Sunday, November 29, 2015

Chadema Mtwara hali tete, wahitaji msaada toka uongozi wa Kitaifa.


Baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Mtwara, wakitoa malalamiko yao mbele ya waandishi wa habari (Hawapo pichani) juu ya mwenendo wa chama chao ambacho kinakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiungozi kiasi cha kusababisha mgawanyiko baina ya wanachama na viongozi, huku wengine wakitishia kutaka kujivua uanachama na kuchoma bendera za chama


Na Juma Mohamed.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani hapa, kimeutaka uongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa kufika haraka kwa ajili ya kutatua mgogoro uliopo baina ya viongozi wa chama ngazi ya mkoa na wilaya.
Akizungumza na Nipashe, Kaimu katibu wa chama hicho wilya ya Mtwara, Salum Sudi (Saibogi), alisema hali ya chama kwa sasa ni mbaya kutokana na uwepo wa kundi la watu 14 ambalo ndani yake wamo waliokuwa viongozi wa chama hicho kabla ya kupinduliwa kama inavyodaiwa, linalokivuruga chama.
Alisema, watu hao wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa mkoa, Kasim Bingwe na Katibu wa mkoa, Willy Mkapa ambao kwa upande mwingine bado wanatambulika kama viongozi halali, linafanya mbinu chafu za kukivuruga chama na kupangua kila kitu kinachofanywa na viongozi waliopo kwa madai kuwa wao ndio viongozi halali wa chama hicho.

Alisema, uongozi uliopo ambao yeye ndio anakaimu nafasi ya ukatibu uliingia madarakani mwezi Septemba mwaka huu baada ya maamuzi ya mkutano wa dharula wa baraza la mashauriano la mkoa, ambapo liliamua kuuondoa uongozi wa awali uliokuwa chini ya mwenyekiti Kasim Bingwe na katibu Willy Mkapa kwa madai kuwa haukuridhishwa na utendaji wao wa kazi.
“Sasa kilichotokea ni kwamba baada ya kundi hili ambalo liliondolewa na balaza la mashauriano la mkoa, likawaachisha hawa kina Bingwe na huyu Mkapa, walichokifanya wakaja wakaungana na kutengeneza kundi lao la kubishana na uongozi wa kikatiba wa Chadema wilaya na ule wa mkoa, wao wakaenda moja kwa moja na kundi la Chama Cha Wananchi (CUF) bila kujali taratibu za UKAWA..swala hili mimi naongea kwa masikitiko makubwa sana nikiwa kama Chadema damu..” alisema.
Alisema, jambo lingine linalopelekea kuwepo kwa mgogoro ndani ya chama hicho ni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za ‘chakula’ zilizotolewa na makao makuu kwa ajili ya kuwalipa mawakala wa chama waliosimamia na kulinda kura kipindi cha Uchaguzi, na kwamba alidai fedha hizo ambazo alikabidhiwa Diwani wa viti maalumu, Lulu Abdallah, hazikutumika kama ilivyopangwa.
“Baadae tulipata kufahamu matumizi ya fedha zile kwamba zipo ambazo alikabidhiwa diwani wa Kata ya Ufukoni (CUF) zingine alikabidhiwa diwani wa Tandika na hii ya Vigaeni ilikoenda haijulikani..kilichozaliwa tukafanya utafiti tukaamini ni hivyo na tukasema huyu mtu hatufai, baada ya kumuhoji yeye anasema tuulize makao makuu, kuna mtu alikuja sijui kutoka Ngome, tukasema hela si ulipewa wewe si unatajwa na hawa madiwani, tunazihitaji tuwalipe mawakala..tukaanza sasa kupambana na mawakala ambao ni kundi wanadai pesa yao ya Chakula, ikawa ni shida kweli..” alisema.
Alisema, baadae walikaa na mawakala na kuwaeleza ukweli juu ya fedha hizo ambapo waliwaelewa na mpaka sasa bado mawakala hao hawajalipwa.
Aidha, matatizo yote yaliyopo yanasababishwa na hilo kundi la watu 14 ambalo anaamini kuwa linapata nguvu kutoka kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, kutokana na namna alivyo karibu nao na kuwasiliana nao mara kwa mara kwa masuala mbalimbali ya chama.
Jambo lingine linalolalamikiwa kwa hilo kundi ni juu ya mchakato wa kumpata Naibu Meya wa manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo kulitokea mkanganyiko baada ya kupendekezwa watu wawili ndani ya chama kimoja kuwania nafasi hiyo.
Upande mmoja uliwasilisha barua manispaa wakimpendekeza Diwani wa Kata ya Shangani, Mbarale Ahmad huku upande mwingine ukiwasilisha barua inayompendekeza Diwani wa Kata ya Rahaleo, Erick Mkapa.
Hata hivyo, Mkapa ambaye alipendekezwa na uongozi unaoongozwa na mwenyekiti Bingwe, barua yake ilikatiliwa kwa madai kuwa imekosa vigezo ambapo Mbarale aliyependekezwa na uongozi wa kina Saibog alikubaliwa na kupigiwa kura za ndio au hapana ambapo hata hivyo kura za hapana zilikuwa nyingi na kumfanya ashindwe kupata nafasi ya Naibu Meya. Uchaguzi huo utarudiwa.
“Na hawa wtu 14 ndio wanakivuruga chama Mtwara mjini, na kikubwa wanachojivunia wanafahamiana na viongozi wakubwa wa Chadema wa Kitaifa ambao sisi tunadharaulika, jambo ambalo lilibidi litembee kikatiba, na huyu wanayemtumia ni Salum Mwalimu, wao wanasema sisi tunajizuuka kwenye wilaya wao wanacheza juu, na kweli inatusumbua, huyu Salum Mwalim anatusumbua kwelikweli..haya mengine anayoyaleta huku hatuelewi kama chama na anasoma katiba, na inafikia hatua sasa tunajiuliza sisi tumekaa kwa hidhini ya katiba ya Chadema au kwa hidhini ya Salum Mwalimu?..” alihoji.
Kwa upande wake, diwani wa viti maalumu anayelalamikiwa, Lulu Abdallah, alisema Chadema kama chama ambacho ni miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Kaiba ya Wananchi (UKAWA) kinafanya shughuli zake kwa kushirikiana na vyama vingine vya umoja huo.
“Na mimi kama mwanachadema wa mkoa wa Mtwara, kama ni diwani wa viti maalumu wa mkoa wa Mtwara, nasema nilifanya kazi pamoja na CUF, CHADEMA, NCCR na NLD na tukampata Mbunge ambaye ni Maftaha Nachuma na tukawapata Madiwani ambao ni CUF na Chadema, na sasaivi tunaendelea na kazi zetu ndani ya manispaa yetu, kama kuna mgogoro ndani ya Chama, naomba ushughulikiwe ndani ya chama na sio kupeleka kwenye vyombo vya habari au serikali ambao hawahusiki kabisa na migogoro yetu ndani ya chama..” alisema Lulu.
Kwaupande wake, Willy Mkapa ambaye amelalamikiwa na kutajwa katika kundi la watu 14, alisema swala la kupendekezwa kwa Erick Mkapa kugombea Unaibu Meya ilitokana na taarifa zake kupelekwa katika uongozi wa Kitaifa kasha wao ndio walitoa maamuzi ya kuamua Mkapa agombee nafasi hiyo kutokana na wasifu wake na hata hivyo mpaka wanafikia maamuzi ya kupeleka taarifa hizo makao makuu, taarifa za Mbarale zilikuwa bado hazijawafikia.
Kuhusu swala la kukataliwa kwa Mkapa, alielekeza lawama kwa mkurugenzi wa manispaa kwa kudai kuwa hakufuata taratibu, kwasababu alitakiwa kufuata maamuzi ya ngazi za juu na si vinginevyo.
“Sawasawa na Rais awe ameteuwa alafu waziri anakuja kuvunja, kitu kama hicho mimi sijawahi kuona..kwahiyo mimi nasema tu kwamba huu mchakato mpaka kufikia pale umeharibiwa kwanza na serikali, na kama mkurugenzi aliona kama kunatatizo angewaita wagombea wote ofisini kwake akakaa nao na kuwaambia zimekuja barua mbili, hebu rudini kwenye chama mkakubaliane mlete barua moja, lakini ukumbini ndio ameanza kuzisoma zile barua..” alisema.
Aliongeza kuwa, mawakala kuto kulipwa pesa zao taarifa hizo sio sahihi kwasababu kuna baadhi ya maeneo walienda kama UKAWA hasa katika kusimamia kura za Rais, ambapo maeneo mengine Chadema hawakuwa na mawakala kwahiyo walitumia mawakala wa CUF kusimamia, kwahiyo tuliwaachia wao.





No comments: