Mabingwa watetezi, Yanga SC |
Na Prince
Akbar
KLABU za AS Vita Club ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na URA ya Uganda zinatarajia kuwasili
nchini Julai 12 mwaka huu kushiriki michuano ya Klabu bingwa Afrika Mashariki na
Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 14 mwaka
huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY
leo kwamba AS Vita Club ambayo iko kundi A pamoja na timu za Simba (Tanzania
Bara), Ports (Djibouti) na URA itawasili saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya
Airways ikipitia Nairobi.
Nayo URA itatua Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jioni ya siku hiyo kwa ndege ya Air
Uganda. AS Vita imepangiwa kufikia hoteli ya Rombo Green View wakati URA itakuwa
hoteli ya Royal Valentino.
Katika michuano hiyo, mabingwa
watetezi Yanga watafungua dimba na Atletico ya Burundi katika mchezo wa Kundi C
Julai 14, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati wapinzani wao wa
jadi, Simba SC waliowekwa Kundi A, wataanza na URA ya Uganda Julai 16, kwenye
Uwanja huo huo.
Wawakilishi wengine wa
Tanzania katika michuano hiyo, Azam FC wao wataanza na Mafunzo ya Zanzibar
katika mchezo wa Kundi B, Uwanja wa Chamazi, Julai 15.
MARA WAIVUA UBINGWA KIGOMA COPA COCA COLA
Na Princess
Asia
MABINGWA watetezi wa michuano
ya Copa Coca-Cola, Kigoma wameng’oka katika michuano ya mwaka huu baada ya
kulala mabao 2-1 mbele ya Mara katika mchezo uliochezwa leo (Julai 7 mwaka huu)
Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Hadi kipindi cha kwanza cha
mechi hiyo ya kutafuta tiketi ya kucheza robo fainali kinamalizika, Mara
walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 21 na George
Martime.
Kipindi cha pili kilianza kwa
nguvu ambapo Mara walifanikiwa kupachika bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa
Israel Daud. Kigoma ilipata bao lake dakika ya 63 mfungaji akiwa Hassan
Ramadhan.
Kwa
ushindi huo sasa Mara itacheza mechi ya robo fainali Julai 10 mwaka huu saa 10
jioni kwenye Uwanja wa Karume na mshindi wa mechi kati ya Morogoro na Pwani
itakayochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Tanganyika
Packers.
Nayo Temeke imepata tiketi ya
kucheza robo fainali baada ya leo kuitoa Ruvuma kwa mikwaju ya penalti katika
mechi ya 16 bora iliyofanyika Uwanja wa Karume. Hadi dakika 90 za kawaida
zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2.
Katika mikwaju ya penalti,
Temeke ambayo itcheza robo fainali Julai 10 mwaka huu saa 2 asubuhi kwenye
Uwanja wa Karume na mshindi wa mechi kati ya Mjini Magharibi na Kagera
inayochezwa leo jioni kwenye uwanja huo ilipata penalti 3 dhidi ya moja ya
wapinzani wao.
Hatua ya 16 bora inaendelea
kesho (Julai 8 mwaka huu) kwa mechi nne. Asubuhi Kinondoni itacheza na Rukwa
(Uwanja wa Karume), na Dodoma itacheza na Arusha (Uwanja wa Tanganyika Packers,
Kawe).
Mechi za jioni itakuwa
Kilimanjaro na Mwanza ambazo zitapambana kwenye Uwanja wa Karume wakati Tabora
itaumana na Tanga kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers
No comments:
Post a Comment