yamefungiwa ndani ya
uwanja, polisi walianza kufyatua risasi hewani namabomu ya machozi kwa ajili ya
kuwatawanya mashabiki hao, ambapo walifanikiwa na kuweza kuondoka na shabiki
huyo.
Baada ya
muda magari ya polisi yalirudi tena uwanjani kwa ajili ya kuwafuata wenzao
ambao walibaki ambapo katika awamu hiyo dhahama iliwakumba waandishi wa habari
ambao walikuwa wakitekeleza majukumu yao.
Waandishi waliokumbwa
na kashkash hiyo ni Gregory Milanzi wa Mtukwao Community Radio na Adam Malima
wa Chanel Ten ambaye alikamatwa na kupelekwa kituoni kwa madai alikuwa anapiga
picha.
Milanzi
ambaye alikuwa na Kamera kwa ajili ya kuchukua habari, alijikuta akipata kipigo
kutoka kwa mmoja wa askari polisi aliyekuwa akimlazimisha kufuta picha na
kumtaka aondoke katika eneo la tukio, ambapo alivunjiwa miwani yake ya macho.
Hata hivyo
viongozi na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC)
wakiongozwa na mwenyekiti Hassan Simba, makamu mwenyekiti Jimmy Mahundi na
katibu Bryson Mshana, walifika kituoni hapo na kufanikisha kumtoa mwandishi huyo
wa Chanel Ten aliyechukuliwa saa 1 usiku na kuachiwa saa 3 usiku.
Katibu wa
Chama hicho, Bryson Mshana, alisema polisi hawakupaswa kuchukuwa jukumu la
kumkamata mwandishi huyo na baadala yake walipaswa kujiridhisha kwanza juu ya
taaluma yake ya uandishi kwasababu eneo la tukio hilo ndipo zilipo ofisi za
Chama cha wanahabari na ofisi hizo zilikuwa wazi.
“Sisi kama
Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara kwanza tunasikitishwa na kitendo
hicho cha mwandishi kubugudhiwa akiwa kazini na kufuatwa mpaka katika ofisi za
Press kwasababu ofisi zipo eneo lango kuu la kuingilia uwanjani kwa pembeni na
mwenye alijitambulisha kuwa ni mwandishi wa habari..” alisema.
Aidha alisema,
kwa mujibu wa maelezo ya mwandishi ni kwamba askari walihitaji Kamera lakini
kutokana na hali ilivyokuwa ya vurugu pengine ndio sababu wakaamua kuondoka
naye mpaka kituoni.
Kwa upande
wake, mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) Athuman
Kambi, alilitaka jeshi la polisi kuangalia namna bora katika kudhibiti vurugu
kama hizo zinapotokea na kuhepuka kutumia nguvu ambazo zinaweza kuleta madhara
zaidi.
“Wito wangu
kwa mashabiki ni kutii sheria wanapokuwa uwnjani, lakini na wenzetu wa jeshi la
Polisi waangalie namna bora ya kutuliza vurugu za aina ile zinapotokea..”
alisema.
Jitihada za
kumpata kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, hazikuweza
kufanikiwa mpaka habari hii inaingia mitamboni.
Katika mchezo
huo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ndanda Fc waliweza kuchomoza na
ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Majimaji, na kufanikiwa kufikisha alama 20.
No comments:
Post a Comment