YANGA SC ya
Dar es Salaam leo imechapwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro kwenye Uwanja
wa Jamhuri mjini hapa.
Hadi
mapumziko, tayari Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani
na beki wa kati, Dickson Daudi dakika ya 11 akiunganisha kwa kichwa kona ya beki
wa kushoto Malika Ndeule.
Bao hilo
lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambao walishindwa kumuweka ulinzi
mchezaji mrefu kuliko wote, Daudi.
Yanga
walijaribu kutaka kusawazisha, lakini mipango yao ilikuwa hafifu na kujikuta
wakiendelea kushambuliwa na dakika ya 43, Hussein Javu aliwainua tena vitini
mashabiki wa Simba waliokuwa wakiwashangilia kwa nguvu leo kwa kufunga bao la
pili.
Kwa ujumla
kipindi cha kwanza, Yanga walicheza ovyo- pasi zao nyingi zilikuwa hazifiki,
walishindwa kuwabana wapinzani wao na zaidi Haruna Niyonzima alishindwa
kuiongoza vema timu, jambo ambalo lilifamnya kiungo mkabaji Athumani Iddi
‘Chuji’ kupanda mbele zaidi kusaidia, ingawa
haikusaidia.
Mabeki
wawili wa kati wa Mtibwa, Daudi na Salvatory Ntebe waliwadhibiti vema
washambuliaji wawili wa Yanga, Hamisi Kiiza na Saidi Bahamnuzi katika dakika 45
za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha
pili, Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet alianza kwa mabadiliko akiwatoa
Frank Damayo na David Luhende na kuwaingiza Simon Msuva na Stefano na Mwasyika,
lakini bado ukuta wa Mtibwa ulikuwa mgumu mbele ya Watoto wa
Jangwani.
Katika
kuongeza mashambulizi, Mtakatifu Tom alimtoa beki Mbuyu Twite na kumuingiza na
mshambuliaji Didier Kavumbangu, lakini bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwa
Yanga.
Dakika ya 86
Hussein Javu aliifungia Mtibwa bao la tatu kwa shuti la mbali, wakitoka
kushambuliwa na kufikia hapo, Yanga ‘walikufa’ na mashabiki wao wakaanza kuuacha
Uwanja wa Jamhuri.
Huu unakuwa
mchezo wa pili kwa Yanga tangu kuanza kwa ligi wakiwasononesha mashabiki wao,
baada ya mechi ya kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye
Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Waswahili
wanasema siku ya kufa nyani, miti yote huteleza, Hamisi Kiiza alipaisha mkwaju
wa penalti dakika ya 89, baada ya Daudi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, , Mbuyu
Twite/Kavumbangu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’,
Frank Domayo/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David
Luhende/Stefano Mwasyika.
Mtibwa
Sugar; Shaaban
Hassan Kado, Malika Ndeule, Issa R Issa, Dickson Daudi, Salvatory Ntebe, Shaaban
Nditi, Jamal Mnyate/Babu Seif Ally, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban Kisiga
‘Malone’ na Vincent Barnabas/Ally Mohamed 'Gaucho'.
No comments:
Post a Comment