Kamati ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ilikutana jana (Septemba 25 mwaka
huu), kusikiliza rufani iliyowasilishwa mbele yake na warufani Mussa H.
Mahundi, Abou Sillia na Alex Mgongolwa,
dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA),
iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa IRFA
uliofanyika Septemba 8 mwaka huu Mufindi, Iringa, na kuomba uchaguzi huo
ufanyike upya kwa kuendeshwa na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, baada ya kupitia maelezo ya
warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa, rufani
iliyowasilishwa mbele yake na Mahundi, Sillia na Mgongolwa ilikosa sifa ya kuwa
rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 8(2),
Ibara ya 21(3) na 24(2).
Kwa kutozingatia matakwa
ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa
rufani hiyo.
Kamati ya Uchaguzi ya
TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya IRFA kuchukua hatua dhidi ya Abuu Changawa,
kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya
28(6) kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa IRFA siku ya uchaguzi.
SHUKRANI KWA WADAU
SERENGETI BOYS
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru wadau waliofanikisha kwa njia mbalimbali,
ziara ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys),
iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Wadau hao ni Chama cha
Mpira wa Miguu Mbeya Mjini (MUFA) chini ya Mwenyekiti wake Suleiman Haroub,
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA), Stanley
Lugenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na Chama cha Mpira wa
Miguu
Wilaya ya Njombe (NDFA).
Wengine ni Chama cha
Mpira wa Miguu Wilaya ya Makambako (MDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Morogoro (MRFA), na klabu za Mbozi United, Kyela United, Tanzania Prisons na
Mbeya City.
Serengeti Boys
inaendelea na kambi yake jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya
mchujo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, dhidi ya
Misri itakayochezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
KAMSHINA MMOJA AONDOLEWA
KWENYE LIGI
Kamati ya Ligi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 25 mwaka
huu), kupitia ripoti za mechi 21 za Ligi Kuu ya Vodacom ambazo zimeshachezwa
mpaka sasa, na kuzifanyia uamuzi wa kikanuni ikiwemo kumuondoa Kamishna mmoja.
George Komba aliyekuwa
Kamishna kwenye mechi namba 20 kati ya Simba na Ruvu Shooting, ameondolewa
kwenye orodha ya makamishna wa ligi, kutokana na upungufu uliojitokeza katika
ripoti yake.
Klabu ambazo zimeandikiwa
barua za onyo ni African Lyon kwa kwenda uwanjani na jezi tofauti na zile
ilizoonesha kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (pre match meeting), Mtibwa
Sugar kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake wakati wa mechi, na
Ruvu Shooting kwa ushangiliaji uliopita kiasi kwenye mechi yao dhidi ya Simba.
Kamati pia imethibitisha
kadi nyekundu ya Emmanuel Okwi kwa kumpiga kiwiko Kessy Mapande wa JKT Ruvu,
hivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(1) anakosa mechi tatu na kulipa faini ya sh.
500,000. Mchezaji huyo atakosa mechi namba 20, 27 na 80.
Kwa upande wa waamuzi,
Ronald Swai ameandikiwa barua ya onyo kutokana na upungufu alioonesha kwenye
mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting, iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Mchezaji Faustin Lukoo wa Polisi Moro, ambaye kwa mujibu wa ripoti ya mwamuzi aliyemtoa nje kwa kadi nyekundu, alimtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi dhidi ya African Lyon na Katibu wa Oljoro JKT aliyemwaga maji kwenye chumba cha timu ya Polisi Moro, masuala yao ni ya kinidhamu, hivyo yamepelekwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
Kwa klabu ambazo timu zao mpaka sasa zinacheza mechi bila kuwa na logo ya mdhamini, suala hilo limepelekwa kwa wadhamini Vodacom kwa vile wenyewe ndiyo wanaogawa vifaa hivyo.
TENGA KUKUTANA NA
WAANDISHI KESHO SAA 6
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga atakutana na waandishi wa habari kesho (Septemba 27 mwaka
huu), saa 6 kamili mchana. Mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
TFF.
No comments:
Post a Comment