Na Juma Mohamed, Masasi.
HALMASHAURI ya mji wa Masasi mkoani hapa imepanga kutumia kiasi
cha sh. Bilioni 11.3 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa watumishi wake ikiwa ni
matumizi yanayotokana na kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2016/2017.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisa habari na
mahusiano wa halmashauri hiyo, Clarence Chilumba, inaeleza kuwa matumizi hayo
yanayotokana na bejeti nzima ya halmashauri hiyo iliyopitishwa ambayo ni sh.
Bilioni 19.09 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo ni sawa na asilimia 59.6 ya
bajeti yote.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, matumizi mengine yanayotokana na
bajeti hiyo ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kiasi cha bilioni
4.8 ambazo ni sawa na asilimia 25.19.
“Bajeti hii ya kiasi cha Tsh billion 19, 092,007,820.00 kwa mwaka
wa fedha wa 2016/2017 imeongezeka kutoka ile ya mwaka Jana ya Tsh.
billioni 16,954,310,834.00 2015/2016 ambayo jumla ni sawa na ongezeko la asilimia
12.6.” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, kupitia bajeti hiyo, vipaumbele Saba vimepangwa kutekelezwa
kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambavyo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa
elimu bora ya msingi na sekondari kwa kuzingatia usawa, kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama katika maeneo ya pembezoni mwa halmashauri na kuboresha
usafi wa mazingira hasa katika maeneo yenye msongamano kama Kituo cha mabasi na
sokoni.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya
Halmashauri na kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu,
kurasimisha makazi yasiyo rasmi na kuongeza kasi ya upimaji viwanja kwa ajili
ya makazi,biashara,viwanda na maeneo ya kuabudia.
“Kuongeza wigo wa ajira na kuboresha hali ya usalama wa
kijamii (socio- Protection) hasa kwa wanawake , vijana, makundi maalumu, wazee
na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na Kukarabati miundombinu ya barabara za
Halmashauri..” ilieleza.
Katika Makisio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2016/17 Halmashauri hiyo
imejikita katika kutekeleza azma ya serikali ya kutoa elimu ya msingi na
sekondari bila malipo kwa kufanya mambo kadhaa ikiwamo, kulipa likizo kwa
walimu, Kugharamia Chakula mashuleni, Kulipa gharama za uhamisho kwa walimu, Uendeshaji
wa ofisi na Gharama za mitihani.
2 comments:
Safi sana kijana ubarikiwe ktk jina la Yesu
Hongera sana Halmashauri ya mji wa Masasi..nadhani na wengine wataiga kutoka kwenu
Post a Comment