Tuesday, May 29, 2012

ANGETILE OSIAH ANG'ATUKA YANGA SC

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah ametangaza kujivua nafasi yake ya ujumbe wa kamati ya uchaguzi ya klabu ya soka ya Yanga.
Osiah amesema kuwa analazimika kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za shirikisho hilo na atawasilisha barua kwa katibu mkuu wa Yanga, Mwesiga Selestine.
Alisema kuwa licha ya kuteuliwa muda mrefu kushika wadhifa wa ukatibu wa TFF, alishindwa kuwasilisha barua ya kujitoa katika kamati ya uchaguzi kutokana na kuingwa na majukumu ndani ya shirikisho hilo.
“Nimelazimika kufanya hivyo kwani kwa sasa Yanga inahitaji kufanya uchaguzi mdogo kwa lengo la kuziba nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi walioachia ngazi Yanga hivyo inabidi nafasi yangu ijazwe ili kamati iweze kuendesha mchakato wake kikamilifu,”alisema.
TFF kupitia kamati ya uchahizi iliyo chini ya mwenyekiti wake Deogratius Lyato iliiagiza kamati ya uchaguzi ya Yanga chini ya mwenyekiti wake Jaji John Mkwawa ifanye uchaguzi wake kuziba nafasi za nane za viongozi waliojiuzulu na mjumbe mmoja aliyefariki dunia.
Hatua hiyo inafuati hivi karibuni kujiuzulu kwa mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga kutokana na shinikizo la baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la Wazee waliomtaka kufanya hivyo kwa madai ya kutoiletea mafanikio klabu na hatimaye kupokwa ubingwa wao wa ligi kuu bara ulioenda kwa Simba na wao kuishia nafasi ya tatu.
Awali makamu mwenyekiti wa Yanga Davis Mosha alitangaza kujiengua katika uongozi miezi michache baada ya kuchaguliwa kwa madai ya kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe wa kamati ya utendaji, Theonest Rutashoborwa alifariki dunia.
Kama hiyo haitoshi, wajumbe wengine walioachia ngazi Yanga ni pamoja na Seif Ahmed, Mbaraka Igangula, Mzee Yusuf, Ally Mayay, Charles Mgondo na Mohammed Bhinda.

KIM:SIKUTEUA WACHEZAJI STARS KWA UPENDELEO


KOCHA wa Taifa Stars Kim Poulsen amekana kupendelea katika uteuzi wa wachezaji wa kikosi hicho na kusema kwamba alichagua wachezaji kutokana uwezo na sifa walizonazo na si kuangalia ni mchezaji wa timu gani.
Alisema nashangazwa na maalalamiko ya baadhi ya wadau wa soka ambao wamekuwa wakielekeza shutuma hizo ambazo hazina ukweli wowote.
Baadhi ya wadau walimekuwa wakimlalamikia kocha huyo kutokana na kuchagua nyota wengi kwenye kikosi hicho wakitokea klabu ya Simba huku mahasimu wao Yanga, akiteua mchezaji mmoja tu.
Aliongeza kuwa kikosi chake ambacho kinajiandaa na mchezo wake wa kuwania kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast kitaenda bila ya nyota wake Nurdin Bakari na Thomas Ulimwenguni ambao walipata majeruhi wakati wa mazoezi yao na kusema kuwa watabaki wakijinoa kabla ya kuungana na wenzao watakaporudi ili kujiandaa.
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Ivory Coast utakaopigwa juni 2 huko Abdjan, Paulsen alisema kikosi chake kinaiheshimu kutokana na kuwa na wachezaji nyota wengi wenye uwezo kisoka kwa ambao wanacheza ligi za ulaya wakiwemo Didier Dragba, Solomon Kalou, Yaya Toure, Kolo Toure na wengineo.
Alisema pamoja na hilo hawaiogopi zaidi ya kuwataka wachezaji wa Stars kutambua hawana tofauti na Ivory Cost isipokuwa ni mbinu tu za hapa na pale ambazo anaamini kwa uwezo walichonacho wachezaji wa Stars wanaweza kushinda.na mechi yao dhidi ya Gambia.

Wachezaji wengine waliopo Stars ni pamoja na makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar). Mabeki: Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Jonas Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba- U20), Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu- U20).
Washambuliaji ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan Singano (Simba-U20), Simon Msuva (Moro United- U20), Haruna Moshi (Simba) na John Bocco (Azam).

No comments: