Friday, September 25, 2015

Wananchi manispaa ya Mtwara wataka mbunge atakaeinua kiwango cha elimu.


Baadhi ya wakazi wa kata ya Rahaleo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, waliojitokeza kusikiliza sera katika uzinduzi wa kampeni za udiwani.

Ktibu wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Mtwara, Said Issa 'Kulaga', akinadi sera za chama hicho katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika kata Rahaleo, Mtwara.


Said Issa


Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, akinadi sera za chama hicho na vipaumbele vyake iwapo atafanikiwa kuchaguliwa, katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika kata Rahaleo, Mtwara.


Na Juma Mohamed.

BAADHI ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani wamesema wanataka wapate mbunge ambaye atainua kiwango cha elimu kwa kutatua changamoto mbalimbali zilizoshindwa kutatuliwa na wabunge waliopita, zinazopelekea kuzorotesha sekta hiyo.
Wakitoa maoni yao baada ya kumalizika kwa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani kwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Swahiba Mkauje, katika kata ya Rahaleo, mkoani hapa, walisema wanafunzi wanaosoma shule mbalimbali katika manispaa hiyo hawana matokeo mazuri katika mitihani yao huku kukiwa na miundombinu mibovu ya elimu.
“Jimbo letu la Mtwara mjini kuna matatizo mengi sana kuhusu swala elimu, yani viajana wengi hawana elimu na manispaa yetu bado haiku vizuri katika kuwatetea wananchi..kipimo cha kugunduwa kwamba elimu iko chini ni kuangalia mazingira ya vijana wetu ambao ukiangalia daftari zao utagundua hawako vizuri yani hata kuandika na kusoma hawajui..” alisema, Abdulhman Said ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kisutu C  kwa Chama cha Wananchi (CUF) kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).


Naye, Zainabu Saidi, mkazi wa kata hiyo, alisema baadhi ya changamoto zinazopelekea kuzorota kwa elimu ni kutokana na kukosa vitendea kazi na uhaba wa waalimu katika baadhi ya shule.
Aidha, walisema kutokana na changamoto hizo, wanaimani na mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, ndio mtu sahihi wa kuweza kuzitatua kutokana na kuwa na taaluma ya ualimu ambapo kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho alikuwa mkuu wa shule ya sekondari Mchinga, mkoani Lindi.
Walisema, alipokuwa huko alichangia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha elimu baada ya kuifanya wilaya Lindi vijijini kuongoza kufaulisha katika matokeo ya kidato cha nne mwaka uliopita katika mkoa huo.
“Wilaya yake ya Lindi nadhani vijana walifaulu mwaka uliopita walipata matokeo mazuri na walipata kuwa wilaya ya kwanza kwa kule alikokuwa akifundisha..sasa na Mtwara wanatuambia hatukusoma, kwahiyo na yeye ana taaluma ya elimu na alipokuja hapa nadhani jimbo letu la Mtwara mjini safari hii tumepata mbunge makini na hakuna zaidi yake..” alisema Swalehe Lihewe.
Mgombea udiwani wa kata hiyo, Swahiba Mkauje, alisema moja ya vipaumbele vyake iwapo atafanikiwa kuwa diwani wa kata hiyo, ni kushughulikia changamoto za elimu kwa kudhibiti matatizo ya mimba za utotoni ambayo yametajwa kushamiri katika shule ya sekondari Rahaleo.
“Kwahiyo nitakaa na bodi ya shule kuangalia tunafanyaje ikiwa tu watanipa ridhaa, ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma vizuri..alafu linguine ni wale watoto muda mwingi wanakuwa nje ya shule, sasa tutaangalia ili tujue tatizo nini au kama ni chakula basi tuake na bodi shule ili tuweze kuwapatia mlo angalau wa asubuhi tu kwasababu hilo linawezekana..” alisema.

Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, akinadi sera za chama hicho na vipaumbele vyake iwapo atafanikiwa kuchaguliwa, katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika kata Rahaleo, Mtwara.


Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia chama hicho, Maftaha Nachuma, aliwahakikishiwa wananchi wa kata hiyo kuwa iwapo watamchagua kuwa mbunge yeye na madiwani wake, suala la kwanza ni kuhakikisha haki inatendeka katika miradi yote ya maendeleo inayopitia halmashauri.
“Mama zangu, baba zangu, kaka zangu na ndugu zangu, naomba ifikapo Oktoba 25 tupelekeni sisi ‘majembe’ tunayeweza kusoma mikataba na kuichambua hata ingekuwa na kurasa 100 tuweze kuleta maendeleo Mtwara mjini..” alisema.


No comments: