Tuesday, May 29, 2012


MAMA VUVUZELA WA MASHAUZI AIPUA NGOMA MPYA KALI KINOMA

MWIMBAJI nyota wa kundi la Mashauzi Classic, Aisha Othman 'Mama Vuvuzela' ameibuka na wimbo mpya uitwao, La Mungu Halina Mwamuzi ambao unatarajiwa kuanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya Radio nchini wakati wowote kuanzia sasa.
Aisha, ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, wimbo huo umetungwa na Thabit Abdul ambaye ni Mkurugenzi wa bendi hiyo na umerekodiwa katika studio za Sound Crafters, chini ya mtaalamu Enrico.
"Wapenzi na mashabiki wangu na mashabiki wa Mashauzi Classic na wapenzi wa Taarabu kwa ujumla, wakae mkao wa kula kupokea kitu kipya kitamu, mtoto nimetulia humo ndani, nimefanya mambo makubwa,"alisema Aisha.

ALIYEFUKUZWA TWANGA PEPETA ATUA KIFALME MASHUJAA BAND

Chaz Baba kulia akimwambia Martine karibu sana. Kushoto ni King Dodo La Bouche, mwasisi wa Mashujaa Band


Martine katikaqti, King Dodoo kulia na Chaz Baba kushoto katika utambulisho wa Meneja huyo mpya asubuhi hii

MENEJA aliyefukuzwa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Martine Sospeter leo ametangazwa rasmi kuwa Meneja mpya wa bendi ya Mashujaa- ikiwa ni siku mbili tu afukuzwe katika bendi yake ya awali iliyompatia umaarufu.
Martine, ametambulishwa asubuhi hii katika mgahawa wa Business Park, Victoria, Dar es Salaam. Pamoja na utambulisho huo, Martine amekanusha madai ya Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka kwamba ametoweka na fedha za bendi hiyo.
Katika taarifa yake ya kumfukuza kazi Martine, Asha alidai Meneja huyo alichukua fedha kwa wateja kwa ajili kuwakodisha bendi- hivyo akamtaka azirejeshe. “Sijachukua fedha yoyote popote, sina deni, kama anadai nina deni, alete ushahidi,”alisema Martine.
Martine alisema kwamba kwa muda mrefu amekuwa akitakiwa na bendi ya Mashujaa kwa dau zuri, lakini amekuwa akikataa kutokana na jinsi anavyomheshimu Asha Baraka, lakini anasikitika amefukuzwa kwa kudhalilishwa.
“Amenikfukuza na kunitolea maneno ya kashfa mimi wakati nipo na bendi yake ziarani mikoani, imeniuma sana. Ila bado nitaendelea kumuheshimu Asha Baraka kama dada yangu na mtu ambaye amenifikisha hapa.”alisema Martine.
Sababu kubwa aliyoitaja Asha ya kumfukuza Martine ni kuwarubuni wanamuziki wa Twanga Pepeta kuhamia kwa wapinzani, Mashujaa. Miongoni mwa wanamuziki wa Twanga waliohamia Mashujaa ni mwimbaji hodari, Charles Baba.

TETESI ZA USAJILI BARA: NYOSSO, UHURU, JABU KUTUA YANGA



Nyosso
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam inataka kuchukua wachezaji watatu kutoka Simba, ambao mikataba yao inaisha karibuni- hao ni mabeki Juma Jabu, Juma Nyosso na kiungo Uhuru Suleiman.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya watu ambao wamepewa jukumu la kufanya usajili Yanga, zimesema kwamba wachezaji wote hao wamekwishafanya nao mazungumzo na wamefikia mwafaka, ingawa bado hawajasaini.
“Fedha itatoa haraka, watasaini, kwa sababu tunatengeneza timu ya kucheza Kombe la Kagame,” kilisema chanzo chetu kutoka Yanga.
Aidha, Yanga pia ipo kwenye mpango wa kusajili washambuliaji wawili ‘pacha’ wa timu ya taifa ya Rwanda, Meddie Kegere na Olivier Karekezi, ambao waling’ara sana kwenye Kombe la CECAFA Challenge mwaka jana Dar es Salaam, Amavubi ikifungwa na The Cranes kwenye fainali.
“Mazungumzo na hao wachezaji wa Rwanda yalikwishafanyika siku nyingi na tumekuwa tukiwasiliana nao kwa kipindi chote hiki, mambo yanaendelea vizuri na watakuja hapa,”kilisema chanzo kutoka Yanga.
Kiunganishi kuu cha wachezaji wa Rwanda na Yanga ni mfanyabiashara, Abdallah Ahmed Bin Kleb ambaye amewekeza nchini humo. Bin Kleb ndiye aliyemsajili kwa fedha yake, kiungo ‘baab kubwa’ wa APR, Haruna Niyonzima msimu uliopita.
Fungu la usajili wa wachezaji Yanga linatoka kwa mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji ambaye ameteua Kamati Maalum kusimamia Usajili pamoja na ajira ya kocha mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic aliyetupiwa virago ‘kiaina’.
Uhuru

Jabu
Baaada ya Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga kujiuzulu, klabu hiyo sasa ipo chini ya Baraza la Wadhamini na Sekretarieti ya klabu chini ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame na wamepania kutetea taji hilo, ili kupoza hasira za mashabiki wao baada ya msimu mbaya uliopita, wakipoteza ubingwa wa Ligi Kuu, sambamba na kukosa hata nafasi ya kucheza michuano ya Afrika, ikiwa ni pamoja na kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu.

Monday, May 28, 2012

BOBAN AWEKEWA MASHINE YE ECG KIFUANI


MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars na Simba, Haruna Moshi Boban, amefanyiwa uchunguzi wa kiafya na kuwekewa kifaa maalumu kifuani.
Gazeti la Mwanaspoti leo limeandika kwamba Boban ambaye ni Nahodha Msaidizi wa Simba, aliwekewa kifaa hicho kwa muda wa dakika 24 kutokana na kusumbuliwa na tatizo la presha ya kushuka iliyogunduliwa na daktari wa Simba hivi karibuni.
Daktari wa Stars, Mwanandi Mwankemwa, ameliambia Mwanaspoti akisema: "Kutokana na tatizo la kuzimia lililomkuta Boban alipokuwa Kinshasa.
Tumemwekea mashine maalum kwenye moyo katika sehemu ya kifuani, hii ni kwa ajili ya kuchunguza moyo wake kama una tatizo.
"Kifaa hicho kinaitwa ECG na hufanya kazi sawa na mishipa ya moyo (PQ Waves) na atakaa nacho kwa muda wa masaa 24."
Kifaa hicho aliwekewa juzi Alhamisi saa nne asubuhi na kiliondolewa jana Ijumaa muda huo.
Mwanandi amesema, katika muda huo, mashine hiyo itagundua kama kuna tatizo lolote kwa mchezaji huyo.
Akiwa na kifaa hicho, Boban alishindwa kufanya mazoezi na Taifa Stars na kuungana na Nurdin Bakari ambaye anasumbuliwa na nyama za paja.
Nurdin amepewa siku saba kwa ajili ya mapumziko na Thomas Ulimwengu ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu wa kulia, alifanya mazoezi mepesi.
Mwanandi ameeleza kuwa suala la Boban kuchezea Stars litategemea majibu ya mashine hiyo.
Lakini jana Ijumaa mchana, Mwankemwa alipoulizwa alisema wanasubiri majibu ya kipimo hicho kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Hindu Mandal.
Akizungumzia suala hilo, Boban alisema: "Hali yangu kiafya ni nzuri, sijisikii tatizo lolote, zaidi ya mkono huu unaonisumbua (anaonyesha katika mkono wake wa kulia ambao una uvimbe kwenye kidole cha kati).
Stars inajipima nguvu na Malawi leo Jumamosi ili kujiandaa na mechi dhidi ya Ivory Coast ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.
Boban alizidiwa alipokuwa Kinshasa akijiandaa kurudi Dar es Salaam baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mafisango. Yeye na Mafisango walikuwa marafiki wa karibu.

No comments: