KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex
Mgongolwa, imewaidhinisha Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuchezea Yanga katika
msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaoanza mwishoni mwa wiki.
Habari kutoka ndani ya kikao cha Kamati
hiyo, kilichomalizika hivi karibuni, zimesema kwamba pamoja na maamuzi hayo,
Yanga imepewa siku 21 kulipa dola 32,000 ambazo Simba SC ilimlipa Twite ili
ajiunge nao, lakini baadaye akaghairi na kusaini na kuhamia Yanga.
Uamuzi huu, unafuatia kikao cha pamoja
baina ya Simba na Yanga Jumatatu iliyopita kuvunjika bila kufikia makubaliano
kuhusu mustakabali wa wachezaji hao.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya
saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki
Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa
wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko
ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini
mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine
2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo,
mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali
kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi
waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema
viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage
ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite
yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi
hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia
maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba
10, mwaka huu, yaani leo.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni
Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu
yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana
Jumapili iliyopita asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo
na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata
suluhu siku iliyofuataSOURCE:BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment