Na Juma Mohamed.
UONGOZI wa
Zahanati ya kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara Mikindani imeingia makubaliano
ya kupokea fedha kutoka kampuni ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta (BG)
kwa ajili ya kununulia vifaa tiba vya magonjwa ya dharula.
Katika
mkataba uliosainiwa jana mbele ya mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally na mganga
mkuu wa mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa, katika Zahanati hiyo, BG
watakabidhi dola za Kimarekani 280,000 ambazo ni zaidi ya sh. Milioni 600.
Akizungumza
mara baada ya kusaini mkataba huo, Mkuu wa Ayfa, Usalama, Ulinzi na Mazingira
wa BG-Tanzania, Stevenson Murray, alitaja baadhi ya vifaa vitakavyopatikana
kutokana na msaada huo kuwa ni pamoja na Gari la wagonjwa (Ambulance) na vifaa
vya huduma za afya za dharura zitakazozingatia ajali mbalimbali ikiwemo
kung’atwa na nyoka.
Alisema,
kampuni hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana bega kwa bega na mkoa wa Mtwara na
Zahanati hiyo, hivyo ni wajibu kwao kutoa msaada pale panapohitajika kufanya
hivyo pamoja na huduma nyingine.
“Kupitia
program za uwekezaji kwa jamii, tunapanga mipango ya muda mrefu yenye lengo la
kusaidia jamii kukabiliana na changamoto muhimu kwa uendelevu..mipango hii
kabambe ya muda mrefu itasaidia kukabiliana na baadhi ya vyanzo
vinavyosababisha kutokea kwa hali za dharura.” Alisema.
Kwa upande
wake, Mganga mkuu wa kina mama katika Zahanati hiyo, Dkt. Raphaela Handler,
alisema msaada huo utasaidia sana kuinua hali ya afya ya jamii kwa kukarabati
majengo na kutoa vifaa tiba muhimu, kwani vituo vya huduma za afya ni mahali
panaposhughulikia mahitaji ya afya moja kwa moja kwa kuboresha huduma.
“Ninavyoona
idadi ya ajali zinazotokana na magari na pikipiki zinazidi kuongezeka kila siku
na inafaa sana kuwa na huduma za hali ya juu zaidi ili kwa kuwa na vifaa
mbalimbali ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi hasa pale wanapopatwa na hali
mbaya zaidi..aina ya vifaa ambavyo BG watatupatia havipatikani katika Zahanati
au hata hospitali za wilaya, lakini wao watavileta hapa..” alisema.
Naye, mkuu
wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa
Mtwara, Halima Dengego, aliishukuru BG kwa kutoa msaada huo na kusema kuwa
wamekua mstari wa mbele katika kusaidia jamii katika sekta zote muhimu.
“Wamekua
wakitoa msaada katika sekta ya afya, elimu, kilimo na hata uvuvi, kwahiyo sisi
kama mkoa tunashukuru kwa msaada wao na tunawahamasisha wadau wengine wanapokwenda
kufanya kazi na jamii Fulani kuweza kuangalia jamii changamoto zake na kutoa msaada
na kuweza kuleta maendeleo zaidi kwenye jamii husika.” Alisema.
BG Tanzania,
imedhamiria kujenga uhusiano endelevu na jamii inayowazunguka, na kwamba
program za uwekezaji kwa jamii zinatolewa kupitia ushirikiano mkubwa na
mashirika yenye utaalamu na kwa kufanya kazi pamoja na serikali na jamii
kubainisha maeneo ya kipaumbele na mahitaji ya pamoja.
No comments:
Post a Comment