Mafunzo SC |
Na Ally
Mohamed, Zanzibar
PAZIA la
Ligi Kuu Zanzibar, limefunguliwa jana kwa mechi mbili kuchezwa katika viwanja
viwili tofauti, kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, Mabaharia wa KMKM
walikutana na Mafunzo, ambapo mechi hiyo imemalizika kwa Mafunzo kuchomoza na
ushindi wa bao 1-0, bao hilo pekee likipatikana katika dakika ya tano, mfungaji
Mohammed Abdulrahman.
Huko
kisiwani Pemba nako ilipigwa mechi moja ikiwakutanisha mabingwa watetezi wa ligi
hiyo, Super Falcon na Chipukizi ambapo kwa mara nyengine tena Super Falcon ambao
ni wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, wamefungwa
2-0.
Hii ni mechi
ya sita mfululizo Super Falcon wanapokea kipigo, wakianzia katika michuano ya
BancABC Super 8, ambapo walipoteza mechi zao zote 3 za hatua ya makundi, kabla
ya kukubali kipigo cha 3-1 kutoka kwa Jamhuri katika mechi ya Ngao ya Jamii
iliyochezwa Septemba 1, mwaka huu Uwanja wa Amaan na juzi wakicheza na Coastal
Union ya jijini Tanga katika mechi ya kirafiki, mchezo uliochezwa Uwanja wa
Ngome, Fuoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja walifungwa
2-0.
Ligi hiyo
inatarajia kuendelea tena leo kwa mechi mbili, katika Uwanja wa Amaan kisiwani
unguja, Klabu ya Malindi ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni SC watacheza
na timu iliyopanda daraja msimu huu, Bandari na katika Uwanja wa Gombani,
kisiwani Pemba washindi wa pili wa ligi iliyopita, Jamhuri wakicheza na Duma,
mechi zota zinatarajiwa kuanza saa 10:30 jioni.
Ligi kuu ya
Zanzibar, ambayo msimu huu inafahamika kwa jina la Zanzibar Grand Malt Premier
League kutokana na mdhamini kinywaji cha Grand Malt, inashirikisha timu 12, huku
timu 8 zikitoka kisiwani Unguja na timu 4 zikitoka kisiwani Pemba, timu
zinazotoka kisiwani Unguja ni Bandari, Chuoni, KMKM, Mafunzo, Malindi, Mundu
ambao wamenunua daraja kutoka kwa Miembeni United, Mtende iliyopanda daraja
msimu huu na Zimamoto.
Kwa upande
wa kisiwani Pemba ni Chipukizi, Duma, Jamhuri na Mabinwa watetezi, Super Falcon.
SOURCE:BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment