Friday, July 17, 2015

Chadema waitolea macho kata ya Meya Mtwara.


Mtia nia ya kugombea Udiwani katika kata ya Shangani, Mtwara mjini, Mbarale Ahmad Mbarale alipokuwa akizungumza na wanahabari jana juu ya azma yake ya kuitaka kata hiyo. (PICHA NA JUMA MOHAMED)

  
Na Juma Mohamed, Mtwara.

Mtia nia ya udiwani katika kata ya Shangani, Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) Mbarale Ahmad Mbarale amesema kata hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na tatizo sugu la ukosefu wa ajira kwa vijana, uchafu wa mazingira na hali duni ya kiuchumi kwa akina mam.

 
Akizungumza na NEWS ROOM jana, Mbarale ambaye tayari ameshachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kuwa yapo matatizo mengi ambayo wananchi wa kata hiyo ambayo ilikuwa chini ya Meya wa manispaa ya Mtwara Mikindani Selemani Mtalika (Shilingi) wanakumbana nayo na kwa kutumia elimu yake na uwezo wa kiuongozi alionao, atahakikisha anafanyia kazi na kuyamaliza.

“Simaanishi kwamba hakuna kilichofanyika, yapo ambayo yamefanyika lakini naamini hayajafanyika katika ubora ambao watu watajua kuwa vimefanyika..lakini mimi kwa mtazamo wangu naona bado kuna haja ya kuboresha zaidi..”alisema.
Alisema uamuzi wake wa kuitaka kata hiyo umekuja baada ya kuangalia changamoto zote zilizopo na kujipima uwezo wake na kuona kuwa anatosha kuwaondolea kero zao wananchi wa kata hiyo kupitia uzoefu na elimu yake aliyonayo ya kiutawala na biashara.

Aidha, Mbarale ambaye ana shahada ya kwanza aliyoipata chuo kikuu cha Dar es Salaam alisema amefanya kazi na mashirika na kampuni mbalimbali kwa kipindi kisichopungua miaka nane, ikiwa ni pamoja na shirika la Basic Needs mkoani hapa kwa kipindi cha miaka miwili na kampuni moja ya mtandao wa mawasiliano ambako alifanya kwa mika mitano.
 
“Kwa kutumia uzoefu huo nilionao wa kutumikia mashirika na kampuni mbalimbali kwa kipindi hicho, na kwa kuishi Mtwara kwa muda mrefu huku nikishuhudia mabadiliko mengi ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanywa na kushindwa kutimiza matakwa na mahitaji ya wananchi..mimi binafsi nikapata hiyo nia pamoja na kushauriwa na baadhi ya watu wenye nia njema kwamba nichukue fomu ili niweze kugombea.” Aliongeza.

……………………………..mwisho…………………………………………………..

No comments: