BREAKING NEWS: NCHUNGA AJIUZULU YANGA BAADA YA KUVAMIWA USIKU WA MANANE NYUMBANI KWAKE
Nchunga akitangaza kujiuzulu leo jioni hii ofisini kwake |
Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa jana na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee.
Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
"Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema
TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:
LLOYD NCHUNGA
BIHARAGU
C/O LLOYD
ADVOCATES,
Morogoro/Bibi
TIti Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension
towers
P.BOX 75111,
Dar-Es- Salaam,Tanzania.
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA
YANGA.
Ndugu wana Habari, najua
kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa
ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita
kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao
tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu
linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa
kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba
tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale
tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote
tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani
tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja,
yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa
wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja
kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya
tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa
katika klab yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana
mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium
Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa
wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata
hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua
za mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia
mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya
marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni
ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya
promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na
kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya
shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka
mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa
yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua
tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa
sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi
ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika
kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha
miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa,
na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika
Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo
maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni
kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki
ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo
tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu
Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali
Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika
suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili
mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali,
tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata
baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa
na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti
wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea
hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI
MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na
sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza
kuubaini mapema.
Sioni mantiki katika hoja
kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu
alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi
kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na
baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na
wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji
walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa
kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha,
kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa
uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi
kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao ,
Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu
hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko
mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA
MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto
naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme
amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua
kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda
hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba
yetu.
Vile vile siko tayari kuona
klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni
kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji
kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja
na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa
mafanikio zaidi.
Nitaendelea kuwa mwanachama
mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na
nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA
MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA
BIHARAGU.
Nakala
kwa:-
Mama Fatma
Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa
taarifa
MALAWI WATUA TAYARI KUIKABILI STARS TAIFA
Stars mazoezini |
TIMU
ya taifa ya Malawi, The Flames inatarajiwa kuwasili nchini leo saa 10 jioni kwa
ndege ya Air Malawi kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars
itakayofanyika Jumamosi (Mei 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi
hiyo ni kwa ajili ya kuipima nguvu Taifa Stars kabla ya mechi yake mchujo ya
Kombe la Dunia Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika Juni 2 mwaka
huu jijini Abidjan. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko
kambini chini ya Kocha Kim Poulsen.
Malawi
itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu ambapo Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti
vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh.
20,000.
Malawi
ambayo itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu baada ya
mechi hiyo itakwenda Zanzibar ambapo Mei 28 mwaka huu itacheza na Zanzibar
Heroes.
Makocha
wa timu zote mbili Taifa Stars na The Flames kesho (Mei 25 mwaka huu) saa 5
asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za
TFF.
MAKALLA AWAKABIDHI BENDERA TWIGA STARS, WAPAA ADDIS
Twiga Stars |
TIMU
ya taifa ya soka ya miguu kwa wanawake Tanzania, Twiga Stars inayotarajia
kuondoka leo saa 11.05 jioni kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia
imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Amos Makalla.
Twiga
Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi
itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya
mchujo kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC)
zitakazofanyika Novemba mwaka huu Equatorial Guinea.
Mechi
hiyo itafanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya
marudiano itachezwa Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda
Equatorial Guinea.
Wachezaji
walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester
Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma
Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah,
Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na
Zena Khamis.
Kwa
upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha
Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa)
na Christina Luambano (Daktari wa Timu).
Twiga
Stars ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu
saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Wakati
huo huo: Ligi
ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa sasa itaanza Mei 27 mwaka huu badala
ya Mei 26 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Uamuzi wa kusogeza mbele
kwa siku kuanza kwa ligi hiyo uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 23 mwaka
huu).
Timu
23 zitachuana katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika katika vituo vya
Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika), Musoma (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume) na
Mtwara (Uwanja wa Umoja) ambapo kinatarajia kumalizika Juni 13 mwaka
huu.
Kituo
cha Kigoma kina timu za Aston Villa ya Singida, Bandari (Kagera), CDA (Dodoma),
JKT Kanembwa (Kigoma), Majimaji (Tabora), Mwadui (Shinyanga) na Pamba
(Mwanza).
Ashanti
United ya Ilala, Flamingo (Arusha), Forest (Kilimanjaro), Korogwe United
(Tanga), Nangwa VTC (Manyara), Polisi (Mara), Red Coast (Kinondoni) na Tessema
ya Temeke ziko kituo cha Musoma.
Kituo
cha Mtwara kina timu za Kurugenzi ya Iringa, Lindi SC (Lindi), Mighty Elephant
(Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Mpanda Stars (Rukwa), Ndanda (Mtwara),
Super Star (Pwani) na Tenende (Mbeya).
HISTORIA YA EURO A-Z MJUE NA MWASISI WAKE
Mabingwa watetezi Hispania |
MICHUANO ya Kombe la Mataifa
ya Ulaya, Euro 2012 inayoandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine itakuwa ni
fainali za 14 za michuano hiyo kufanyika.
Lilikuwa ni wazo la Henri
Delaunay, Katibu wa Shirikisho la Soka Ufaransa, ambaye aliibuka na wazo hilo
kwa mara ya kwanza kwenye bara hilo, mwaka 1927.
Kwa
mara ya kwanza alipata sapoti kidogo sana na michuano hiyo haikuanza hadi mwaka
1960. Hadi mwaka 1980 ni timu nne tu zilikuwa zinacheza hatua ya fainali, lakini
sasa ni timu 16 na imekuwa moja ya michuano mikubwa katika kalenda ya
soka.
Michuano yote 13 iliyotangulia
imeacha kumbukumbu kibao – BIN ZUBEIRY inakuletea wasifu wa
michuano hiyo hadi kufikia fainali za mwaka huu.
Mfungaji wa bao la ubingwa fainali zilizopita za Euro,Torres amerejeshwa kikosini dakika za mwishoni, je atang'ara tena? |
1960
MICHUANO ya kwanza ilifanyika
Ufaransa na bingwa alikuwa Soviet Union. Mabingwa hao waliongozwa na kipa wao
gwiji, Lev Yashin langoni kwenye michuano hiyo. Kipa aliyeipa England taji la
Kombe la Dunia, Gordan Banks alifunikwa na kipa huyo.
1964
Hispania kwa sasa wanatawala
katika ulimwengu wa soka, lakini mafanikio yao ya kwanza yalikuja katika Euro ya
1964, wakati walipotwaa taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani katika timu
iliyoongozwa na Luis Suarez. Kiungo huyo aling’ara kwenye michuano hiyo, ambayo
Hispania ilifunika mbaya.
1968
Michuano ya tatu ya Ulaya
ilifanyika Italia na kama ilivyokuwa Hispania 1964, pia michuano hii ubingwa
ulichukuliwa na wenyeji. England ilifika Nusu Fainali na ilifungwa na Yugoslavia
katika mechi ya kusisimua, iliyokuwa na upinzani mkali. Alan Mullery wa England
alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo.
1972
Waliokuwa mabingwa watetezi wa
Ulaya, Italia walishindwa kufuzu kuingia kwenye fainali hizo, wakiangushwa na
Ubelgiji waliokuwa wenyeji, katika Robo Fainali. Pamoja na hayo, Ujerumani
waliweza, waliwafunga wenyeji hao na kufuzu kutinga fainali za michuano hiyo,
ambako waliifunga iliyokuwa USSR mabao 3-0 na kutwaa Kombe.
1976
Michuano ‘iliyong’ara’ ya Euro
1976 taji lilichukuliwa na Czechoslovakia walioifunga Ujerumani Magharibi kwenye
fainali kwa mikwaju ya penalti mjini Belgrade. Lakini pia ilikuwa michuano
ambayo Wales ilikaribia kufuzu.
1980
Mfumo wa michuano ulibadilika
mwaka 1980, kwa timu nane kuingia kwenye fainali, lakini mwonekano wa matokeo
haukubadilika, kwa Ujerumani kutwaa ubingwa. Pamoja na hayo, kulikuwa kuna
‘maajabu’ kadhaa ikiwemo Ubelgiji iliyokuwa na vipaji babu kubwa kufika fainali,
mmojawao akiwa ni Jean-Marie Pfaff.
1984
Ufaransa walikaribia kutwaa
taji la Kombe la Dunia mwaka 1982, kabla ya kupokonywa tonge mdomoni na
Ujerumani Magharibi katika Nusu Fainali ya kukumbukwa, lakini hakukuwa na
maajabu katika ardhi ya nyumbani, wakati Wafaransa walipoongozwa na gwiji wake
Michel Platini kutwaa taji hilo.
1988
Ilikuwa ni michuano ambayo
mshambuliaji wa Uholanzi, Marco van Basten alikuwa hana wa kumfananisha naye,
kutokana na kufunga mabao ambayo yaliiwezesha nchi yake kutwaa Kombe. Pamoja na
hayo, ilikuwa habari tofauti kwa USSR, iliyoongozwa na kocha wake gwiji, Valery
Lobanovsky walipokaribia kutwaa taji.
1992
Denmark haikufuzu kwenye
fainali hizo nchini Sweden, lakini walipata nafasi kutokana na Yugoslavia kuwa
katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, hivyo kushindwa kushiriki. Na vijana hao
wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, wakiifunga Ujerumani kwenye
fainali. Kim Vilfort, ambaye alifunga kwenye fainali alielezea namna ambavyo
Denmark walikuwa na maandalizi mazuri kabla ya fainali hizo.
1996
Euro 96 – michuano ambayo
ilipewa jina soka imerejea nyumbani. England ilifika Nusu Fainali, lakini
ikafungwa na Ujerumani kwa mikwaju ya penalti. Ujerumani ilifanikiwa kutwaa taji
hilo kwa kuifunga Czechs Uwanja wa Wembley. Mshambuliaji wa England, Alan
Shearer alifanya vitu adimu sana kwenye fainali hizo.
2000
England ilifanikiwa kuifunga
Ujerumani, lakini hawakufanikiwa kufuzu kutoka kwenye kundi lao na vijana wa
Kevin Keegan walirejeshwa nyumbani kimaajabu. Ufaransa walitwaa Kombe la Dunia
nyumbani kwao mwaka 1998 na wakadhihirisha ubabe wao kwa kutwaa taji la Ulaya
pia kwenye fainali zilizoandaliwa kwa pamoja na Ubelgiji na Uholanzi. Kiungo
Emmanuel Petit aliyeng’ara kwenye michuano hizo alielezea siri ya mafanikio ya
nchi yao.
2004
Euro 2004: Ugiriki walipoibuka
mabingwa. Ilikuwa unakwenda kuwa mwaka wa Ureno, katika fainali ambazo walikuwa
wenyeji, lakini wakafungwa na Ugiriki 1-0 kwenye fainali. Cristiano Ronaldo
aliumizwa sana na matokeo hayo, kwani ulikuwa mwaka wa kufurahia mafanikio na
timu yake ya taifa, lakini ikashindikana.
2008
Katika michuano iliyoandaliwa
kwa pamoja na Uswisi na Austria, ambayo ilifana, Hispania waliibuka mabingwa
baada ya miaka 44 ya kusubiri taji la kimataifa. Hispania waliifunga 1-0
Ujerumani katika fainali, bao pekee la Fernando Torres dakika ya 33 na sasa
wanaingia kwenye fainali za mwaka huu kutetea taji, wakiwa pia mabingwa wa
dunia. Je, wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
MENEJA KILIMANJAREO ABAINI SIMBA NA YANGA ZA TANO DUNIANI, MUZIKI WETU UNAUZA ZAIDI NJE
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Geroge Kavishe akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati akitambulisha kampeni ya 100% tz Flava leo katika hoteli ya New Africa. |
UCHUNGUZI uliofanywa na Meneja
wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe umemuonyeaha mambo mawili makubwa kuhusu
Tanzania- kwanza ni muziki wa nchini kuwa bidhaa inayonunuliwa zaidi nje na pili
Simba na Yanga kuwa kwenye tano ya wapinzani wa jadi jadi dunaini.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa kampeni ya 100% TZ Flava, iliyofanyika kwenye hoteli ya New Africa
mchana huu mjini Dar es Salaam, Kavishe alisema kwamba mbali na Simba na Yanga
kuwa kwenye tano bora ya wapinzani wa jadi duniani, pia zinashika nafasi ya pili
Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Executive Solutions, waratibu wa kampeni ya 100% tz Flava akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya New Afrika leo |
Akiizungumzia kampeni hiyo,
Kavishe alisema kwamba itatembea kwa miezi sita na itapambwa na mambo mengi
mazuri ya kujivunia kuhusu Tanzania.
Alisema kampeni hiyo itakuwa
na sehemu tatu, ambayo ni kwanza kuzindua alama ya kampeni hiyo, 100% tz Flava-
tusherehekee kilicho chetu.
“Kwenye hii kampeni,
imetengenezwa ili kumpa mteja raha, lakini lazima iache ujumbe, ambao ni furahia
kilicho chetu. Kampeni inahusu muziki wetu, tumetumia picha za wanamuziki
wetu,”alisema Kavishe na kuongeza;
“Kwanza nataka niwaambie kama
mlikuwa hamjui, bidhaa ambayo inauzika nje zaidi kwa sasa hapa Tanzania, ni
muziki wetu, watu wa nje ya nchi wananunua sana muziki wetu na ndio bidhaa
inayoongoza kuuzika nje ya nchi,”alisema.
Alisema pia wametumia picha za
Simba na Yanga, klabu ambazo zinadhaminiwa na bia hiyo. “Hakuna nchi duniani,
klabu zake za ndani zina ukubwa na uzito ambao Simba na Yanga zinao. Mvuto wa
Simba na Yanga duniani ni wa tano kwa ukubwa. Na kwa Afrika wa pili,”alisema
Kavishe.
Aidha, Kavishe pia alisema
katika kampeni hizo, pia wametumia lugha za mtaani, ambazo pia ni fahari ya
Tanzania kwa mfano piga tarumbeta, neno linalowakilisha kunywa bia kwa kutumia
chupa moja kwa moja na kula bata, yaani kula raha.
Mapema, Kavishe alisema
kampeni hii ni mwendelezo wa kampeni ya Kili Jivunie Utanzania, ambayo amesema
kwa kiasi kikubwa imefanikiwa.
“Bia ya Kilimanjaro Lager ipo
tangu mwaka 1954. Ilipotea wakati wa harakati za uhuru na ikarudi mwaka 1966
kama Kilimanjaro Premium Lager na hadi leo tunasukumana nayo, tunabadilisha
nembo na kadhalika, lakini bado tupo nayo,”alisema.
Kavishe alisema bia kama
maisha ya mwanadamu, inazaliwa, inakuwa, inakomaa na inakufa- lakini kudumu kwa
bidhaa sokoni kunatokana na kampeni inayofanywa kuibakiza sokoni.
Alisema uchunguzi walioufanya
mwaka 2009 ili kutambua kwa nini bia ya Kilimanjaro ipo sokoni na wateja
wanaionaje, uliwaonyesha kwamba bia hiyo inakubalika mno mbele ya Watanzania.
Waandishi wakisikiliza kwa makini |
“Sisi tulikuwa tunajua ni
Safari Lager, tukataka kujua bia ipi inakubalika zaidi kama ya Kitanzania,
majibu yaliyokuja hatukukubaliana nayo. Hatukuamini, walisema ni Kilimanjaro
Premium Lager,” alisema.
Kavishe alisema Safari Lager
iko sokoni tangu mwaka 1977 na ilikuwa inachukuliwa kama ni bia ambayo asili
yake ni Tanzania kutokana na alama ya kanyumba ka msonge, lakini wateja wao
wakasema ni Kilimanjaro kwa sababu ya alama ya mlima Kilimanjaro, mnyama Twiga
na kufanya vitu ambavyo vinawagusa Watanzania moja kwa moja
No comments:
Post a Comment