Mwamuzi
Oden Mbaga wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) ndiye anayechezesha mechi ya kirafiki kati ya
Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana).
Mechi
hiyo inachezwa leo Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi.
Mbaga anasaidiwa na waamuzi wasaidizi wa FIFA, John Kanyenye kutoka
Mbeya na Erasmo Jesse wa Morogoro.
TFF
imeteua waamuzi hao baada ya kupata maombi kutoka kwa Shirikisho la
Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ambao ndiyo waandaaji wa mechi hiyo ambayo
ni moja ya vipimo kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Henry Michel kutoka
Ufaransa.
TAFCA YAONGEZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU
Kamati
ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA)
imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama
hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan
Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa
wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
Hivyo,
amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho
itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana
ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
Nafasi
zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu
Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa
Kamati ya Utendaji.
No comments:
Post a Comment