Thursday, April 12, 2018

WAHAMIAJI HARAMU 23 WAKAMATWA KATIKA NYUMBA ZA WAGENI MTWARA



Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Lukas Mkondya, akiongea na waandishi wa habari juu ya matukio matatu yaliyojitokeza mkoani humo, ambayo ni Kukamatwa kwa Wahamiaji haramu 23, Kukamatwa kwa watuhumiwa 13 wa wizi wa Pikipiki pamoja na kushikiliwa kwa watuhumiwa Tisa wanafunzi wa chuo cha Sella Maries tawi la Mtwara kwa makosa ya kuhamasisha maandamano mitandaoni pamoja na lugha za kumkshifu Rais.



MTWARA

Wahamiaji haramu 23 ambao ni raia wa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi na Rwanda wamekamatwa mkoani Mtwara wakiwa wamehifadhiwa katika nyumba za kulala wageni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara Lukas Mkondya, alisema baada ya kuahoji watuhumiwa hao, wote wamekiri kusafirishwa na mfanyabiashara raia wa jijini Dar es Salaam ambaye bado hajakamatwa aliyedhamiria kuwapeleka nchini Ufaransa.

“Baada ya kupata taarifa hizo askari walikwenda kufanya upekuzi katika nyumba za wageni, na kufanikiwa kuwakamata hao wahamiaji 23 ambao wameingia nchini kwetu kinyume cha sheria..katika mahojiano hayo, wahamiaji hao wametoka katika nchi zifuatazo..kuna wahamiaji wametoka nchi ya Kongo au Zaire, kuna wengine wametoka nchi ya Rwanda na wengine ni raia wa Burundi.” Alisema Mkondya.

Katika tukio lingine, jeshi hilo limewakamata watu 13 kutoka katika kijiji cha Chikongo wilayani Tandahimba kwa tuhuma za kuhusika na wizi sugu wa pikipiki katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Miongoni mwa Pikipiki zilizokamatwa na jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara katika kijiji cha Chikongo wilayani Tandahimba, baada ya kufanyika msako wa kuwabaini watu wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa pikipiki hizo.

Aidha, jeshi hilo linawashikilia wanafunzi Tisa wa chuo kikuu kishiriki cha Stella Maries mkoani Mtwara ambao wanatuhumiwa kuhamasisha maandamano pamoja na kuchapisha lugha za kumkashifu Rais.






No comments: