Monday, September 10, 2012

OKWI AFURAHIA UWEPO WA NGASA MSIMBAZI






 
 STRAIKA namba moja wa Simba, Emmanuel Okwi ametua nchini juzi Jumapili jioni akitokea Uganda na kuitamkia Mwanaspoti maneno mazito ya moyoni kwamba alikuwa anatamani siku nyingi sana kucheza na Mrisho Ngassa.

Okwi ambaye atakuwa kwenye kikosi cha leo Jumanne cha Simba dhidi ya Azam kwenye Ngao ya Hisani, alisema hata wapinzani wampangie ukuta mzito kiasi gani akisimama kwenye fowadi na Ngassa itakuwa balaa.

"Ngassa ni mchezaji mzuri. Tokea nimekuja Tanzania kujiunga na Simba nilikuwa napenda sana staili ya uchezaji wa Ngassa, niliposikia amejiunga na Simba nimekuwa na shauku kubwa kucheza naye. Nafikiri mambo yatakuwa mazuri.

"Ni mchezaji mwenye kasi na kujua kusoma mchezo na anaweza kuendana sana na kasi yangu, nafikiri kwa sasa Simba mbele itakuwa mchakachaka.

Ngassa ni mchezaji aliyejaliwa kasi ya kipekee. Naamini tutaelewama na kuwa tishio," alisema Okwi ambaye amejibu mapigo ya kocha wa Yanga, Tom Saintfiet aliyepanga kumsimamishia ukuta wa mabeki watano.

Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara Simba na Yanga zitapambana Oktoba 3, mwaka huu, Yanga itakapojaribu kufuta kipigo cha mabao 5-0 kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet aliiambia Mwanaspoti kuwa alifuatilia kwa makini mchezo huo kwenye mkanda wa video na kukiri kuwa mabeki walikosa mbinu za kumzuia Okwi.

Mabeki ambao wamepewa kazi maalumu kumchunga Okwi ni Mbuyu Twite, Juma Abdul, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondan 'Vidic'na Oscar Joshua na pia wakati mwingine Athuman Iddi 'Chuji' akitakiwa kushuka kwenye beki kuongeza nguvu.

Okwi alitua nchini juzi saa 1:19 ya jioni akitokea Uganda alikokwenda kwa majukumu ya timu yake ya Uganda 'The Cranes' kucheza na Zambia kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2013.

"Kwanza nafurahi kusikia kocha wa Yanga amenikubali na kuamua kuniwekea watu watano kunikaba. Inawezekana wakafanikiwa kunishika, lakini kumbuka Simba si Okwi peke yake kuna wachezaji wengi wanaweza kufunga pia.

"Nikiwa mchezaji ambaye nafahamu majukumu yangu nafikiri hilo haliwezi kuninyima usingizi wa kuifunga Yanga.

Nitafanya mawasiliano mapema na wenzangu ili waweze kutumia mwanya huo kufunga," alisema Okwi aliyefunga mabao 12 kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita lakini nyuma ya John Boko wa Azam FC aliyeibuka mfungaji bora kwa kuzamisha mabao 19.

No comments: