Mbunge wa Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) juu ya namna atakavyotekeleza ahadi zake |
Mbunge wa Mtwara mjini, Maftaha Nachuma (CUF) akipokea zawadi za Kimasai kutoka kwa Elizabeth Mboya. |
Na Juma
Mohamed.
WANANCHI wa
Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa wamelalamikia ukosefu wa ajira licha
ya uwepo wa kampuni kadhaa za uwekezaji, na kumtaka mbunge wa jimbo hilo
Maftaha Nachuma, kushughulikia kero hiyo kwa kuhakikisha zinapatikana fursa
nyingi kwa wazawa kuliko wageni.
Wakizungumza
juzi baada ya kumpokea mbunge huyo anayewakilisha Chama cha Wananchi (CUF), akitokea
Dodoma katika shughuli ya kuapishwa na uzinduzi wa Bunge la 11, walisema
kumekuwa na tabia ya kutoa ajira kwa wageni kuliko wenyeji wa mkoani hapa jambo
ambalo ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya viongozi kuwa ajira zitolewe kwa
wazawa zaidi ili wanufaike na uwekezaji.
Muhuzuni
Chinjaru, ambaye ni mkazi wa Kilimahewa, alisema kumekuwa na propaganda zinazozungumzwa
na baadhi ya watu kuwa ukosefu wa ajira kwa wakazi wa Mtwara ni kutokana na
kukosa elimu inayoendana na mahitaji ya sehemu husika, akidai kuwa swala hilo
sio la kweli na kwamba wananchi wengi wanaelimu na wamejifunza fani mbalimbali.
Maftaha Nachuma akipokea zawadi |
“Kwahiyo tunamuomba
Mhe. Mbunge asimamie swala la ajira, hakuna ajira Mtwara, makampuni yanakuja Mtwara
mengi sana lakini unaona vijana tunakosa ajira..utaona kampuni inahitaji vijana
wa Mtwara wapate ajira pale 100, lakini ukiangalia wanaopata ajira ni vijana 20
na 80 wote ni wakuja, sio upendeleo lakini uzawa upo bwana kila mahali..”
alisema.
Aidha,
alimtaka Mbunge kutatua kero za migogoro ya ardhi ambayo kwa zaidi ya miaka
mitatu imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi hasa wa maeneo ya Kilimahewa, Matangila
na Chame ambayo imeshindwa kutatuliwa na viongozi waliopita.
Alimtaka kuhakikisha
anainua kiwango cha elimu ambacho kinaaminika kuwa kimeshuka kutokana na hali
ya ufaulu inavyoonekana katika mitihani ya watoto wao na kwamba mwanafunzi
anamaliza kidato cha nne akiwa hajui kusoma na kuandika.
“swala la
elimu alifanyie kazi kwasababu watoto wafika darasa la tano mpaka la saba mpaka
wanamaliza kidato cha nne, hajui kuandika wala kusoma na hata kiingereza
hakijui..kwahiyo ni kero kubwa sana, mbunge asimamie vizuri na kama yeye fani
yake ya ualimu basi asimamie vizuri..” aliongeza.
Naye, Rahma
Mtipa, alisema wananchi wanaimani na mbunge huyo kuwa atatekeleza yote aliyoahidi
wakati wa kampeni zake za kuomba kura lakini zaidi ni kuwawezesha wanawake kwa
kuwapatia fursa mbalimbali zitakazowasadidia kupiga hatua kimaendeleo na kuacha
kuwa tegemezi.
“Na kama
wanavyosema elimu bure basi tunaomba iwe bure kweli ili watoto wetu wahepuke
kuwa wadhurulaji wa mitaani..atuwezeshe kuunda vikundi ili tuseme vikundi hivi vimewezeshwa
na mbunge, kwahiyo na sisi tunamuomba atuhamasishe sisi wanawake tuunde vikundi
vyetu tuweze kujiajiri wenyewe..” alisema.
Awali akizungumza
na waandishi wa habari, Mbunge huyo alisema atahakikisha anatumia fedha za
mfuko wa jimbo kutatua kero mbalimbali wanazokumana nazo wananchi katika maeneo
tofauti ikiwa ni pamoja na kujenga sehemu ya kupumzikia wauguzi katika
Hospitali ya Rufaa ya Ligula, kununua magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na
magari ya kubeba wanafunzi.
Elizabeth Mboya |
“Tunalo
tatizo la Ambulance kwenye Hospitali zetu, hatuna Ambulance kule Hospitali ya
Likombe, hatuna Ambulance Ligula (ipo) wala Mikindani, tutatumia fedha za Jimbo
na nimshukuru tu Mhe. Rais kwamba wakati anahutubia Bunge alisema safari hii
ataongeza fedha ya Jimbo ili sisi wabunge tuweze kushirikiana naye katika
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi..” alisema Maftaha.
Kuhusu
changamoto ya miundombinu mibovu iliyopo katika Manispaa ya Mtwara inayopelekea
wananchi kukumbwa na Mafuriko wakati wa mvua kubwa, alisema atajitahidi
kushirikiana na Manispaa kutatua tatizo hilo huku akiahidi kwenda kuhoji kuhusu
ujenzi wa mradi wa mfereji mkubwa wa kupeleka maji baharini kujua ujenzi wake
umefikia hatua gani.
No comments:
Post a Comment