Na Princess
Asia
MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj
Ismail Aden Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora (CCM), jana amefanyiwa upasuaji
wa mgongo jana katika hospitali ya APOLO, India.
Daktari wa Simba SC, Cossmas
Kapinga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, sababu ya Rage kufanyiwa
upasuaji huo ni maradhi yanayojulikana kitaalamu kama Lumbar Disc
Prolapse.
Dk
Kapinga alisema Rage, ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha Radio cha Voice Of
Tabora (VOT) yuko kwa muda wiki moja nchini India akipatiwa matibabu na baada ya
upasuaji huo wa jana, anaweza kupewa ruhusa kuanzia kesho kurejea
nchini.
Kabla ya kuwa Mwenyekiti wa
Simba SC, Rage alikuwa kiungo wa klabu hiyo miaka ya 1970 na miaka ya 1980
aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu, wakati pia amekuwa Katibu wa Shirikisho la Soka
Tanzania (enzi za FAT), Makamu wa Pili wa rais wa TFFna Mjumbe wa Kamati
mbalimbali za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
NDOO NNE ZA KAGAME ZILIVYOTUA YANGA, JE WATABEBA YA TANO 2012?
Na Prince
Akbar
MICHUANO ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, inatarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu yaani Jumamosi
ijayo, kwa mabingwa watetezi, Yanga kufungua dimba na Athletico ya Burundi,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager,
wanaingia kwenye michuano hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kutetea taji lao,
baada ya kusajili wachezaji wapya nyota na kuajiri kocha mpya kutoka Ubelgiji,
Thom Saintfiet.
Miongoni mwa wachezaji nyota
waliosajiliwa Yanga ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Kelvin Yondan kutoka
Simba SC, Simon Msuva kutoka Moro United, Said Bahanuzi kutoka Mtibwa Sugar,
Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Ladisalus Mbogo kutoka Toto African na Nizar
Khalfan aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa
Marekani.
Hao wanaungana na nyota
wengine wa Yanga waliowezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mwaka jana kama
kipa Yaw Berko kutoka Ghana, Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’, Nadir Haroub Ally
‘Cannavaro’, Nahodha Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Godfrey Taita, Rashid
Gumbo, Jerry Tegete na Shamte Ally.
Lakini kikosini kuna Yanga
kuna nyota wengine wa msimu uliopita, lakini hawakucheza Kombe la Kagame kama
viungo Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Athumani Iddi ‘Chuji’.
SIRI YA JEURI YA
YANGA
Yanga inajivunia udhamini wa
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager,
ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa kampuni ya
Shivacom.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium
Lager ilianza kuidhamini Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa
kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es
Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager,
ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC, imekuwa
ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za
uendeshwaji wa klabu.
Na inaaminika udhamini huo
ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya kmaribuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano (2008, 2009 na
2011) sambamba na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka
jana.
ZANZIBAR MWAKA
1975:
Iliingia kama bingwa wa
Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa
Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa
michuano.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja
na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga
Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza
Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu
Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga
iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali
Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba
SC.
Mabao ya Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na
taji la kwanza la michuano hiyo.
KAMPALA, UGANDA MWAKA
1993:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara
na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa
Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga
ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao
2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo
kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga
ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako
ilikutana tena na SC Villa.
Kwa kuzingatia matokeo ya
mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta
mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba na
Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la pili la
michuano hiyo.
Marehemu Kizota aliibuka
mfungaji bora wa michuano hiyo.
KAMPALA, UGANDA MWAKA
1999:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara,
ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda
wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka
1993.
Timu zilizoshiriki michuano
hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya,
Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
Naadiga Dekedaha ya Somalia,
KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji Express na SC Villa za
Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
Kwa matokeo hayo, Kundi D
ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na
mabingwa watetezi.
Mechi ya kwanza, Yanga
ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga
walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao ya
Sekilojo Chambua dakika ya 23
na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
Katika Robo Fanali, Yanga
ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory
Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa
penalti.
Katika Nusu Fainali, Yanga
ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji
Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya
90.
Hivyo kwa mara ya pili, Yanga
ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari
hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa
zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan
Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya mchezo
huo.
Mchezo ukahamia kwenye mikwaju
ya penalti na Manyika Peter akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua
penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1,
Uwanja wa Nakivubo.
DAR ES SALAAM
2011:
Yanga ilifanikiwa kutwaa taji
la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, baada ya
kuifunga Simba bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Shukrani kwake mshambuliaji wa
kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah aliyefunga bao hilo, pekee dakika ya 108,
akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kitaalamu na kiungo Rashid
Gumbo.
Kabla ya taji hilo walilotwaa
Jumapili sambamba na dola za Kimarekani 30, 000, sawa na Sh. Milioni 45 za
Tanzania, Yanga walitwaa tena Kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kwenye
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakiifunga Simba mabao 2-0 na baadaye mara mbili
mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 na 1999, mara zote wakiifunga SC Villa ya
huko.
Ulikuwa mchezo mgumu ambao
ulidumu kwa dakika 120, timu zikionyesha kucheza tahadhari, kabla ya Asamoah
kumaliza kazi.
Kikosi kilichoipa Yanga kombe
la nne la Kagame kilikuwa; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha
Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid Gumbo, Godfrey
Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari, Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah na
Hamisi Kiiza.
Yanga iliyokuwa Kundi B la
michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi
saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare
moja.
Katika Robo Fainali, Yanga
ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya
bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
Katika Nusu Fainali, Yanga
ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia
sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza Simba SC katika
fainali.
Ikumbukwe katika michuano ya
mwaka huu, Yanga iliingia kama ‘viti maalumu’, kwani Simba SC ndio walikuwa
wawakilishi halisi kama mabingwa wa Bara.
Ili kushiriki mashindano ya
mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe CECAFA dola za Kimarekani 20,000 kama faini ya
kugomea mechi ya mshindi wa tatu wa michuano hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es
Salaam.
Yanga ilitakiwa kucheza na
Simba mwaka huo kuwania nafasi ya tatu, ikiwa chini ya Mwenyekiti aliyekuwa na
misimamo mikali, Wakili Imani Omar Madega, Yanga iligoma kwa sababu
hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa mapato ya
milangoni.
Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa
mataji yake manne ya Kombe la Kagame- na Jumamosi wanaanza changamoto ya
kuifukuza rekodi ya watani wao wa jadi, Simba SC waliotwaa taji hilo mara sita,
je wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na
kuona.
NDOO SITA ZA KAGAME ZILIVYOTUA MSIMBAZI, WATABEBA YA SABA 2012?
Na Mahmoud
Zubeiry
WAKATI michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza
Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabingwa wa kihistoria wa michuano
hiyo, Simba SC wamepania kutwaa taji la saba.
Simba wanataka taji la saba na
kwa sababu hiyo wako kwenye maandalizi ya uhakika ili michuano hiyo ikianza wawe
imara waweze kutimiza ndoto zao, ambazo mwaka jana zilishindikana.
Mwaka jana, michuano hiyo
ikifanyika Dar es Salaam, Simba ilimkosakosa kidogo tu mwali wa Kagame, baada ya
kufungwa 1-0 katika fainali na watani wao wa jadi, Yanga katika fainali, ambayo
huwezi kukosea kusema walitawala mchezo, lakini kama ilivyo ada ya soka, bahati
haikuwa yao.
Simba SC imeweka kambi
Zanzibar ambako pia wanashiriki michuano ya kukipima kikosi chake, Kombe la
Urafiki.
Chini ya kocha wake Mserbia,
Profesa Milovan Cirkovick, Simba SC imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota
wapya kadhaa, wakiwemo nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Patrick Kanu Mbivayanga anayecheza nafasi ya kiungo na beki wa kati Lino
Masombo.
Simba pia imemsajili kiungo
bora Afrika Mashariki na Kati, Mussa Mudde ambaye pia anaweza kucheza kama beki
wa kati, wakati imesajili wazawa kama Juma Jebba kutoka Azam FC, Abdallah Juma
kutoka Ruvu Shooting, Kiggi Makassy kutoka Yanga, Salim Kinje aliyekuwa anacheza
Kenya sambamba na kuwarudisha kikosini wachezaji wake iliyowatoa kwa mkopo msimu
uliopita Haruna Shamte na Amri Kiemba.
Kuchanganya na nyota wake wa
msimu uliopita kama kipa bora Afrika Mashariki na Kati, Juma Kaseja,
mwanamichezo Bora Tanzania, Shomary Kapombe, viungo wenye vipaji vya hali ya juu
Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman na washambuliaji tishio Felix
Mumba Sunzu kutoka Zambia na Emmanuel Okwi kutoka Uganda, Wekundu wa Msimbazi
wana uwezo wa kutimiza ndoto zao.
SIRI YA JEURI YA SIMBA
SC:
Simba SC inajivunia udhamini
wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager,
ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa Mohamed Enterprises
Limited.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium
Lager ilianza kuidhamini Simba Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa
kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager,
ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Simba, Yanga SC, imekuwa
ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za
uendeshwaji wa klabu.
Na
inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya karibuni ya klabu
hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili katika kipindi cha miaka
mitano (2010 na 2012) sambamba na kufika Fainali ya Klabu Bingwa wa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.
Hadi sasa kwenye kabati la
mataji la Simba SC, pale makao makuu ya klabu yao, kuna mataji sita ya Kombe la
Kagame, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko klabu nyingine yoyote kwenye historia
ya michuano hiyo, je ilitwaa vipi mataji hayo?
MWAKA
1974:
Hizi zilikuwa fainali za
kwanza rasmi za michuano hiyo na zilichezwa kwa mtindo wa ligi mjini Dar es
Salaam.
Simba iliipiku timu tishio
enzi hizo Afrika Mashariki na Kati, Abaluhya FC ya Kenya, sasa AFC Leopards kwa
kumaliza na pointi tano dhidi ya tatu za vigogo hao wa soka ya
Kenya.
Ilikusanyaje pointi hizo?
Ilianza kwa kuifunga 1-0 Abaluhya kabla ya kuifunga 1-0 Navy FC ya Zanzibar,
kabla ya kuifunga 1-0 Abaluhya na kumaliza kwa sare ya bila kufungana na Simba
FC ya Uganda.
Kikosi cha Simba wakati huo,
kilikuwa kinaundwa na wakali kama Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Shaaban
Baraza, Mohamed Kajole ‘Machela’ (sasa marehemu), Aloo Mwitu/Mohamed Bakari
‘Tall’, Omar Choggo (sasa marehemu), Athumani Juma Kalomba (sasa marehemu),
Khalid Abeid, Martine Kikwa, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu
(sasa marehemu), Abdallah Kibadeni, Saad Ally na Abbas Dilunga.
Ni
wakali hawa hawa ambao pia waliifikisha Simba SC Nusu Fainali ya Klabu Bingwa
Afrika, mwaka 1974 na kutolewa na Mehallal El Kubra ya Misri, wakitoka kuitoa
timu ngumu na tishio barani enzi hizo, Hearts Of Oak ya Ghana.
MWAKA 1991
Simba ilishindwa kutetea taji
hilo mwaka 1975 baada ya kufungwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga katika fainali
visiwani Zanzibar na wakalazimika kusubiri hadi mwaka 1991 ili kupata taji la
pili la michuano hiyo katika fainali nyingine zilizofanyika Dar es Salaam.
Walibebaje taji? Simba
ilianzia Kundi A mjini Dar es Salaam ambako waliongoza na kufanikiwa kuingia
Nusu Fainali, ambako walikutana na Gor Mahia ya Kenya na kushinda 1-0, hivyo
kutinga fainali.
Katika fainali, Wekundu wa
Msimbazi walikutana na SC Villa ya Uganda, iliyokuwa tishio ikiongozwa na
mshambuliaji bora zaidi kuwahi kutokea Uganda, Majjid Musisi Mukiibi na kushinda
mabao 3-0, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ na Kocha Mchezaji Hassan Afif
waking’ara mno na kuwa chachu ya ushindi.
Siku hiyo, Jamhuri Mussa
Kihwelo ‘Julio’ alikuwa ana kazi moja tu- kumdhibiti Musisi (sasa marehemu),
asilete madhara na akafanikiwa. Ilikuwa hadi Musisi anakunywa maji, Julio
anamsubiri arudi uwanjani aanze kutembea naye tena.
Kikosi cha Simba kilichotwaa
taji hilo, kilikuwa kinaundwa na wakali kama Iddi Pazi ‘Father’, Mavumbi Omar,
Raphael Paul (sasa marehemu), Twaha Hamidu ‘Noriega’, Jamhuri Kihwelo, Method
Mogella (sasa marehemu), Iddi Suleiman ‘Meya, Issa Kihange, Bakari Iddi, Ayoub
Mzee/Hassan Afif, Zamoyoni Mogella, Itutu Kiggi ‘Road Master’/Khalfan Ngassa,
Hamisi Thobias Gaga ‘Gaga Rhino’, Frank Kasanga ‘Bwalya’ na Gebo Peter.
MWAKA
1992:
Simba ilifanikiwa kutetea taji
hilo katika fainali zilizofuata visiwani Zanzibar, ikiwa imeboresha zaidi kikosi
chake kwa kuingiza nyota wapya kama kipa Mwameja Mohamed, beki George Masatu na
kiungo Hussein Aman Marsha.
Simba iliyokuwa katika Kundi
B, katika mechi ya kwanza iliifunga 1-0 Bata Bullets FC ya Malawi, mechi ya pili
iliifunga 2-0 Jamhuri SC ya Pemba kabla ya kumalizia kwa sare ya bila kufungana
na El Hilal ya Sudan, hivyo kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba
ilikutana na Small Simba SC ya Zanzibar na kushinda 1-0, hivyo kutinga Fainali,
ambako ilikwenda kukutana na watani wao wa jadi, Yanga SC na kushinda kwa
penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa
Amaan.
MWAKA
1995:
Simba ilishindwa kutetea taji
mjini Kampala, Uganda ingawa bahati nzuri Kombe lilipakizwa kwenye ndege
kurudishwa Dar es Salaam na watani wao, Yanga. Kutoka hapo, Wekundu wa Msimbazi
walilazimika kusubiri hadi mwaka 1995 kutwaa taji lingine la michuano
hiyo.
Ilikuwa ni katika michuano
mingine iliyofanyika Dar es Salaam na Simba tena walipangwa Kundi A na katika
mechi ya kwanza walitoka sare ya 1-1 na Express FC ‘Red Eagles ’ ya Uganda,
mechi ya pili waliichapa 3-1 Morris Supplies ya Somalia kabla ya kuitandika 4-1
Adulis ya Ethiopia na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba
ikiwa inaundwa na idadi kubwa ya nyota wake walioifikisha timu Fainali za Kombe
la CAF mwaka 1993, iliifunga 1-0 El Mourada ya Sudan na kuingia
Fainali.
Katika Fainali, Simba
ilikutana na Express ‘Red Eagles’ na kushinda kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya
1-1 ndani ya dakika 120, siku hiyo George Magere Masatu akijifunga na
kuwasawazishia bao Tai Wekundu dakika ya 53, yaani dakika mbili tu tangu Hussein
Amaan Marsha aifungie Sijmba bao la kuongoza dakika ya 51.
MWAKA
1996:
Simba ilifanikiwa kwa mara ya
pili na ya mwisho kihistoria kutetea taji hilo, mwaka 1996 katika fainali
zilizofanyika Tanzania tena, kwenye miji ya Mwanza na Dar es
Salaam.
Simba ilipangwa tena katika
Kundi A mjini Dar es Salaam na katika mechi ya kwanza, iliifunga 2-0 Small Simba
ya Zanzibar, kabla ya kulala 1-0 mbele ya APR FC ya Rwanda na kumaliza kwa
ushindi wa 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Kwa
matokeo hayo, Simba ilishika nafasi ya pili katika kundi hilo kwa pointi zake
sita, ikizidiwa pointi moja tu APR iliyoongoza kundi hilo, hivyo kutinga Nusu
Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba
ilishinda 1-0 dhidi ya Gor Mahia, bao pekee la Bitta John hivyo kutinga
fainali, ambako ilikutana na APR na kulipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, bao pekee
la George Magere Masatu dakika ya 115.
MWAKA
2002:
Mwaka 1997 michuano hiyo
haikufanyika na mwaka 1998, Simba ilishindwa kutetea taji, baada ya kuchukuliwa
na Rayon Sport ya Rwanda visiwani Zanzibar. Mwaka 1999, taji lilichukuliwa na
Yanga mjini Kampala, Uganda na 2000 na 2001 Simba hawakupata tiketi ya kucheza
michuano hiyo, hadi 2002 katika fainali zilizofanyika visiwani Zanzibar.
Naam, Simba waliandika
historia ya kuwa timu inayoongoza kutwaa taji hilo, ilikuwaje?
Simba ilipangwa Kundi B na
katika mchezo wa kwanza, ililazimishwa sare ya bila kufungana na vibonde Elman
ya Somalia, kabla ya kuzinduka kwenye mechi ya pili na kuifunga Prince Louis ya
Burundi, mabao 2-1, wafungaji wake Emmanuel Gabriel dakika ya 27 na Yussuf Macho
dakika ya 78, na baadaye kuirarua Forodha ya Zanzibar mabao 3-1, wafungaji
Joseph Kaniki ‘Golota’ dakika ya 22, Steven Mapunda ‘Garrincha’ dakika ya 65 na
Macho ‘Musso’ dakika ya 90 na mechi ya mwisho, bao la kujifunga la Kevin Malumbe
dakika ya 88 liliwapa Wekundu wa Msimbazi ushindi wa 1-0 dhidi ya Tusker ya
Kenya.
Kwa
matokeo hayo, Simba iliongoza Kundi hilo kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na
Prince Louis iliyovuna pointi saba, Tusker pointi tano sawa na Elman, wakati
Forodha ilitoka patupu kabisa.
Katika Nusu Fainali, Simba
ilikutana na mabingwa wa Zanzibar enzi hizo, Mlandege na kushinda 2-0, mabao ya
Yussuf Macho ‘Musso’ dakika ya 37, na Shekhan Rashid Abdallah kwa penalti dakika
ya 90.
Katika fainali, Simba
ilikutana tena na Prince Louis na bao pekee la Nteze John Lungu dakika ya sita,
lilitosha kuwafanya Simba waitwe mabingwa wa Kombe la Kagame mara nyingi zaidi
hadi sasa.
Kikosi cha Simba siku hiyo
kilikuwa; Mohamed Mwameja, Said Sued, Ramadhan Wasso/Majuto Komu dk 35, Amri
Said, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Stephen Mapunda ‘Garrincha’/Joseph
Kaniki dk 74, Shekhan Rashid, Yussuf Macho, Nteze John/Emmanuel Gabriel dk 6 na
Mark Sirengo.
Naam, hivyo ndivyo namna
ambavyo Simba SC walivyobeba ndoo sita za Kombe la Kagame na katika fainali za
mwaka huu, wanaingia kusaka ndoo ya saba ili kudhihirisha umwamba wao katika
soka ya Afrika Mashariki na Kati, nani atawazuia, Yanga tena? Bila shaka hilo ni
jambo la kusubiri na kuona.
MAXINSURE WAISAIDIA TWIGA STARS VIFAA VYA M NA UPUUZI
Na Prince
Akbar
KAMPUNI ya bima ya Maxinsure
imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga
Stars) vyenye thamani ya sh. milioni 1.3.
Vifaa hivyo ambavyo ni jezi,
bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira miwili vimekabidhiwa leo (Julai
12 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano
wa kampuni hiyo, Amisa Juma.
Akikabidhi vifaa hivyo, Amisa
amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii lakini vilevile
wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo wanajua haina mdhamini kutokana na
vipaji na uwezo ambao umekuwa ukioneshwa na wachezaji
wake.
Pia
amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu hiyo ili
iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia
kushiriki.
TEMEKE NA MWANZA NUSU FAINALI COPA COCA COLA KESHO
Na Princess
Asia
TEMEKE na Mwanza zinapambana
kesho (Julai 13 mwaka huu) katika nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Copa
Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30 asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya pili itaanza
saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na
Tanga.
Mechi ya kutafuta mshindi wa
tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa Jumapili (Julai 15 mwaka huu). Mechi
ya mshindi wa tatu itaanza saa 5 asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo
itafanyika kuanzia saa 9 kamili alasiri.
Mwanza ilipata tiketi ya nusu
fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke ikitinga hatua hiyo kwa ushindi
wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo
ulioipa Morogoro tiketi ya nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao
1-0.
CECAFA YATAJA VIINGILIO KAGAME
Mashabiki wa Yanga |
Na Princess
Asia
KIINGILIO cha chini katika
mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) vitakuwa
sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi
timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa
mtetezi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY
leo kwamba, mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa ni viti vya
bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C
sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh.
20,000.
Wambura amesema kwamba, siku
ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi
ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti
vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona
mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
Amesema timu za El Salam Wau
ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku
(Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki
kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.
CECAFA leo imetangaza
marekebisho madogo ya ratiba ya michuano hiyo na mechi ya Simba na URA ya Uganda
iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai
15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
CECAFA imefanya mabadiliko
hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja
huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana na mabadiliko hayo,
mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili jioni, mechi nyingine
Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa
Chamazi.
Pia
siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine
itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya
Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi za ufunguzi wa
mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa
kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni
Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.
SIMBA NA URA SASA JUMAPILI TAIFA KAGAME
Musonye kulia, kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah |
Na Prince
Akbar
BARAZA la Vyama vya Soka
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limerekebisha ratiba ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na sasa mabingwa wa Tanzania,
Simba SC watacheza na URA Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, badala ya
Jumatatu.
Katibu Mkuu wa CECAFA,
Nicholaus Musonye ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mechi ya Simba
imerudishwa Jumapili, baada ya fainali ya Copa Coca Cola kuhamishiwa Uwanja wa
Karume siku hiyo, tofauti na awali ilipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa hivyo
kusababisha mechi ya Simba na URA isogezwe mbele.
Kwa
mabadiliko hayo, sasa Jumapili kutakuwa kuna mechi tatu za Kagame, mechi ya
Simba na URA Uwanja wa Taifa itatanguliwa na mechi kati ya Vita Club ya DRC na
Ports ya Djibouti, wakati Chamazi Azam itamenyana na Mafunzo ya Zanzibar.
RATIBA KOMBE LA
KAGAME:
Julai 14, 2002
1
APR vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa (Saa 8
mchana)
2
YANGA vs ATLETICO Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)
Julai 15,
2002
3
AZAM vs MAFUNZO Chamazi (saa 8 mchana)
4
VITA CLUB vs PORTS Uwanja wa Taifa (saa 10
jioni)
5
SIMBA vs URA Uwanja wa Taifa (saa 10
jioni)
Julai 17, 2012
6
ATLETICO vs APR Uwanja wa Taifa (saa 8
mchana)
7
WAU SALAAM vs YANGA Uwanja wa Taifa (saa 10
jioni)
Julai 18,
2012
8
VITA CLUB vs URA Uwanja wa Taifa (saa 8
mchana)
9
PORTS vs SIMBA Uwanja wa Taifa (saa
10jioni)
Julai 19,
2012
10
ATLETICO vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa (saa 8
mchana)
11
MAFUNZO vs TUSKER Uwanja wa Taifa (saa 10
jioni)
Julai 20,
2002
12
PORTS vs URA Uwanja wa Taifa (saa 8
mchana)
13
YANGA vs APR Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)
Julai 21,
2012
14
AZAM vs TUSKER Uwanja wa Taifa (saa 8
mchana)
15
SIMBA vs VITA CLUB Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)
Julai 22m, 2012
(MAPUMZIKO)
ROBO
FAINALI
Julai 23,
2012
16
B2 vs C2
17
A1 vs C3
Julai 24, July
18
C1 vs A2
19
B1 vs A3
Julai 25, 2012
(MAPUMZIKO)
NUSU
FAINALI
Julai 26, July
20
Winner 16 vs Winner 17
Julai 26,
2012
21
Winner 18 vs Winner 19
Julai 27,
2012 (MAPUMZIKO)
FAINALI NA MSHINDI WA
TATU
Julai 28,
2012
22
Loser 20 vs Loser 21
23
Winner 20 vs Winner 21
MTAKATIFU TOM AWATEMA DAMAYO, MSUVA, NSAJIGWA KIKOSI CHA KAGAME, YONDAN NDANI
Na Prince
Akbar
KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom
Saintfiet amewaacha kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kuanzia Jumamosi wachezaji watatu
nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa
na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari mchana huu, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani,
Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba wachezaji hao watakuwa na timu ya taifa
ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa mechi ya kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.
Mtakatifu Tom anasoma majina |
“Kwa mujibu wa kanuni
natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na
Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye maandalizi
ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu
hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia
Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini
amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Amewataja wachezaji aliowateua
baada ya kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani
kuwa ni; makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David
Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus
Mbogo, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid
Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa
Assenga, Hamisi Kiiza na washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry
Tegete.
Yanga, ambao ndio mabingwa
watetezi wa Kagame, watafungua dimba na mabingwa wa Burundi, Atletico FC
Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
KIKOSI CHA YANGA
KAGAME;
Makipa; Yaw Berko na
Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul,
David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus
Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi
‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar
Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said
Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
Mtakatifu Tom akizungumza na Waandishi hapo |
No comments:
Post a Comment