Saturday, November 28, 2015

Walimu Mtwara vijijini wakosa makazi bora..

Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msangamkuu, Zaitun Mkamumba, akiwa mbele ya moja ya nyumba za walimu zilizopo katika shule yake. 



Moja ya nyumba ya walimu.


Moja ya nyumba za walimu-shule ya msingi Msangamkuu






Na Juma Mohamed.

WALIMU wa shule ya msingi Mkubiru, halmashauri ya Mtwara vijijini, wamelalamikia ugumu wa maisha wanaoupata kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha ambazo haziendani na kipato wanachokipata kwa mwezi, na kujikuta wanakabiliwa na madeni.
Wakizungumza na Nipashe wiki iliyopita, walisema kuna mambo mengi ambayo yamekuwa ni changamoto katika mazingira yao ya kazi, ikiwa ni pamoja na miundombinu mibovu katika shule yao kiasi cha kuzidi kuyafanya maisha yao kuwa magumu.
Moja ya changamoto ambazo walizieleza ni kukosekana kwa nyumba za walimu shuleni hapo na kusababisha walimu wengi kuishi maeneo ya kijijini ambako wanalazimika kupanga na kulipa kodi kila mwezi huku wakikabiliwa na changamoto nyingine ya usafiri wa kutoka huko wanakoishi mpaka kufika shuleni kiasi cha kulazimika kutumia pesa kwa ajili ya nauli ya pikipiki za kubeba abiria (Bodaboda).

Moja ya nyumba za walimu katika shule ya msingi Mkubiru, halmashauri ya Mtwara vijijini ambayo hata hivyo mwalimu aliyekuwa akiishi amehamishwa kutokana na kuhofia usalama wake kutokana na ubovu wa nyumba.


“Hali ya mshahara na maisha yalivyopanda haviendani, na hii ndio maana inasababisha baadhi ya walimu kujihusisha na biashara labda zingewza kuwakwamua..mshahara nalipwa sh. 350,000 na matumizi yangu kwa mwezi yanafika sh. 520,000, kwahiyo mwisho wa mwezi najikuta nakabiliwa na madeni sana mpaka inafikia wakati tunagombana na wenye nyumba maana kama majengo unavyoyaona hakuna nyumba za waalimu sisi tuliokuwa wengi tunaishi mitaani kwa kupanga..” alisema mwalimu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.
Alisema, kuna mahitaji ambayo analazimika kuyapata kila siku na yanahitaji pesa ikiwa ni pamoja na kununua samaki wanaopatikana kwa sh. 5,000 ambao ndio mboga kubwa kutokana na kijiji hicho kuwa katika mazingira karibu na bahari na mchele ambao wananunua sh. 2,200.
“Mahitaji mengine ambayo nalazimika kutumia pesa kila siku ni vocha kwa ajili ya mawasiliano (Hakutaja anatumia kiasi gani) pamoja na viungo kama nyanya, vitunguu na vingine, kwasababu samaki siwezi kupika bila viungo..” aliongeza.
Alisema, kutokana na kubanwa katika majukumu yao ya kufundisha, wanajikuta wanakosa hata muda wa kufanya shughuli nyingine ambazo labda zingeweza kuwapatia kipato mbadala tofauti na mshahara wao, huku akisema kuwa mpaka sasa anakabiliwa na deni la sh. 126,000.
Alisema, toka ameanza kazi shuleni hapo mpaka sasa ni kama mwaka mmoja na miezi kadhaa imepita na kwamba kitu ambacho anajivunia kuwa nacho ni kumiliki kiwanja ambacho hata hivyo upatikanaji wake kwa kiasi kikubwa umechangiwa na ndugu zake waliompatia pesa kiasi cha sh. Milioni 1.2 huku mwenyewe akitoa sh. 250,000.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkubiru, halmashauri ya Mtwara vijijini, Hazam Nambunga, akielezea changamoto alizonazo shuleni kwake.


Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hazam Nambunga, alikiri kukumbwa na changamoto hizo na kusema kuwa nyumba za walimu zilizopo ni mbili ambazo moja anaishi mwalimu mkuu na nyingine anaishi mwalimu mwingine mmoja.
Aidha, alisema, shule hiyo nakabiliwa pia ukosefu wa ofisi ya waalimu ambapo ambayo ilikuwa ikitumika jingo lake lipo katika hali mbaya na halifai kutumika tena kiasi cha kulazimika kutumia darasa moja kama ofisi ya waalimu na kwamba wanafunzi wa darasa la awali ambao walikuwa wakisomea katika chumba hicho kusomea chini ya miti.

“Tunamwomba Mhe. Rais wa awamu ya tano, pamoja na mambo mengine, aangalie sana na kuboresha masilahi ya walimu zaidi kuboresha miundombinu kwa kutujengea nyumba bora za walimu” alisema.

No comments: